Ufaransa: Viongozi wa Ulaya wamfikia Trump baada ya mkutano
4 Septemba 2025Viongozi wa Ulaya wamezungumza na rais wa Marekani Donald Trump baada ya mkutano wao wa kilele na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kuhusu dhamana za usalama kwa Kiev endapo kutakuwa na makubaliano ya kusitisha vita ambavyo vimedumu kwa miaka mitatu na nusu sasa, tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.
Mazungumzo ya viongozi hao na Trump, yamefanyika kwa njia ya video, baada ya wakuu wa Ulaya kumaliza mkutano wao mjini Paris Ufaransa, kujadili dhamana za usalama kwa Ukraine.
Dhamana hizo zilizopendekezwa na kile kinachojulikana kama 'muungano wa walio tayari' kuisadia Ukraine lakini ambazo bado hazijawekwa wazi, zinatarajiwa kujumuisha mafunzo ya hali ya juu kwa jeshi la Ukraine pamoja na uwezekano wa kupelekwa kwa wanajeshi kutoka baadhi ya mataifa ya Ulaya kushika doria Ukraine. Pendekezo ambalo limeikasirisha Urusi.
Dhamana hizo ni sehemu ya msukumo wa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuonyesha kuwa Ulaya inaweza kuchukua maamuzi binafsi baada ya rais wa Marekani Donald Trump kuanzisha mazungumzo ya moja kwa moja na rais wa Urusi Vladimir Putinkatika ikulu yake White House.
Mkutano huo wa kilele unaoongozwa kwa pamoja na Macron na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer unalenga kuweka dhamana za usalama endapo kutakuwa na makubaliano ya usitishaji vita, na kupata taswira kamili ya msimamo wa Marekani.
Rutte: Putin hana mamlaka kuamua kuhusu wanajeshi kupelekwa Ukraine
Huku hayo yakijiri Katibu Mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO, Mark Rutte, amesema Urusi haina mamlaka ya kuamua iwapo mataifa ya Magharibi yanaweza kupeleka wanajeshi nchini Ukraine kama sehemu ya dhamana za kiusalama iwapo makubaliano ya kusitisha mapigano yatafikiwa.
"Lakini kwa kila mtu anayefuatilia hili, tafadhali, wanaume na wanawake, raia wa Jamhuri ya Czech na kote barani Ulaya, Kanada na Marekani. Tusijidanganye kuhusu Urusi. Tunajua kile ambacho Putin anajaribu kufanya, na ushahidi uko wazi nchini Ukraine wakati huu tunapozungumza. Na ni huko ambako tishio la muda mrefu lipo, nasikitika," amesema Rutte.
Rutte amesema ikiwa Ukraine inataka vikosi vya kigeni kwa dhamana yake ya usalama na kusimamia mkataba wa amani, ni wajibu wao kuamua na si yeyote yule. Rutte alisema hayo Alhamisi mjini Prague, nchini Jamhuri ya Czech.
Kwenye mkutano uliofanyika Paris Ufaransa, Marekani iliwakilishwa mjumbe wake maalum Steve Witkoff ambaye pia alikutana na Zelensky pembeni.
Zelensky amedai kuwa Putin hana nia ya kusitisha mapiganona kutaka awekewe vikwazo zaidi.
Viongozi wengine kama Rais Zelensky walihudhuria mkutano huo moja kwa moja lakini baadhi akiwemo Starmer walihudhuria kwa njia ya video.
Ulaya haujaungana kikamilifu kuhusu upelekaji vikosi vya amani Ukraine
Wakati wa mkutano Starmer alisema ni muhimu kupiga hatua zaidi kumwekea Putin shinikizoi zaidi, ili kufikia makubaliano ya usitishaji vita. Hayo yamesemwa na msemaji wa ofisi ya Starmer
Muungano wa walio tayari kuisadia Ukraine unajumuisha nchi 30, ikiwemo Canada, Australia na Japan.
Hata hivyo yaonekana bado hakuna uwiano hata miongoni mwa nchi za Ulaya kuhusu dhamana zinazopendekeza.
Hivi karibuni kansela wa Ujerumani Friedrich Merz alisema ni mapema sana kuanza kujadili suala la kupeleka vikosi vya kulinda amani Ukraine.
(AFPE)