Uganda: Besigye kuhukumiwa katika mahakama ya kiraia
18 Februari 2025Wakati utawala wa Uganda ukikabiliwa na shinikizo la kumwachia huru mwanasiasa mashuhuri wa upinzani Kizza Besigye, afisa mmoja wa serikali amesema mwanasiasa huyo atashtakiwa katika mahakama ya kiraia badala ya ile ya kijeshi.
Besigye, mgombea urais mara nne katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki, alitoweka mwezi Novemba mwaka jana katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, na kuonekana siku chache baadaye mbele ya mahakama ya kijeshi katika mji mkuu wa Uganda, Kampala.
Soma: Mke wa Besigye asema mashitaka ya mumewe ni "uzushi"
Mwanasiasa huyo alianza pia mgomo wa kula wiki iliyopita na siku ya Jumapili alikimbizwa hospitali baada ya hali yake ya afya kuzorota. Besigye ambaye amekuwa mkosoaji wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni, anakabiliwa na mashtaka kwenye mahakama ya kijeshi yanayojumuisha umiliki wa silaha kinyume cha sheria. Washirika wake wamesema mashtaka hayo yamechochewa kisiasa.