Udondozi wa magazeti ya Ujerumani, tarehe 20-07-2006
20 Julai 2006Wahariri wa magezeti ya kila siku ya Ujerumani wameandika kuhusu njia za kujinusuru za mgogoro huu. Kwanza wanajiuliza nani au nchi gani inaweza kuzipatanisha pande zinazogombana huko mashariki ya kati.
Gazeti la Berlin TAGESSPIEGEL limeandika, kwa vyovyote vile Marekani haiwezi kufanya kazi hii:
„Hapo zamani Marakani ilikuwa na nafasi nzuri ya kuwa mpatanishi, hasa wakati ule ilipokuwa inapigania haki ya kuwepo kwa taifa la Waisrael. Lakini kipindi hicho kimepita sasa, badala yake maamuzi yote yanapitishwa na viongozi wa kijeshi kwa malengo mengine ya kuilinda Israel. Hali hii imepelekea hata uhusiano wa Marekani na nchi nyingine za mashariki ya kati kudorora. Kuna uwezekano wa Umoja wa Ulaya kuchukua nafasi hiyo, lakini mpaka sasa hili ni pendekezo tu.“
Lakini gazeti la Rostock, OSTSEE-ZEITUNG, linaona Marekani bado ni muhimu katika ufumbuzi wa mzozo huu:
„Bila ya mchango na ushiriki wa dola kuu Marekani, hapatakuwa na amani ya kudumu, wala haitawezekana kupeleka kikosi imara cha Umoja wa Mataifa kulinda amani huko kusini mwa Lebanon. Kwa upande mwingine, Hisbollah wataendelea kujijengea taifa lao ndani ya taifa la Lebanon na hivyo kuendelea kuiponza nchi hii.“
Kuhusu mada hii, gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEIMNE ZEITUNG limeandika:
„Jumuiya ya kimataifa ina msimamo mmoja kuhusu mzozo huu wa kivita; kwa wengi aliyesababisha yote haya ni wanasiasa wenye kufuata msimamo mkali. Kwa upande mmoja kikundi cha Hamas kwenye ukanda wa Gaza, na kwa upande mwingine kikundi cha Hisbollah nchin Lebanon. Lakini msimamo huu unaweza pia kuchochea mzozo wenyewe.
Marekani na Umoja wa Ulaya magharibi zimezitenga nchi za Syria na Iran kwa madai zinachochea ugaidi wa kimataifa. Ili kukabiliana na shinikizo hili, watawala wa Teheran na Damaskus wamekusanya nguvu na kutumia ushawishi wao kuchochea machaguko katika eneo zima la mashariki ya kati.
Amani ya kudumu huko mashariki ya kati itapatikana baada ya mtego kuu kutenguliwa.“
Tugeukie sasa mada nyingine: Waziri wa kazi Franz Müntefering ametoa pendelekezo la serikali kutoa ruzuku ya mishahara ili watu wasio na kazi walio na umri mkubwa zaidi ya miaka 50 waweze kuajiriwa.
Mada hii imemulikwa na magazeti hii leo, ambapo gazeti la NÜRNBERG NACHRICHTEN limeandika:
„Pendekezo la Müntefering la serikali kuwasaidia wazee kupata kazi ni sawa na pendekezo la watu kufanya kazi mpaka umri wa miaka 67 – yote ni mapendekezo yanayolenga mageuzi ya kina kwenye soko la kazi. Mjadala huu utasaidia sana kurekebisha hali ya mambo nchini.“
Lakini gazeti la MÄRKISCHE ODERZEITUNG kutoka Frankfurt limetoa tahadhari kwa limeandika:
„Mpango huu unaweza kutumiwa pia vibaya: makampuni yatapokea ruzuku ya serikali na hapohapo kuendelea kufukuza kazi watu wanaopokea mishahara mikubwa. Haitachukua muda mrefu, walengwa, yaani watu wasio na ajira wanashangaa kuona mpango huu hauwasaidii kama ilivyokusudiwa.“