Udondozi wa magazeti ya Ujerumani tarehe 13-09-2004
13 Septemba 2004Tamko la rais wa Ujerumani, Horst Köhler, kwamba tofauti za kimaisha kati ya mikoa ya mashariki na magharibi itaendelea kuwa hivyo, umezua mtafaruku mkubwa ambao unaonekana hata kwenye safu za maoni ya magazeti nchini.
Gazeti la BERLINER ZEITUNG limeandika:
"Kwa mara ya kwanza mwanasiasa wa ngazi ya juu nchini ametilia mashaka msingi wa muungano wa Ujerumani. Mojawapo kati ya misingi ya muungano huu ni kulinganisha hali za maisha katika nchi nzima.
Mpaka sasa azma hii haijatimizwa, lakini ndiyo mwelekeo. Tofauti za kimaisha ndiyo kiini cha watu wa mashariki kulalamika na kujiona wao ni watu wa tabaka la chini. Mpaka sasa wahusika nchini walikuwa wanakwepa kujihusisha na jambo hili, labda usemi wa Köhler utasaidia."
Kuhusu mada hii, gazeti la DIE WELT, halioni sababu ya watu kuja juu, kwa kuandika:
"Kwamba haiwezekani kuhakikisha hali sawa ya kimaisha nchini kote, ndiyo hali halisi na inaeleweka. Baadhi ya mikoa ya mashariki ina hali nzuri kuliko baadhi ya maeneo katika mikoa ya magharibi. Kuna mambo mengi, kwa mfano kodi za nyumba zinatofautiana sana, hata ndani ya mikoa ya magharibi. Tofauti hizi siyo kitu kibaya: zipo na zitaendelea kuwepo.
Inashangaza kuona watu wanamlalamikia rais Köhler. Inavyoelekea wakazi wa mashariki walikuwa wanangojea upenyo kama huu kuanza kudai kwamba wanapunjwa."
Mada nyingine iliyopewa uzito wa hali ya juu kwenye safu za maoni ya magazeti ya Ujerumani ni madai ya fidia ya bunge la Poland. Pamoja na kwamba, jambo hili limepatiwa suluhu na miaka 60 sasa imepita, tangu vita vilipomalizika, Poland imeanza tena kudai fidia ya vita.
Gazeti la KÖLNISCHER RUNDSCHAU limeandika:
"Ni wazi kwamba hata wabunge wa Poland wanajua kwamba, suala la fidia lilipatiwa ufumbuzi kwenye mkataba wa mwaka 1953. Pia makubaliano ya muungano mpya wa Ujerumani, 2 – kwa – 4, kati ya mataifa mawili ya Ujerumani na madola makuu, nayo yalitoa ufumbuzi wa suala hili.
Kwa mantiki hii, madai ya fidia hivi sasa ni uchokozi tu. Ni sawa na kumwaga mafuta kwenye moto ambao ulikuwa unaelekea kuzima."
Nalo gazeti la HANDELSBLATT limeshangazwa na madai haya na kuandika:
"Bunge la Poland limejitia matatani kwa madai yake ya fidia ya vita. Madai haya hayana msingi. Uthibitisho huu unaonekana kwenye makubaliano ya Potsdam ya mwaka 1945, makubaliano kati ya Ujerumani mashariki ya zamani na Poland ya mwaka 1953, na makubaliano ya ujirani kati ya Ujerumani na Poland ya mwaka 1990.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Poland imepatia kusema kwamba jambo hili lilishamalizika. Uamuzi huu wa bunge la Poland unanuia kufufua uhasama wa zamani na kufanya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili hapo mbeleni kuwa ngumu zaidi."
Nalo gazeti la MAIN POST linahoji kwa kuandika:
"Mtu aliyedhani kwamba uhusiano kati ya Ujerumani na Poland unaelekea kuboreka kama ule wa Ujerumani na Ufaransa, amekatishwa tamaa. Madai ya fidia ya vita ya bunge la Poland yanaonyesha kwamba, makovu bado hayajapona, pamoja na kwamba miaka 65 imepita tangu Ujerumani ilipoivamia nchi hii ya jirani."