Udondozi wa magazeti ya Ujerumani, tarehe 30-Januari-2006
30 Januari 2006Kuanzia Jumapili hii kansela wa Ujerumani Bi. Angela Merkel anafanya ziara yake ya kwanza nchini Israel. Ziara hii imegubikwa na hali tete kwenye eneo la mashariki ya kati baada ya kundi lenye kufuata siasa kali la HAMAS kujinyakulia ushindi mkubwa kwenye uchaguzi wa bunge kwenye maeneo ya Wapalestina.
Kuhusu mada hii gazeti la Ujerumani la FINANCIAL TIMES limeandika:
“Ziara ya kansela Merkel huko mashariki ya kati kwenye kipindi hiki cha msukosuko ni ujumbe mahsusi kutoka Ujerumani, kuwa inaunga mkono taifa la Wayahudi. Kimsingi kila serikali mpya ya Ujerumani ina wajibu wa kutambua haki ya kuwepo kwa taifa la Wayahudi na ikibidi hata kutoa msaada wake.
Hata hivyo kwa upande mwingine, kwa kutokana na sababu za kihistoria, Ujerumani haiwezi kushika usukani kwenye ufumbuzi wa matatizo ya mashariki ya kati.”
Nalo gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT limetoa maoni yake kuhusu msimamo wa Israel dhidi ya chama kipya tawala cha Wapalestina:
“Nchini Israel hivi sasa ni kipindi cha kampeni za uchaguzi. Mtu atakayethubutu kusema siku moja atafanya mazungumzo ya amani na chama cha HAMAS, huenda akazuiwa hata kushiriki kwenye uchaguzi ujao wa tarehe 28-Machi.
Hata hivyo inajulikana wazi kuwa, Israel lazima itafute njia ya kushirikiana na HAMAS, kwani hata chama cha PLO kilikuwa kikundi cha kigaidi kabla ya kubadilika na kuwa chama cha kisiasa. Aidha huu ndiyo ukweli wa mambo ambao hawawezi kuukwepa na ndivyo siasa zinavyokwenda kwenye mfumo wa kidemokrasia.
Muhimu tu ni chama cha HAMAS kukanusha matumizi ya nguvu na kutambua haki ya kuwepo kwa taifa la Wayahudi.”
Na kuhusu sasa uwezekano wa chama cha HAMAS kukanusha matumizi ya nguvu, gazeti la NEUE DEUTSCHLAND limeandika:
“Kwa chama cha HAMAS ni wazi kwamba, bila msaada wa nchi za nje, chama hiki hakiwezi kuwa na mafanikio ya kisiasa. Taasis za utawala wa ndani wa Wapalestina zinategemea misaada ya nje -- Ujerumani peke yake inatoa msaada wa Euro milioni 100 kila mwaka.
Hata hivyo gazeti hili linasema; Tishio la misaada ya fedha peke yake siyo suluhu. Sanasana nchi za magharibi zikisitisha misaada kwa wapalestina, hali ya mambo itakuwa mbaya zaidi. Hata kundi la HAMAS linawajibika kuendeleza mikakati ya amani huko mashariki ya kati.”
Makala iliyopewa uzito wa hali ya juu kwenye gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG inahusu pia suala la Palestina.
Gazeti hili limeandika wazi kuhusu mpango wa nchi za magharibi wa pengine kumng’ang’ania rais wa Wapalestina ABBAS ili wasilazimike kukaa meza moja ya wafuasi wa HAMAS – hususani kabla ya kukanusha matumizi ya nguvu.
Gazeti hili limeendelea kwa kuandika:
“Ziara ya Kansela Merkel katika kipindi hiki inafanana na kazi ya zimamoto. Mpango wa nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani uko wazi: kumshauri rais Abbas asikubali kushindwa na kuachia madaraka -- japo inajulikana kuwa amechoka. Hali inakuwa mbaya zaidi kwa vile baadhi ya wafuasi wa chama kilichoshindwa cha FATAH nao hawataki kukubali kushindwa.”
Mada nyingine iliyopewa uzito mkubwa na magazeti ya Ujerumani hii leo ni ajali ya kuvunjika kwa paa la banda la maonyesho nchini Poland na kusababisha zaidi ya watu 66 kuuawa na zaidi ya watu 180 kujeruhiwa.
Gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN linahoji hatua zilizochukuliwa na wahusika kufuatia ajali kama hizi zilizotokea mahali pengine.
“Mara hii paa la ukumbi wa maonyesho limevunjika na kuwaathiri wafugaji wa njiwa waliokuwa wamekutana nchini Poland. Wiki nne zilizopita wahanga wa ajali kama hii walikuwa wanamichezo wa kuteleza kwenye theluji hapa Ujerumani. Na miezi miwili iliyopita wahanga wa ajali kama hii walikuwa waogeleaji huko kaskazini mwa Russia.
Gazeti hili linahoji sasa: Je, ajali zote hizi hazitoshi kuwawajibisha wahusika?
Pia limeandika: Nchini Poland kila mara majengo ya michezo na maduka yanaanguka. Kwa nini watu hawataki kujifunza kwa makosa yaliyopita?