Udondozi wa magazeti ya Ujerumani
8 Agosti 2006Gazeti la Westdeutsche linasema waziri wa afya wa Ujerumani Ulla Schimdt, anayakashifu wazi makampuni ya bima ya afya hapa nchini. Yanafanya machache kupunguza muda wa wanachama wao kusubiri kukutana na daktari kenye kliniki za kibinafsi. Je makampuni haya yanatakiwa kufanya nini?
Juhudi za madaktari kuliingilia kati swala hili ni jambo linalokishughulisha chama cha madaktari. Na ushahidi wa ubaguzi wa wagonjwa utakuwa vigumu kuuwasilisha. Lakini hilo halimsumbui waziri Schimdt, kwa sababu tayari anazozana na makampuni ya bima juu ya fedha za wanachama.
Gazeti la Rhein Neckar la mjini Heidelberg linayalaumu makampuni ya bima kwa muda mrefu wa kusubiri daktari. Kisheria wagonjwa walio na bima wanatakiwa kusubiri muda mrefu kwa sababu makampuni yao yanalipa fedha kidogo. Madaktari wanasema wagonjwa walio na bima hupata ruzuku wakati wanapotumia fedha zao kununua vifaa. Vifaa kama vile vya kufanyia uchunguzi wa eksirei havingeweza kununuliwa na wagonjwa binafsi. Jambo la sawa lingekuwa kutoa fedha kwa juhudi sawa.
Muhariri wa gazeti la Allgemeine la mjini Mainz anasema ikiwa Bi Schmidt hataki pumzi imuishie katika juhudi za kuleta mageuzi kwenya mfumo wa afya, hatakiwi kuruka kila kikwazo anachowekewa. Nalo gazeti la Berliner Kurier linasema kuna mwokozi mmoja katika matatizo ya mfumo wa afya: Mtu anayelipa mchango wake wa fedha. Mtu hulipa kwa kufikiria.
Kwa mara nyengine tena waziri Schmidt anamtupia mizigo mtu anayechanga fedha, jambo ambalo lilikuwa likifanywa na serikali iliyopita. Hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanywa na serikali ya sasa kuhusu jambo hilo. Ilichokifanya ni kuahidi kupunguza kiwango cha fedha mtu anazotakiwa kulipa kama kodi ya huduma za afya. Lakini sasa kiwango hicho kimetangazwa kupanda. Uwezo kwamba kiwango kinaweza kuongezeka siku za usoni, hauibabaishi serikali.
Mada ya pili inahusu kupanda kwa bei za mafuta kufuatia kufungwa kwa kiwanda kikubwa kabisa cha mafuta nchini Marekani. Gazeti la General Anzeiger la mjini Bonn linasema hali ni tete katika soko la mafuta. Kila habari mbaya zina athari zake; iwe ni matamshi ya rais wa Iran Mohamed Ahamedinajed kuendelea mbele na mpango wake wa kinyuklia au kuvuja kwa mafuta katika mfereji wa mafuta huko Alaska. Yote haya yanapunguza kiwango cha mafuta katika soko.
Hakuna anayetaka kusikia kuhusu athari za kupanda kwa bei na upungufu wa mafuta katika soko. Ukweli ni kwamba wanaotumia mafuta wanahitaji kulipa fedha zaidi.
Naye mhariri wa gazeti la Märkische Oderzeitung la mjini Frankfurt anasema haiwezekani kuondokana na matatizo haya katika kipindi kifupi. Inahitaji muda kutafakari upya juu ya wapi, kiwango na bei za nishati. Hakuna jibu la rahisi. Ipo haja ya kutumia aina nyengine za nishati zitakazohakikisha hakuna upungufu na zitakazoyalinda mazingira, badala ya kulipa dola 100 kwa kila pipa la mafuta.
Mhariri wa gazeti la Mittelbayerische anatukamilishia kwa kusema sisi watumizi wa nishati lazima tutafute mkakati wa siku za usoni. Sio kuhifadhi fedha za kwendea likizo ya pili, kununua simu ya tatu ya mkono au kunua runinga kubwa, ila kununua magari yanayotumia nishati kidogo na vifaa vya kukusanya nishati ya jua. Fedha nyingi zitahitajika lakini vitapunguza uhuru wa makampuni makubwa ya nishati kufanya yatakavyo na kusaidia uchumi wa nchi kukua.