Udondozi wa magazeti ya Ujerumani
5 Oktoba 2005Gazeti la MANHEIMER MORGEN linaona kutunukiwa kwa tuzo ya nobeli kwa mjerumani ni sifa kubwa kwa sekta ya utafiti hapa nchini.
„Tuzo hii imewakata kauli watu wanaodai utafiti wa hali ya juu nchini Ujerumani hauwezekani. Akiwa Mjerumani wa 24 kutunukiwa tuzo ya Nobeli, mwanasayansi THEODOR HÄNSCH amepatiwa tuzo ya fizikia, tena kwenye mwaka wa kumwenzi mwanasayansi wa kale EINSTEIN.
Jambo la kutia moyo zaidi ni kuwa, mwanasayansi huyu, tofauti na waliomtangulia, hafanyi kazi za ufatiti nchini Marekani, bali anafanya utafiti wake nchini Ujerumani tangu miaka 20 iliyopita.“
Gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN linaongezeka kwa kuandika, tuzo hii ya nobeli ni zana nzuri ya kupambana na watu wanaochafua sifa ya Ujerumani.
„Hii ni nafasi nyingine tena ya kushangilia: Ujerumani imekuwa mshindi wa tuzo ya nobeli. Huu ni ushahidi kwamba sekta ya utafiti wa hali ya juu nchini Ujerumani haiko nyuma.
Pamoja na kwamba hadhi ya vyuo vikuu vya Ujerumani ni ya wastani tu kwa sasa, watafiti hapa nchini wanafanya kazi nzuri.“
Kuhusu mada ya pili iliyozingatiwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani, kuanza kwa mazungumzo ya uanachama kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki, gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE, limeandika:
„Serikali ya Uingereza ilikuwa imepania kwa kila njia, kuondoa vikwazo vyote vilivyokuwa vinahatarisha mazungumzo haya kuanza. Mkakati wa Uingereza umefanikiwa.
Lakini la kujiuliza; Je, mafanikio haya yamepatikana kwa kuitumia CROATIA kama chambo ili kuondoa upinzani wa Austria?“
Kuhusu mada hii, gazeti la LANDESZEITUNG linasema, kufunguliwa kwa mazungumzo ya uanachama kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki kunatoa nafasi nzuri ya kuimarisha demokrasia.
„Kwa mara nyingine viongozi wa nchi za Ulaya wamezozana kwa muda mrefu -- mara hii juu ya uanachama kamili wa Uturuki. Kwa bahati tu, mzozo huu ulikuwa karibu uwe kichekesho.
Kwa upande mwingine, uamuzi waliofikia wa kuanza mazungumzo ya uanachama na Uturuki, unatoa nafasi nzuri ya kuimarisha demokrasia nchini Uturuki.“
Kwa kuhitimisha udondozi wa magazeti ya Ujerumani hii leo, tuangalie yaliyoandikwa na gazeti la ABENDZEITUNG kuhusu kujongeleana kwa Umoja wa Ulaya na Uturuki.
„Mara hii ilikuwa kama mjadala wa bei mnadani. Kwa mara nyingine Austria imeamsha hisia za woga dhidi ya Uturuki. Lakini ghafla ikabadili msimamo wake baada ya chaguo lake CROATIA kupewa nafasi, ya kuanza pia mjadala wa uanachama.
Ni vigumu kusema wazi, utamadumi wa nchi za Umoja wa Ulaya utaathirika au utanufaika vipi kwa kuijongelea nchi ya mashariki.
Hata hivyo hii ni nafasi nzuri kwa Ulaya kuacha kuzingatia masuala ya ulinzi peke yake, bali kuzingatia pia faida inayoweza kupata kwenye upande wa utamaduni.“