Udondozi wa magazeti ya Ujerumani tarehe 26-Agosti-2004
26 Agosti 2004Kuhusu ajali ya ndege mbili nchini Russia, gazeti la TAGESSPIEGEL limeandika uchambuzi wake kwa kuuliza swali kwanza:
"Ilikuwa ajali au shambulio? Mpaka sasa haijulikani, ilikuwaje ndege mbili zianguke wakati mmoja huko kusini mwa Russia. Kwa kweli hili ni baa kubwa kwa Russia, baa ambalo linawafanya Wajerumani wakumbuke hata mzozo ulioanza kusahaulika katika maeneo ya Caucasia. Itakumbukwa kwamba, nchini Chechnya kuna kizazi kilichokulia vitani. Kizazi hiki ambacho hakijui kitu kingine zaidi ya vita na hakina matumaini ya maisha mazuri, ndiyo kwanza kinachochea wimbi la vitendo vya kigaidi."
Nalo gazeti la GENERAL ANZEIGER kuhusu mada hii limeandika:
"Ni vigumu kuamini kwamba ugaidi siyo sababu ya ajali za ndege mbili za aina ya Tupelov nchini Russia. Hata kule kukanusha kwa kiongozi wa waaasi wa Chechnya, ASLAN MAS’CHADOW, kwamba hawahusiki na ajali hiyo, siyo ufumbuzi wa mambo, kwani kwenye eneo la Caucasia kuna vikundi vingi vya waasi. Hata mashambulio ya zamani yaliyofanywa na magaidi wa Chechnya hayakupatiwa maelezo ya kutosha."
Kwa kumalizia mada hii ya ajali au shambulio la kigadi nchini Russia, gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG limeandika:
"Kama ilivyokuwa kwenye shambulio la kigaidi kwenye ukumbi wa maonyesho mjini Moskow, taasisi za serikali zilificha ukweli wa mambo kuhusu gesi ya sumu iliyotumiwa. Mara hii pia, taasisi za upelelezi nchini, zinadai kwamba hazijapata ushahidi wowote ule, kwamba ajali hii imesabishwa na magaidi."
Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limejishughulisha na ripoti ya wizara ya ulinzi ya Marekani kuhusu mateso ya wafungwa nchini Iraq:
"Ripoti ya uchunguzi wa mateso ya wafungwa nchini Iraq, kwamba kiini cha makosa hayo ni mpango mzima wa uvamizi wa kivita nchini Iraq, ni pigo kubwa kwa waziri wa ulinzi bwana Rumsfeld. Ripoti hii inasema, vita hivyo havikupangwa vizuri na hapakuwa na wanajeshi wa kutosha. Kwa upande mwingine ripoti hii inavuruga kampeni za uchaguzi kwa raisi Bush. Hasa pale inapodaiwa kwamba, vita vya Iraq havikuwa na mafanikio kwa vile hapakuwa na mipango mizuri baada ya kupatikana kwa amani."
Hivyo ndivyo linavyoona hata gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU, kwa kuandika:
"Mtelezo ulioishia ABU GHRAIBU ulianzia kwenye ikulu ya Marekani. Kwanza kabisa ni kwa vile Rais Bush, kwa uamuzi wake peke yake, aliamua kuacha kufuata makubaliano ya kimataifa ya Geneva kwa wafungwa wa Marekani huko Afghanistan na Guantanamo. Kwa kufanya hivi alifungua mwanya kwa wahusika kukiuka sheria hata nchini Iraq. Rais wa Marekani na waziri wake wa ulinzi ndiyo wanatakiwa kuwajibika kwa makosa yaliyofanywa kwenye jela ya ABU GHARAIB nchini Iraq."
Kuhusu matumani ya kumalizika kwa mzozo mjini Najaf, gazeti la HANDELSBLATT limeandika:
"Ayatollah ALI EL SISTANI huenda ndiyo tumaini la mwisho la kumaliza mzozo wa Najaf na hivyo kuepusha baa kubwa zaidi. Hii ni kwa vile kiongozi huyu wa kidini, mwenye umri wa miaka 73 ameamua kutoa mchango wake kwa kwenda kwenye mji huo mtakatifu.
Lakini, wito wake wa kuwataka wananchi waandamane kuelekea Najaf, una walakini, hasa iwapo atashindwa kumshawishi mshindani wake MUKTADA EL SADR kuafikiana na mpango wa amani."
Nalo gazeti la BERLINER ZEITUNG kuhusu mada hii limeandika:
"EL SISTANI ameitisha maandamano ya washia kwenda Najaf wakalinde maeneo takatifu dhidi ya majeshi ya kigeni. Wito huu unazua matatizo ya ziada kwa wanajeshi wa Marekani.
Inavyoelekea uongozi wa majeshi ya kigeni nchini Iraq hauna washirika wa kutegemea. Viongozi wa utawala wa mpito wanategemea mno ulinzi wa Marekani, kila wanapotoka nje ya maeneo ya ulinzi mjini Baghdad, hujikuta wanahatarisha maisha yao."