Udondozi wa magazeti ya Ujerumani, tarehe 21-09-2005
21 Septemba 2005Gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG limemulika mikakati ya kuwania madaraka ya viongozi wa vyama vikuu vya kisiasa.
„Tangu mwanzoni kansela Gerhard Schröder alitegemea vyama vya kihafidhina vitatengana na Bi. Angela Merkel baada ya kushindwa kupata kura nyingi kama vile walivyotegemea.
Lakini badala yake, kwa lengo la kuonyesha mshikamano, vyama hivi vimemchagua tena Bi. Merkel kuongoza vyama hivi bungeni -- tena kwa kura nyingi zaidi, yapata asilimia 98. Ni vigumu kujua, vyama hivi vitaendelea mpaka lini kumlinda mgombea wao wa ukansela aliyeangushwa vibaya kwenye uchaguzi uliopita.
Kwa upande mwingine ari ya kansela Schröder kuendelea kutawala inaonyesha kama vile alishinda kwenye uchaguzi uliopita. Pengine anafanya hivi ili kuongeza sauti ya chama chake kwenye serikali ya mseto.“
Nalo gazeti la KÖLNER RUNDSCHAU linahoji: „Mshikamano wa vyama conservative kwa Bi Merkel una faida gani?“
„Iwapo chama cha Social Democrats kitaendelea kukwamisha serikali ya mseto ya vyama vikuu, na hapohapo kukizuia chama cha Kijani kuunda serkali ya mseto na vyama vya kihafidhina pamoja na FDP, basi Bi. Merkel atabaki mikono mitupu.
Baadhi ya viongozi wa vyama conservative tayari wameanza kutoa ushauri tete kwa BI. Merkel; yaani badala ya kumjenga wanazidi kumbomoa. Kwa mfano baadhi yao, wametoa pendekezo la kuunda serikali ya uwingi mdogo bungeni.“
Kwa kutokana na mvutano wa kisiasa unaoendelea nchini hivi sasa, gazeti la Heidelberg, RHEIN-NECKAR-ZEITUNG, linasema Ujerumani inahitaji mageuzi.
„Matokeo ya uchaguzi yanawalazimu wanasiasa kuunda serikali bila kujali misimamo ya vyama vyao. Aidha vyama vya kisiasa vinapaswa kuwa tayari kuweka pembeni itikadi zao na kutelekeza wito wa wapiga kura.“
Tukigeukia sasa mada muhimu ya pili kwenye magazeti ya Ujerumani hii leo kuhusu kung’atuka polepole kwa Bwana Joschka Fischer, gazeti la DIE WELT limeandika:
„Bwana Fischer ana wasiwasi na serikali yeyote ile ya mseto kati ya chama cha Kijani na chama cha FDP, hususani yeye akiendelea na kazi yake kama waziri wa mambo ya kigeni.
Kwa hiyo Kansela Schröder amepunguziwa uwezekano wa kushirikiana na chama cha Kijani --- kwani kiongozi huyu pekee ndiye angeweza kukiweka sawa chama cha kijani ili kikubali kushirikiana na chama cha FDP.
Kwa hiyo, siku mbili baada ya uchaguzi mkuu, kuna ishara ya Ujerumani kuongozwa na serikali ya mseto ya vyama vikuu vya kisiasa -- SPD na vyama ndugu vya kihafidhina.“
Kwa kuhitimisha udondozi wa magazeti ya Ujerumani hii leo tuangalie kilichoandikwa kwenye gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG.
„Bwana Joschka Fischer amesema yuko tayari kung’atuka na kubaki na kazi ya ubunge tu, tena kwenye upande wa upinzani.
Lakini huenda akafanya kazi hiii kwa muda tu, kabla ya mwanasiasa huyu hodari kupewa kazi nyingine kwenye Umoja wa Ulaya au Umoja wa Mataifa.
Kwa hiyo kazi ngumu ya upinzani itabidi awaachie wengine. Hatimaye mwanasiasa mashuhuri wa chama cha Kijani aliye na historia tete ameamua kutulia na kuwapisha wengine.“