Udondozi wa magazeti ya Ujerumani, tarehe 7-Oktoba 2004
7 Oktoba 2004Kufuatia uamuzi wa tume ya Umoja wa ulaya hapo jana wa kuanza mazungumzo ya uanachama na Uturuki, gazeti la NÜRNBERGER NACHRICHTEN linaona, uamuzi huu umeiweka Uturuki mahali pagumu, kwa kuandika:
"Uturuki imefunguliwa njia ya siku moja kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Ulaya, lakini kabla ya hapo Uturuki imewekewa masharti magumu. Nchi hii ikitaka kuepuka kusitishwa kwa mazungumzo haya, inatakiwa daima, ionyeshe mafanikio kwenye vita dhidi ya rushwa, mateso kwa mafungwa, unyanyasaji wa walio wachache na kuthibitisha kwamba wanajeshi hawana tena uchu wa kuongoza nchi.
Gazeti hili limemamizia kwa kuandika: Uturuki inahitaji muda mrefu ili kutekeleza mambo haya."
Nalo gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU limejaribu kuweka pamoja maoni ya upande unaopinga na ule unaounga mkono uanachama wa Uturuki, kwa kuandika:
"Hapo mwezi wa Disemba viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya watakutana na kuchambua kwa makini mapendekezo ya tume.
Muhimu kwao ni kutafuta njia ambayo itahakikisha mazungumzo ya uanachama wa Uturuki yanakidhi matakwa ya Umoja wa Ulaya na ya Uturuki pia. Uturuki siyo kama nchi nyingine zinazotaka kujiunga na Umoja wa Ulaya. Umoja wa Ulaya umetambua jambo hili na ndiyo maana umejizatiti kwa vigezo mbalimbali."
Gazeti la MITTELDEUTSCHE ZEITUNG limeongezea kwa kuandika:
"Iwapo Uturuki katika kipindi cha miaka 10 hadi 15 ijayo, itajiunga na Umoja wa Ulaya, hii itakuwa ishara nzuri na ya kutia moyo kwa nchi nyingine za kiislamu. Aidha hatua hii itathibitisha kwamba, uislamu unaona na demokrasia kama vile ilivyo kwa uislamu na maendeleo. Kwa upande mwingine uanachama wa Uturuki utatengua ubashiri wa Osama bin Laden kwamba, vita kati ya wakristo na waislamu haviwezi kuepukwa."
Lakini gazeti la DIE WELT kutoka Berlin lina msimamo tofauti; lenyewe linasema:
"Uturuki bado haijafikia hatua ya kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya. Hata hivyo Umoja wa Ulaya umeafiki kuanza mazungumzo na Uturuki. Sasa ni zamu ya Uturuki kuonyesha kama kweli, iko tayari, kutekeleza masharti yote hata kama kiongozi wa nchi hii, bwana Erdogan anayapigia kelele.
Gazeti la DIE WELT limesisitiza kuwa, Uturuki ndiyo inauhitaji Umoja wa Ulaya na siyo kinyume chake. Anayeomba uanachama ni Uturuki na siyo Umoja wa Ulaya."
Tugeukie mada ya pili kwenye uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani leo hii: Shirika la kutengeneza ndege la Marekani BOENG limefungua mashtaka kwenye shirika la biashara duniani dhidi ya mshindani wake mkubwa wa Ulaya, AIRBUS.
Gazeti la FINANCIAL TIMES linasema hizi ni mbinu tu katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu nchini Marekani:
"Mtu akinyimwa haki yake, huwa na sababu ya kufungua mashtaka mahakamani. Lakini shirika la BOENG linafanya hivi kwa vile limepoteza nafasi ya kwanza kibiashara kwa mshindani wake wa Ulaya AIRBUS. Haitegemewi kabisa shirika moja kati ya haya kuibuka kama mshindi kwenye kesi hii. Sanasana kuanzia tarehe 2-Novemba mashirika haya yataendelea na kazi kama kawaida, kwani kampeni za uchaguzi nchini Marekani zinakuwa zimemalizika."