Udondozi wa magazeti ya Ujerumani, tarehe 12.06.06
12 Juni 2006Kuhusu tukio la watu watatu kujiua wenyewe – watu wanaoshikiliwa tangu miaka mingi iliyopita na Marekani kwenye kambi ya wafungwa ya Guantanamo Kuba, gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG limeandika:
„Kwa mujibu wa maelezo ya utawala wa Marekani, wafungwa watatu wa kwanza wameamua kujiua.
Tangu zamani inajulikana kuwa maisha ya wafungwa ya kutengwa kwa miaka mingi kwenye kambi hiyo ni magumu. Lakini mkuu wa kambi hiyo, Harry Harris, amesema, wafu hao hawakujali maisha yao wala ya watu wengine. Akaendelea kwa kusema, kitendo cha wafungwa hao kujiua wenyewe, hakitokani na ugumu wa maisha, bali ni namna fulani ya kuendeleza vita dhidi ya Marekani.“
Gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG limeendelea kwa kuandika; Tamko hili linaonyesha jeshi la Marekani bado halielewi kinachoendelea – ni mateso makubwa kuwatenga watu kwa miaka mingi hivyo bila ya kuwafungulia mashtaka. Rais wa Marekani George W. Bush ameharibu sifa yake na sifa ya nchi yake kwa kiwango kikubwa.“
Hata gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG lina msimamo kama huu, ila limeongezea kwa kuandika, Marekani inavyojaribu kutoa maelezo ya tukio hili, inaonyesha kama vile Marekani bado ina wazimu wa kuona inaonewa kila wakati. Tangu shambulio la kigaidi la tarehe 11-Septemba, nchi hii ndiyo kwanza inazidi kuongeza idadi ya maadui.
Kuhusu mada hii, gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU limeandika:
„Tangu muda mrefu inajuliaka wazi kwamba, kambi ya wafungwa ya Guantanamo haikidhi matakwa ya kisheria ya nchi za magharibi. Pamoja na harakati za kupambana na ugaidi wa kimataifa, kuna hitilafu za kimsingi. Kufuatia tuhuma za kusafirisha wafungwa katika nchi za nje kinyume cha sheria na njia tete za kuhoji wafungwa, tukio la wafungwa kujiua wenyewe ni ishara nyingine inayothibitisha hitilafu hizo.”
Gazeti hili limemalizia kwa kuandika: “Hali itaendelea kuwa hivi, mpaka nchi za magharibi zitakapofanikiwa kumbadili rais Bush.”
Tugeukie mada nyingine muhimu kwenye magazeti ya Ujerumani hii leo: Michuano ya kombe la dunia la kabumbu. Mpaka sasa michezo yote inakwenda vizuri, hali ya hewa ni nzuri, magoli yanavutia na mashabiki wanashangilia vizuri.
Hata hivyo dosari inayojitokeza kila mara ni mpango wa rais wa Iran, Ahmedinejad, kutaka kuhudhuria pia kwenye michezo hii. Kiongozi huyu anakana mauaji ya halaiki ya Wayahudi na kutishia kuisambaratisha Israel.
Gazeti la GENERAL-ANZEIGER limeandika:
„Michuano ya kombe la dunia la kabumbu ni nafasi nzuri na ya kipekee kwa Ujerumani kurekebisha sura yake katika nchi za nje. Mamilioni ya watu wanafuatilia kwa makini michuano hii – Wajerumani lazima waonyeshe ukarimu na unyenyekevu wao kwa wageni.“
Na kuhusu rais wa Iran, Ahmedinejad, anayepanga kuhudhuria kwenye michuano hii iwapo timu yake itafika kwenye robo fainali, gazeti la DER TAGESSPIEGEL limeandika:
„Kwa mujibu wa kanuni za kimataifa, si rahisi kumzuia kuingia Ujerumani. Lakini hii ni nafasi ya kumwambia ana kwa ana kuwa amekuja kwenye hafla ya walimwengu kwa marafiki, na yeye hayumo kwenye kundi hili. Wageni wanaokuja hawawezi wote kuwa marafiki.“