Udondozi wa magazeti ya Ujerumani tarehe 30-08-2004
30 Agosti 2004Baada ya mageuzi tete ya mfumo wa kazi na misaada ya ustawi wa jamii, hivi sasa nchini Ujerumani unaendelea mjadala mwingine wa mageuzi ya mfumo wa bima ya afya. Badala ya wafanyakazi tu kulipa kiwango fulani cha mishahara yao kwenye bima hii, kuna mapendekezo kutoka zaidi kwenye vyama vikuu vya upinzani, kuwa hata watu waliojiajiri na wafanyabiashara wachangie.
Uongozi wa chama tawala cha SPD umejadili jambo hili, lakini badala ya kutoa mapendekezo yake, kansela Schröder amesema, mageuzi haya yaahirishwe mpaka baada ya uchaguzi mkuu hapo mwaka 2006.
Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeandika, hii ni mbinu tu ya kisiasa, na kuendelea kwa kuandika:
"Kansela ametoa msimamo wake kabla hata ya kutoa nafasi kwa uongozi wa chama cha SPD kutoa mapendekezo yao kuhusu bima ya wananchi wote. Kuahirisha mageuzi haya mpaka kwenye uchaguzi mkuu hapo mwaka 2006, kunamaanisha kuwa chama cha SPD kitazungumzia sana jambo hili, lakini hakitatekeleza kitu."
Hivi ndivyo wanavyoona pia wahariri wa gezeti la GENERAL ANZEIGER, wanaposema:
"Jambo moja liko wazi: Inavyoonekana mkutano maalumu wa uongozi wa chama cha SPD kuhusu mageuzi ya bima ya afya, umefikia uamuzi kwamba, hii mada inafaa kutumiwa kwenye mbinu za kurushiana mpira kisiasa.
Pamoja na kwamba chama hiki tangiapo kinapinga pendekezo la vyama vikuu vya upinzani la kuwataka watu wote wachangie kwenye bima ya afya, SPD haisemi hivyo wazi ili iendelee kuvigonga vyama hivyo polepole.
Gazeti la GENERAL ANZEIGER limemalizia kwa kuandika: Hata chama cha SPD kimetoa mapendekezo tete, -- kwa mfano ushuru kwa akiba za wananchi. Mpango huu utawafanya watu watoroshee mali zao katika nchi za nje, na wengine waache kubana matumizi kwa ajili ya akiba ya baadaye."
Gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG limejishughulisha na michezo ya Olimpiki iliyomalizika Jumapili jioni kwa hafla kubwa.
"Kumbukumbu ya mafanikio ya michezo ya olimpiki mjini Sydney ilikuwa mzigo mzito kwa michezo ya Athens. Wagiriki hawakujitahidi vya kutosha kutengua hali hii. Kilichobaki kwa Ugiriki, ni sifa mbaya na michezo iliyogharimu pesa nyingi ambazo haitazirudisha kamwe."
Hata gazeti la HANDELSBLATT lina msimamo huuhuu.
"Michezo ya Olimpiki mjini Athens itaingia kwenye kumbukumbu mbaya kwa kutokana na matukio ya matumizi ya madawa. Hili ni pigo kubwa kwa kulinganisha na michezo ya Olimpiki ya mwaka 2000 mjini Sydney ambayo ilifana sana.
Haya yote ni kinyume kabisa na matangazo ya televisheni ya kamati ya michezo ya Olimpiki ambapo watu mashuhuru kama vile Nelson Mandela na Koffi Annan wanahimiza michezo ya haki na siyo ya udanganyifu.
Wapenzi wa michezo hii ya kimataifa wangependa sana kufuatilia kwa makini idadi ya medali kwa kila nchi, lakini kwa kutokana na hali halisi, hawawezi kuwa na uhakika na washindi. Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2004 mjini Athens imeonyesha kwamba, medali zinazotolewa kwenye michezo ya nguvu, siyo za uhakika."