Udondozi wa magazeti ya Ujerumani
10 Agosti 2006Kuhusu kampuni ya DocMorris gazeti la Allgemeine kutoka mjini Mainz limesema maduka ya dawa hapa Ujerumani mpaka sasa yanalindwa na sheria inayolinda kumbukumbu za kihistoria na kwa vyovyote ni hayo pekee yanayopatikana ndani ya majengo ya thamani kubwa. Mfumo mzima unafaidi ulinzi wa waundao sheria. Sasa haya yote yanaweza kubadilika.
Kweli ingekuwa hatari kumuogesha mtoto kwa kumwagia maji. Kitu ambacho lakini hakihitajiki tena ni sheria zinazowekea mpaka biashara, na hapo mageuzi ni muhimu. Ikiwa madaktari na mawakili wanalazimika kushindana katika kazi zao, basi pia wauzaji dawa wanatakiwa wayakubali mashindano.
Gazeti la Ostthüringer kutoka mjini Gera linasema ikiwa kampuni ya DocMorris itafaulu katika mzozo wa kisheria, soko la madawa nchini Ujerumani litakabiliwa na mabadiliko yatakayosababisha athari. Sio tu wauzaji madawa peke yao, bali pia makampuni yatakuwa mbioni kufungua maduka ya kuuzia dawa na matawi ya maduka ya dawa. Kuongezeka kwa biashara ya dawa na bei za dawa katika miaka miwili iliyopita kumeonyesha kwamba mashindano zaidi yameleta manufaa kwa wateja na wanaolipa kodi.
Nalo gazeti la Berliner limesema wafanyakazi huria nchini Ujerumani wanalitawala soko. Tayari ni jambo la kushangaza kuona kwamba wataalamu wengi wa dawa hawataki kujua juu ya soko, huku biashara yao ikiwa hatarini. Sababu ni kwamba wagonjwa wanapata ushauri mzuri. Si jambo linaloeleweka kwa nini mfamasia anayefanya kazi katika duka kubwa la dawa atoe ushauri mbaya. Ikiwa kweli wauzaji dawa wanayajali maslahi ya wagonjwa zaidi kuliko pesa, basi wangekubali kuwepo mashindano katika soko.
Mhariri wa gazeti la Kölner Express anasema vyakula hapa Ujerumani vinauzwa kwa bei rahisi kwa sababu kuna mashindano yanayopunguza bei hizo. Gharama za simu zinaendelea kupungua tangu makampuni mengine ya huduma za simu yalipojitokeza kushindana na makampuni yaliyokuwa yamelitawala soko.
Kuhusu bei za dawa mambo yatakuwa tofauti. Ikiwa kutakuwa na mashindano katika biashara ya uuzaji dawa iliyomea mizizi, basi wateja watapumua kwa kutumia pesa kidogo kwani bei zitapungua. Na ikiwa maduka mengi ya dawa yatafunguliwa karibu karibu, baadhi yao yatalazimika kufungwa. Na kwa yale yanayota huduma nzuri zaidi kwa wateja basi bila shaka yataaminika miongoni mwa wateja.
Mada ya pili inahusu hatua ya serikali ya Ujerumani kutaka usalama katika vinu vya nyuklia uchunguzwe baada ya hitilafu kutokea katika kiwanda cha nyuklia cha Forsmark nchini Sweden. Mhariri wa gazeti la Süddeutsche la mjini München amesema usalama wa viwanda vya Ujerumani hautakiwi kuwa swala la kuwashughulisha wanasiasa.
Hitilafu nchini Sweden zimesababisha mjadala kuhusu nyuklia hapa nchini. Mhariri anasema ikiwa kifaa kinachoonyesha vipimo ndani ya kinu cha nyuklia kinaweza kufeli kufanya kazi kwa dakika 20, basi hiyo si hitilafu ya kupuuzwa.
Gazeti la Berliner Kurier limesema ni bahati kwamba Ujerumani haina tatizo kama lile la Sweden katika vinu vyake vya nyuklia. Waziri wa mazingira Sigmar Gabriel anatambua kuna hatari inayoweza kutokea. Ndiyo maana ameamuru uchunguzi ufanywe katika viwanda vya Ujerumani kabla tatizo la umeme kutokea.