Udondozi wa magazeti ya Ujerumani tarehe 8-Septemba-2004
8 Septemba 2004Mvutano kuhusu mjadala wa bajeti ya serikali hapo mwakani, umewakumba hata wahariri wa magazeti ya Ujerumani. Kwa mfano gazeti la FINANCIAL TIMES limeandika:
"Jinsi vyama vikuu vya upinzani vinavyodai, mtu anaweza kusema kuwa takwimu zilizowasilishwa bungeni na waziri wa fedha, Hans Eichel, si za uhakika. Lakini swali lililopo; nani basi ana mpango mzuri zaidi? Kwa upande huu hata vyama vya upinzani havina la kusema, wao wamekalia kumkosoa tu waziri wa fedha, huku wakiendelea kukwamisha kuondolea kwa misamaha ya kodi. Kwa mfano misamaha ya kodi inayotolewa kwa wananchi wanaojenga binafsi za kuishi.
Pendekezo la kupunguza matumizi yote kwa asilimia 5, kama vile alivyopendekeza kiongozi wa chama cha CSU, Edmund Stoiber, haliwezekani kabisa. Kwa kufanya hivyo bajeti ya kilimo na jeshi la ulinzi pamoja na pensheni, itabidi ipunguzwe mno."
Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeongezea kwa kuandika:
"Vyama vikuu vya upinzani, CDU na CSU, havina chaguo jingine zaidi ya kupinga mswada wa bajeti. Hata kama vyama hivi kwa kushirikiana na chama cha FDP vikija madarakani hivi sasa, viongozi wao hawatafanya kitu kingine ili kupunguza madeni, zaidi ya kuuza mali za taifa."
Kinyume na maoni ya wahariri wa magazeti hayo mawili, wahariri wa gazeti la DIE WELT wanamlaumu vikali waziri wa fedha:
"Ikiwa deni la taifa litaendelea kuongezeka kwa karibu Euro bilioni 30, au bilioni 45 kama vinavyodai vyama vya upinzani, ni kichekesho kumsikia waziri wa fedha, akidai bado anaendelea na msimamo wake kupunguza madeni. Ukweli wa mambo ni kuwa hapunguzi tena nakisi ya bajeti ya serikali."
Kuhusu mada hii, gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG limeandika:
"Kuyumbayumba kwa uchumi wa Ujerumani kulichangiwa pia na vyama vya upinzani. Vyama vya upinzani havimtendei haki waziri wa fedha, vinapodai kuwa, yeye peke yake ndiye aliyesababisha Ujerumani ishindwe kukidhi kanuni za muungano wa sarafu ya Euro. Wapinzani wanatakiwa kuwajibika pia, kwa vile wao ndiyo wanaokwamisha mikakati ya kupunguza matumizi. Kwa kutokana na mbinu za kisiasa, vyama vya upinzani vinapinga mpango wa kupunguza ruzuku mbalimbali."
Nalo gazeti la OSTTHÜRINGER ZEITUNG limeandika, mswada wa bajeti ni kama hadithi ya uwongo.
"Nakisi ya bajeti na kuongezeka kwa deni la taifa mwaka huu kunapita hata kiwango kilichowekwa kwenye katiba ya nchi. Kwa mara ya nne mfululizo, Ujerumani itashindwa kutimiza masharti ya kuhakikisha uthabiti wa Euro."
Kwa kumalizia uchambuzi wa leo wa magazeti ya Ujerumani, kuhusu mswada wa bajeti ya serikali bungeni, gazeti la BADISCHEN NEUSTEN NACHRICHTEN limeandika:
"Kinyume na hotuba za bajeti alizokuwa anatoa waziri wa fedha miaka iliyopita, ambapo alitumia zaidi takwimu, mara hii amezungumzia masuala yenyewe na siyo mchezo wa namba.
Kiongozi aliyejipatia sifa nyingi kwa kupunguza matumizi, hivi sasa ameacha hata kutunza vizuri hesabu zake. Inavyoelekea, lengo lake hivi sasa ni kutafuta namna ya kuendelea kutawala na siyo kupunguza madeni ya taifa. Serikali ya Ujerumani ingekuwa kampuni, ingekuwa tayari imekwenda muflisi."