Udondozi wa magazeti ya Ujerumani
7 Agosti 2006Tukianzia na azimio la Umoja wa Mataifa juu ya mapigano nchini Lebanon, gazeti la Abendzeitung limeandika: baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linataka mapigano yasitishwe, kwanza kundi la Hezbollah likomeshe mashambulio yake mara moja dhidi ya Israel na baadaye Israel ikomeshe harakati zake zote za kijeshi.
Lakini Israel inahisi ina haki ya kuendeleza kampeni ya kujilinda kutokana na ugaidi. Pia hatua ya Lebanon kulikataa azimio hilo inadhihirisha kwamba halitakomesha umwagikaji wa damu.
Gazeti la Tagesspiegel la mjini Berlin linasema bado haijabainika wazi vipi suluhisho la kudumu linavyoweza kufikiwa. Juhudi halisi za Umoja wa Mataifa bado ziko pale pale: Makubaliano ya kupeleka jeshi la kimataifa nchini Lebanon, wapi wanajeshi watakakotoka, kazi yao na juu ya yote muda watakaohitaji.
Mhariri wa gazeti la Kölnische Rundschau katika maoni yake amesema vita vya Lebanon vitamalizika wakati kikosi cha kimatafa kitakapozitengenasha pande zinazopigana. Katika hatua hii hatari ya kisiasa na kijeshi bado Umoja wa Mataifa hauna malengo yaliyo wazi. Idadi kubwa ya raia wa Lebanon wasio na hatia, ambao wanaona nchi yao ikiharibiwa kwa mabomu, hawawezi kuelewa mbinu ya Marekani ya kuchelewesha usitishwaji wa vita.
Gazeti la Süddeutsche Zeitung lina maoni tofauti. Mhariri anasema serikali ya mjini Washington imekuwa ikisita linapokuja swala la kuikosoa Israel. Ama kweli rais George W Bush anatakiwa kutambua kwamba Israel haiwezi kuwachakaza wanamgambo wa Hezbollah kutumia mashambulio yake ya kijeshi, wala kuyazuia mashambulio ya Hezbollah.
Gazeti limesema Ufaransa ilitaka kufikia makubaliano ya haraka ya kuweka silaha chini halafu mazungumzo ya kutafuta makubaliano ya kisiasa yafanyike. Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa bado linatakiwa kuliidhiniisha azimio lililopendekezwa na Ufaransa na Marekani. Mjadala bado uko wazi.
Likitugeuzia mada, gazeti la Rhein Neckar la mjini Heidelberg limesema inaonekana chama cha CDU cha kansela Angela Merkel sasa kimo katika likizo ya kisiasa ya wakati wa kiangazi. Uhusiano wake na chama cha SPD katika serikali ya muungano unalegalega. Angela Merkel ambaye mpaka sasa amefanya machache kuyatimiza matakwa ya chama chake, anatakiwa kufanya mageuzi muhimu, sio tu katika chama cha SPD bali pia katika chama chake cha CDU.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema hakuna kitu kinachoweza kuwa na gharama kubwa katika ulingo wa siasa kama ahadi zisizo na mipaka na zisizoweza kutimizwa. Tangu mwanzoni raia walitabiri ahadi za wanasiasa hazingeleta matumaini makubwa sio tu katika uchumi bali pia mfumo wa afya. Matokeo ni kwamba wanasiasa bado waanamini ushindi wa uchaguzi, huku raia wakiwa wamezitupilia mbali ahadi zilizotolewa wakisema haziaminika.
Hatimaye gazeti la General Anzeiger linasema serikali ya muungano inajikuta katika uhusiano mgumu katika mwaka huu. Kujiondoa kutakuwa hatari kubwa na hakutakuwa na maana yoyote. Kansela Angela Merkel anajua anatakiwa kuongoza muungano wa vyama viwili ambavyo vimekuwa vikipingana katika miongo iliyopita na ambavyo vina idadi karibu sasa ya wafuasi. Serikali ya muungano ina kibarua cha kufanya mabadiliko muhimu itakayoweza kuyaidhinisha kutumia wingi wake wa wabunge.