Ufaransa yapinga wazo la Israel la kutwaa maeneo ya Gaza
22 Machi 2025Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot amesema Ufaransa inapinga aina yoyote ya unyakuzi wa ardhi ya Palestina, iwe katika Ukanda wa Gaza au kwenye Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Hayo ni baada ya Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz kutishia hapo jana kutwaa baadhi ya maeneo ya Gaza na kuyajumuisha kama himaya ya Israel, ikiwa wanamgambo wa Hamas hawatowaachia huru mateka waliosalia.
Akiwa katika mji wa mashariki mwa Ufaransa wa Dijon, Barrot amesema mustakabali wa eneo hilo utawezeshwa na suluhu la mataifa mawili.
Hayo yanaarifiwa wakati Israel imezidisha mashambulizi yake huko Gaza na kusambaratisha hali ya utulivu iliyoshuhudiwa katika eneo lililokumbwa na vita, jeshi la Israel limewataka hapo jana wakaazi wa maeneo ya Al-Salatin, Al-Karama na Al-Awda kusini mwa Gaza kuyahama makazi yao kabla ya mashambulizi makali yanayotarajiwa.
Jeshi la Israel limesema limefanikiwa usiku wa Ijumaa katika mji wa kusini wa Ashkelon kudungua makombora mawili yaliyofyetuliwa na Hamas iliyodai kuwa shambulio hilo ni jibu kwa mauaji yanaoendelea dhidi ya raia huko Gaza.
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz ameonya kwamba watazidisha mashambulizi ya angani, majini na ardhini hadi mateka wote watakapoachiliwa na kushuhudia Hamas ikishindwa, na kusisitiza kuwa watatumia shinikizo zote iwe za kijeshi na kiraia.
Soma pia: Israel yatanua kampeni yake ya kijeshi Gaza
Wimbi hilo jipya la mashambulizi ya Israel huko Gaza linafanyika kwa uratibu wa serikali ya rais Donald Trump wa Marekani, hatua iliyoibua ukosoaji mkubwa. Uturuki imelaani kile ilichosema ni shambulio la "makusudi" la Israel kwenye hospitali iliyojengwa na nchi hiyo huko Gaza, huku rais wa Urusi Vladimir Putin akielezea "kusikitishwa" na mashambulizi mapya ya Israel.
Netanyahu akabiliwa na shinikizo ndani ya Israel
Kwa siku kadhaa sasa, maelfu ya watu wamekuwa wakiandamana mjini Jerusalem wakimtuhumu waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa kuanzisha tena operesheni za kijeshi bila kujali usalama wa mateka. Baadhi wamekuwa wakimtaka ajiuzulu kwa kushindwa katika jukumu lake la kuwalinda waisrael wote wakimtuhumu pia kutaka kuyumbisha demokrasia kwa faida zake za kisiasa ili tu asalie madarakani.
Hata Rais wa Israel Isaac Herzog alielezea wazi wasiwasi wake kuhusu hatua ya serikali ya Netanyahu akisema haiwezekani kuanzisha mapigano na wakati huohuo uendelea na mchakato wa kuwarejesha nyumbani mateka karibu 58 ambao bado wanashikiliwa na kundi la Hamas.
Mazungumzo ya amani yalivunjika wakati Israel ilipokataa kuanzisha awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo vipengee vyake viliitaka Israel kuviondoa kabisa vikosi vyake huko Gaza na Hamas kuwaachia mateka wote waliosalia.
(Vyanzo: Mashirika)