Udondozi wa magezeti ya Ujerumani tarehe 2-12-2004
2 Desemba 2004Kuhusu kashfa ya unyanyaswaji wa askari iliyoibuka ndani ya jeshi la ulinzi la Ujerumani, gazeti linalochapishiwa mjini Düsseldorf, HANDELSBLATT, limeandika:
"Kwa muda mrefu jeshi la Ulinzi la Ujerumani lilikuwa na sifa ya kujiongoza vizuri, lakini inavyoelekea limeanza kushindwa kuzuia matukio mabaya. Jeshi la ulinzi linalojishughulisha na mambo mengi ya hatari katika nchi za nje, linahitaji uongozi thabiti na usimamizi mzuri zaidi.
Wanajeshi wanapoandamwa na unyama kutoka nje ni rahisi kujisahau na kuanza kuruhusu ukiukwaji wa haki za binadamu baina yao.
Gazeti la HANDELSBLATT linahitimisha rai yake kwa kuandika: Kwa mantiki hii, wakufunzi wanapaswa kupewa mafunzo mengine na lazima wawe wanakaguliwa."
Kuhusu mada hii, gazeti la ESSLINGER ZEITUNG limeandika:
"Kwenye majeshi yote ya ulinzi duniani, nidhamu ya uraiani huwa haifuatwi. Mfumo wa wanajeshi kutii amri na kunyimwa uhuru wa kujiamulia mambo, hupelekea wanajeshi kuwa na tabia ambayo kwenye maisha ya kawaida haiwezi kukubalika. Mafunzo ya wanajeshi lazima yafanyiwe marekebisho, vinginevyo sifa ya jeshi la ulinzi la Ujerumani itavurugwa.
Kwa kumalizia mada hii, gazeti la FRÄNKISCHE TAG kutoka Bamberg, limeandika:
"Jambo la kutilia maanani kwenye kashfa hii ni ukweli wa mambo kwamba, baadhi ya makuruta wanaonyanyaswa na walimu wao, huwa hawalalamiki. Je, huwa wanafanya hivyo kwa kuona haya mbele ya wanaume wenzao? Au, mtu anapovaa magwanda ya jeshi na kuvua nguo za kiraia, hujitolea pia hali ya kujiamini na moyo wa kuthubutu. Ikiwa hivi, basi jeshi la ulinzi litakuwa limeshindwa kujiongoza lenyewe."
Mada ya pili iliyopewa uzito mkubwa kwenye magazeti ya Ujerumani hii leo ni uhalali wa kutaifishwa kwa ardhi ya wananchi wa Ujerumani, uliofanywa kati ya mwaka 1945 na 1945. Mahakama kuu ya masuala ya katiba imehalalisha zoezi hilo.
Gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE limeandika:
"Mahakama kuu imesema wazi kuwa, mageuzi ya sheria ya ardhi hayakuacha mwanya kwa watu binafsi kutoa madai binafsi.
Wajerumani kwa ujumla – kama jamii iliyokumbwa na mkosi wa kuanzisha na kupigana kwenye vita vya pili vya dunia -- lazima iwajibike. Inawezekena kwamba wakati wa kutekeleza mageuzi hayo, makosa yalitendeka. Kwani siyo manazi peke yao ndiyo walipoteza ardhi zao, bali hata wakulima waliokuwa wanapinga utawala wa kinazi.
Kwa upande mwingine uamuzi huu unaipa nguvu serikali kwenye mvutano wake na wajerumani waliolazimishwa kuhama kwa sababu ya vita ambao wanadai kurejeshewa mali zao katika nchi za Ulaya mashariki. Hawa nao ni sehemu ya jamii iliyokumbwa na mkosi wa kuanzisha vita."
Kuhusu mada hii, gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG linahoji:
Je, serikali ya Ujerumani ilinufaika na utaifishwaji wa ardhi kwenye maeneo yaliyokuwa yanakaliwa na Urusi ya zamani? Kwa mara nyingine tena, mahakama kuu ya masuala ya katiba imesema: HAPANA. Mtu akidai alitaifishwa ardhi kinyume cha sheria huko Ujerumani Mashariki, basi madai haya yataendelezwa hata katika sehemu nyingine nyingi."