Udondozi wa magazeti ya Ujerumani
3 Agosti 2005Gazeti la Suddeutsche linatufungulia ukurasa wa udondozi wa magazeti ya Ujerumani na mzozo wa nuklia wa Iran. Gazeti linasema viongozi wa Iran wanafahamu wazi kwamba malengo yao ya kutaka kutengeneza silaha za nuklia ni jambo linalowatia wasiwasi viongozi wa mataifa ya magharibi.
Ikiwa Iran haitaendeleza shughuli zake za urutubishaji wa madini ya uranium, italazimika kugharimika sana. Serikali ya Tehran lakini ni lazima isipitishe mpaka katika mchezo wake huu wa kubadili msimamo wake kila kukicha kuhusiana na mpango wake wa nuklia.
Ikiwa shughuli za kutengeneza gesi ya uranium zitaanza kweli juma hili katika kiwanda cha Isfahan, basi serikali ya Iran itakuwa imevuka mpaka na kufikia kiwango kisichotakikana. Utengenezaji wa gesi ya uranium ni jambo ambalo linaweza kusamehewa na jamii ya kimataifa, lakini utengenezaji wa gesi hiyo kinyume cha sheria sio jambo linaloweza kusamehewa hata kidogo, limesema gazeti hilo.
Kuhusu mada hii gazeti la Münchener Tageszeitung limeandika juu ya jukumu linalomkabili rais George W Bush kuhusu mabishano kati ya Iran na umoja wa Ulaya juu ya mpango wa nuklia wa Iran. Kufikia sasa ahadi nyingi za kiuchumi zilizotolewa na jumuiya ya Ulaya zimezaa matunda. Kwa kejeli mhariri anasema, Iran sasa inarudia tena mpango wake wa nuklia, hatua ambayo ni ushindi wa kidiplomasia.
Kwa wakati huu pia rais Bush anakabiliwa na kibarua kipya. Taifa hilo la kiislamu linafanya litakalo, hata ijapokuwa linapendelea kupata ahadi zaidi kutoka kwa jumuiya ya Ulaya badala ya kufikishwa mbele ya baraza la usalama la umoja wa mataifa. Kwa maoni yake gazeti linasema mchezo huu una hatari ya maangamizo kwani diplomasia na amani zimo hatarini. Sasa ni lazima umoja wa Ulaya udhihirishe uwezo wake. Hatua ya umoja wa Ulaya kutoa ahadi kwa Iran bila kizitimiza inaweza kumtia matatani rais Bush katika siku za usoni.
Likigeukia mada ya pili gazeti la Südwest Pressse kutoka Ulm limezungumzia kuhusu pesa zinazolipwa watu wasiokuwa na ajira hapa Ujerumani. Mahakama imepitisha kwamba sheria zinaendana na katiba. Kwanza kukubali kwamba haiwezekani tena fedha kugawanywa, ambazo tangu hapo kiwango kimekuwa chini, kutasababisha kuwepo kwa madai mengi. Kwa hiyo itakuwa makosa kuwakaripia mahakimu.
Mahakimu wamelizungumzia jambo hili gumu na wanaweza tu kufanya kazi na sheria zilizopo. Kuzitupilia mbali sheria hizo ni jukumu la mahakama ya katiba ya Ujerumani na kuzibadili ni swala la kisiasa. Kwa kweli hakutarajiwi kufanyika kitu chochote kuhusiana na jambo hili. Tayari sheria zilizopo juu ya msaada wa kijamii mara kwa mara haziwafai raia, kuhakikisha wanapata kiwango kinachoweza kuwasaidia kujikimu maishani.
Gazeti la Rhein-Neckar kutoka mjini Heidelberg kuhusu mada hii limesema mapendekezo ya nne ya Hartz yanaweza kumsababisha kansela Gerhard Schröder kupoteza kazi yake. Ukweli ni kwamba marekebisho ya sheria za utoaji wa msaada wa kijamii zimefaulu tangu hapo jana mbele ya mahakama. Kwa mtu binafsi sheria hizo zinaonekana kuwa ngumu lakini zinafaa.
Msaada wa kijamii kwa watu wasio na kazi unatakiwa kugharimia mahitaji ya kimsingi. Pia lakini fedha hizo zinatakiwa kumuezesha mtu kununua kitanda cha mtoto mchanga na kulipia gharama za bima ya maisha. Gazeti linasema Bwana Oscar Lafontaine kiongozi wa chama cha WASG na kiongozi wa PDS, Gregor Gysi, watafurahia uamuzi kama huu wa kisheria.
Mada ya mwisho ilihusu hali ya wasiwasi iliyojitokeza kwa wajerumani wengi kuhusu malipo yao ya uzeeni. Gazeti la Die Welt kutoka Berlin linasema idadi kubwa ya wajerumani wanaopokea malipo ya uzeeni sio jambo la kushangaza, ila linazusha hali mpya ya wasiwasi. Kadri asilimia 60 ya wajerumani watapokea fedha kidogo kuliko vile wanavyofikiria. Thuluthi moja ya idadi ya wajerumani tayari wanakaribia kustaafu, jambo ambalo bila shaka litazungumziwa sana na wagombea wa kisiasa katika kampeni za uchaguzi ujao.
Gazeti la General Anzeiger kutoka Bonn linatukamilishia kwa kusema kwamba ni lazima mtu ajiwekee akiba yake mwenyewe ya uzeeni. Lakini hata hivyo wajerumani wengi hawawezi kufanya hivyo. Sababu ni nyingi zikiwemo ukosefu wa ajira, kukosekana kwa kazi za kudumu, hali mbaya ya kiuchumi na idadi kubwa ya wanawake wanaolea watoto peke yao. Kwa maoni yake gazeti linasema kwa mtazamo huu, kujiwekea akiba ya binafsi sio suluhisho litakalowasaidia raia wa Ujerumani watakapokuwa wazee.