Ufaransa haitasita kuiwekea tena Iran vikwazo
29 Aprili 2025Ufaransa imesema haitafikiria mara mbili kuiwekea tena Iran vikwazo vya Umoja wa Mataifa ikiwa mazungumzo yanayonuiwa kutafuta mkataba mpya kuhusu mpango wake wa nyuklia hayatafanikiwa.
Hayo yalisemwa jana usiku na waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot wakati alipozungumza mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Waziri huyo amesema makubaliano yaliyopo sasa yanafika mwisho wiki chache zijazo na ikiwa hakutakuwa na hakikisho juu ya masilahi ya kiusalama ya Ulaya basi hawatasita kutekeleza vikwazo vyote vilivyowekwa miaka kumi iliyopita.
Ufaransa, Uingereza na Ujerumani zinaunda kundi la E3 ambalo ni sehemu ya mkataba uliosaniwa 2015 na Iran unaokamilika mwezi wa Oktoba na zina mamlaka ya kuviweka tena vikwazo.
Iran imeomba mkutano na nchi hizo tatu, ikiwezekana Ijumaa wiki hii mjini Roma, lakini bado hazijajibu.