Udondozi wa magazeti ya Ujerumani tarehe 4-Agosti-2004
4 Agosti 2004Kwanza tuangalie yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta. Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linaona kupanda kwa bei ya mafuta kunaweza kuwa na faida pia, kwa kuandika:
"Kuna uwezekano bei ya mafuta kupanda zaidi kuliko ilivyofikia hivi sasa. Hata hivyo hii siyo sababu ya watu kuanza kutapatapa ovyo. Baada ya kufanya marekebisho ya kupungua kwa thamani ya fedha, bei za mafuta hivi sasa, bado ziko chini ya bei za mafuta za miaka ya 70.
Na ikumbukwe kwamba, msukosuko wa kupanda kwa bei ya mafuta wa miaka ya 70 ulikuwa na manufaa pia. Kwani uliwalazimisha watu binafsi na wenye viwanda kubana matumizi ya mafuta adhimu. Kwa mantiki hii, huenda hata wasiwasi wa sasa utakuwa na manufaa. Kwa vyovyote vile, itakuwa jambo baya zaidi, iwapo wenye magari na mameneja wa viwanda hawatatafuta njia ya kukabiliana na njama za nchi za mafuta, OPEC."
Hayo ndiyo maoni ya gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU.
Kuhusiana na soko la mafuta, gazeti la SCHWARZWÄLDER BOTE, limeandika:
"Inavyoelekea kuna mafuta ya kutosha: kupanda kwa kasi kwa bei ya mafuta kunatokana na walanguzi wa mafuta kwenye masoko ya kimataifa. Wasiwasi wa matukio mengine ya ugaidi nao unachangia kwenye kuyumbayumba kwa bei ya mafuta.
Kupanda kwa bei ya mafuta ni sumu kwa ustawi wa uchumi, kwa hiyo, itakuwa vyema, kama wahusika watatumia nafasi hii kutafuta njia za kuacha kutegemea mafuta."
Hayo yameandikwa kwenye gazeti la SCHWALZWÄLDER BOTE.
Sasa tugeukie mada nyingine iliyopewa uzito wa juu kwenye magazeti ya Ujerumani hii leo, ambayo ni mpango mpya wa serikali wa kupunguza misaada kwa watu wasio na kazi.
Gazeti la DIE WELT limeandika:
"Kwa mujibu wa waziri wa uchumi Clemens, mpango mpya utafanya watu wasio na ajira wachelewe kulipwa misaada kwa siku chache tu, ikimaanisha kwamba wahusika hawataathirika sana. Lakini wakosoaji wa mpango huu wanadai, watu wasio na kazi wakipewa msaada huu siku tano tu baadaye, basi wanaweza kufa kwa njaa na pengine kufukuzwa kwenye nyumba za kupanda. Ukweli wa mambo ni kuwa, serikali itabana matumizi kwa kiwango fulani: kwani mwaka 2005 itatoa misaada hii mara 11 tu. Hata hivyo kubadilishwa kwa siku ya kutolewa malipo, hakuna athari kubwa kwa wahusika."
Kinyume na maoni hayo, gazeti la NORDSEE-ZEITUNG limeandika:
"Unyama ulio kwenye mpango mpya wa misaada ya watu wasio na ajira unazidi kuonekana wazi. Kwanza, watu wanaotafuta kazi watalazimishwa kutumia akiba yao baada ya mwaka mmoja. Wahusika hawakukomea hapo, sasa wanataka pia kiwango kinachotolewa na wazazi wasio na kazi kwa watoto wao kila mwezi, kisizidi EURO 750, kinyume chake kitapunguzwa kwenye msaada wa wazazi. Inavyoonekana, wahusika hawaelewi jinsi mpango huu unavyowadhalilisha watu wasio na kazi."
Nalo gazeti la HANDELSBLATT kuhusu mada hii limeandika:
"Mageuzi ya misaada kwa watu wasio na ajira yanalenga kuwapa nafasi mamilioni ya watu wasio na kazi wajitegemee zaidi. Lakini wakosoaji wa mageuzi haya hawazungumzii jambo hili. Wengi wanazungumzia pesa tu zinazotolewa baada ya mpango mpya kuanza kufanya kazi hapo mwaka 2005. Mpango mpya utawabana zaidi watu wa maisha ya kati kuliko watu maskini."
Kwa kumalizia uchambuzi wa magezeti hii leo tuangalie yaliyoandikwa kwenye gazeti la BERLINER KURIER kuhusu mpango mpya wa misaada kwa watu wasio na ajira.
"Hii ni habari nyingine mbaya. Mara hii wahusika wamevipania kuviteketeza vitabu vya benki za watoto. Watu wanazidi kugadhibika. Lakini kwa upande mwingine, serikali inatafuta njia za kuzuia watu kughushi misaada ya ustawi wa jamii. Watu walikuwa na upenyo wa kuficha pesa kwenye akaunti za watoto. Wahusika wamepania sasa kuuziba upenyo huu. Ila wasisahau kwamba, mikakati yote hii inazidi kuwaumiza watu wasio na uwezo."