Udondozi wa magazeti ya Ujerumani
9 Agosti 2006Gazeti la Frankfurter Allgemeine limesema Israel haitawaondoa wanajeshi wake kwa hiari kutoka Lebanon kwa wakati huu ijapo waziri mkuu Ehud Olmert hajalikataa moja kwa moja pendekezo la Lebanon kuwapeleka wanajeshi wake kusini mwa nchi hiyo.
Mjini Jeruslaem hakuna anayeamini uwezo na umoja wa jeshi la Lebanon na kundi la Hezbollah, ambalo pia limeuunga mkono mpango huo. Kwa Israel hiyo sio oparesheni ya kijeshi kama ilivyokuwa mwaka wa 1978 wakati wa operesheni ya Litani; mtu anayatilia maanani zaidi mawazo ya maangamizo na tisho la rais wa Iran, Mahamoud Ahamadinejad.
Gazeti la Financial Times Deutschland linaliona pendekezo la Lebanon kama ishara ya matumaini. Mhariri anasema hakuna hali ya utulivu ya kijeshi nchini Lebanon. Hata katika ngazi ya kidiplomasia hakuna dalili za kupatikana suluhisho la kumaliza vita.
Jeshi la Lebanon linaweza kujaza pengo litakalowachwa wakati jeshi la Israel litakapoondoka kusini mwa Lebanon. Linahitaji msaada wa haraka kutoka kwa mataifa ya magharibi kwa kuwa ni kioo cha mivutano ya ndani ya nchi na halijajaribiwa katika vita. Sio mpango unaofaa lakini kwa sasa hakuna mpango mzuri mwingine zaidi ya huo.
Gazeti la Frankfurter Rundschau limesema pendekezo la Lebanon ni fursa mpya. Hata kama jeshi la Lebanon halitaweza kulidhibiti vizuri eneo la kusini, ni wazo zuri likilinganishwa na mawazo mengine, hususan jeshi hilo litakapopata msaada kutoka kwa kikosi cha kimataifa.
Lakini mhariri wa gazeti la Westfalen Blatt la mjini Bielfeld anasema ikiwa pendekezo la kuwatuma wanajeshi wa Lebanon litaungwa mkono na wote basi kwa mara ya kwanza kutakuwa na muelekeo. Pande zote mbili zitahisi zimeshinda. Israel itakuwa imetimiza kile ambacho serikali ya Lebanon haijafaulu kutimiza miaka iliyopita. Mhariri anasema wakati huo huo kuondoka kwa Israel kutakuwa ushindi mkubwa kwa kundi la Hezbollah ambalo halijashindwa.
Nalo gazeti la Tageszeitung la mjini Berlin linasema uamuzi wa serikali ya Lebanon kupeleka wanajeshi wake elfu 15 katika eneo la kusini huenda ikawa hatua itakayosaidia kufikia makubaliano katika mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Ni aibu kwa Umoja wa Ulaya kwamba pendekezo la kwanza kupeleka wanajeshi kusini mwa Lebanon lilitolewa na nchi za kiarabu. Jambo hili linatakiwa kufikiriwa upya kwa haraka mjini Berlin, London na Paris.
Mada ya pili inahusu kupanda kwa bei za mafuta. Gazeti la Westfälische Nachrichten la mjini Münster limesema kupanda kwa bei za mafuta sio kwa sababu ya upungufu. Katika miezi iliyopita iliripotiwa kuwa mapipa milioni 1.8 ya mafuta yalitolewa zaidi ya yale yaliyohitajika. Kwa hiyo mafuta ni mengi lakini kuna tetesi kwamba mabenki, taasisi nyengine za fedha na makampuni ya mafuta yanatumia wasiwasi wa usalama kujipatia faida kubwa.
Naye mhariri wa gazeti la Badische Neue Nachrichten kutoka Karlsruhe anasema sio tu likizo na mgogoro wa Mashariki ya Kati unaosabisha bei za mafuta kupanda, bali pia kufungwa kwa viwanda wa mafuta vya Alaska nchini Marekani kutasababisha bei kupanda zaidi. Wanaotumia mafuta wanalazimika kulipa zaidi sio tu nchini Marekani bali pia barani Ulaya.