Ufaransa yakabidhi fuvu la mfalme Toera
26 Agosti 2025Ufaransa leo imerejesha nchini Madagascar mafuvu ya watu watatu waliouwawa wakati wa enzi za ukoloni. Miongoni mwa mafuvu yaliyorejeshwa ni la mtu anayeaminika alikuwa mfalme wa Madagascar aliyekatwa kichwa na wanajeshi wa Ufaransa wakati wa mauaji ya halaiki yaliyofanyika karne ya 19.
Mafuvu ya mfalme Toera na watu wengine wawili kutoka jamii ya kabila la Sakalava yalikabidhiwa katika sherehe iliyofanyika kwenye wizara ya utamaduni ya Ufaransa.
Madagascar imekaribisha kurejeshwa kwa mafuvu hayo ikisema ni ishara nzuri kwa watu wa kisiwa hicho.
Wanajeshi wa Ufaransa walimkata kichwa Mfalme Toera mnamo mwaka 1897 na fuvu lake kupelekwa nchini humo kama nyara na baadaye likawekwa kwenye makumbusho ya taifa ya historia mjini Paris pamoja na mamia ya mabaki ya watu wengine waliouwawa kwenye kisiwa hicho cha Madagascar kilichoko Bahari ya Hindi.