Udondozi wa magazeti ya Ujerumani
20 Februari 2006Gazeti la Sudduetsche kutoka mjini München laandika: hakuna matumaini ya kuviondoa vikwazo katika mzozo wa mashariki ya kati katika siku chache zijazo. Mpango wa Marekani na Israel kuisambaratisha serikali ya Hamas nchini Palestina kwa kusitisha misaada ya kifedha na kukatiza kulipa ushuru huenda usifaulu ila badala yake unaweza kuwageukia.
Kundi la Hamas halitasambaratika ila litafaulu kupata uhuru wa Palestina kama ilivyotakiwa katika mikataba iliyosainiwa mjini Oslo. Hatimaye kundi la Hamas litakuwa na nguvu zaidi za kisiasa kuweza kusifika na kupata umaarufu katika maeneo yanayokaliwa na Israel.
Mhariri wa gazeti la Trierische Volksfreund kwa maoni yake anasema ikiwa umoja wa Ulaya na Marekani zitaiga mfano wa Israel na kukatiza misaada ya kifedha kwa Palestina, misaada itapatikana kutoka nchi nyengine kama vile Saudi Arabia au Iran, ili kujaza pengo lililoachwa. Matokeo yake itakuwa ni kuchochea siasa kali na kupoteza kabisa uwezekano wote wa kutumia uzoefu wa kisiasa kuutanzua mzozo huo.
Zipo ishara zinazoonyesha kwamba upo uwezekano wa kundi la Hamas kuyatimiza matamshi yake makali. Moja wapo ya ishara hizo ni kusitisha mapigano na Israel kwa miaka kadhaa. Busara na diplomasia sasa vinahitajika na anayetaka kweli kuleta amani katika mashariki ya kati anatakiwa kuwacha kutumia mabishano ya wazi.
Nalo gazeti la Neue Presse la mjini Hannover kuhusu mada hii limeandika: juhudi za kundi la Hamas katika jamii hazilifanyi kundi hilo kuwa na demokrasia ya kweli. Ndio maana ni muhimu misaada ya kifedha ikatizwe. Kwa wakati huu serikali ya Hamas itakosa misaada ya mashirika ya kutoa misaada ya kiutu kwa ujenzi wa nchi, shule na vyuo vikuu.
Kijana wa kipalestina aliye na kazi na anayetaka kujiendeleza kimaisha hatokubali kutumiwa kama mshambuliaji wa kujitoa muhanga maisha. Vivyo hivyo mwanasiasa hatokubali kushiriki katika serikali inayokubali demokrasia shingo upande.
Likitugeuzia mada gazeti la Stuttgarter limeandika juu ya mkutano kuhusu hali ya baadaye ya jimbo la Kosovo unaoanza hii leo mjini Vienna Austria. Kwa mda wa kama miaka saba sasa mataifa mbalimbali yamejishuhulisha sana katika jimbo la Kosovo yakitumia ujanja wa mbuni yakitumai kwa njia moja au nyengine kuweza kukabiliana na hali katika jimbo hilo la Serbia.
Jumuiya ya kimataifa ilifaulu kuuzima mzozo wa Kosovo baada ya mashambulio yake ya mabomu ya mwaka wa 1999 na sasa hatimaye imetambua kwamba mzozo huo hauendelei tena.
Mada ya tatu iliyowashughulisha sana wahariri wa magazeti hii leo ni kuenea kwa homa ya mafua ya ndege. Gazeti la Abendzeitung limewakosoa viongozi wa mkoa wa Meckenburg Vorpommern hapa Ujerumani kwa vile wanavyoshughulikia kuenea kwa homa hiyo.
Viongozi hao walishangaa kufuatia kufariki kwa ndege walioambukizwa homa ya mafua kana kwamba haikujulikana miaka kadhaa iliyiopita kwamba virusi wanaosababisha homa hiyo hatari wangeweza siku moja kuingia Ujerumani.
Jana maelfu ya ndege wanaofungwa nyumbani waliuwawa eti kama hatua ya usalama. Hatua hiyo inazidisha hofu miongoni mwa raia kwani kwa njia moja au nyengine haiwezi kuaminika kwamba vita dhidi ya homa ya mafua ya ndege vitafaulu. Mhariri anagairi kwa kusema pengine maeneo mengine ya Ujerumani bado ni salama.
Nalo gazeti la Leipziger Volkszeitung limezieleza juhudi za kukabiliana na homa ya mafua ya ndege kama janga. Kinachoendelea hivi sasa ni kulaumiana baina ya watu wanaotakiwa kuziongoza juhudi hizo na kupambana na homa hiyo.
Lakini gazeti la Mitteldeutsche kwa upande wake limezisifu juhudi za viongozi katika kuzuia kuendelea kuenea kwa homa ya mafua ya ndege. Viongozi wamewaonya raia wasihofu na kuwatolea mwito wawe na utulivu kwani kuzuka kwa homa hiyo na uchunguzi uliofanywa kwa ndege waliokufa umezusha maswali mengi miongoni mwa wananchi ambayo mpaka sasa bado hayajaweza kujibiwa kwa kina.
Nalo gazeti la Frankfurter Allgemeine limeandika: Homa ya mafua ya ndege inaenea kwa kasi na hakuna kitu kinachoweza kuizuia kuenea. Ndege wengi wamekufa baada ya kuambukizwa homa hiyo na picha zinazoonyeshwa kwenye runinga ni ushahidi wa kuwepo kwa janga kubwa. Kisiwa cha Rügen kazkaini mwa Ujerumani ambako homa hiyo iligunduliwa kimeleezwa kama kisiwa cha kifo.