Udondozi wa magazeti ya Ujerumani, tarehe 06.04.2006
6 Aprili 2006Kwa mara ya kwanza nchini Ujerumani, ugonjwa wa homa ya mafua kwa ndege umewakumba kuku na bata wanaofugwa kwenye jumba moja katika mkoa wa Saxony. Ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu, hadi sasa zaidi ya kuku na bata 10,000 wameuliwa.
Kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa, gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG limeandika:
„Wanasiasa na wanunuzi wa kuku na bata wanatakiwa kuwa na subira. Kwanza kabisa, pamoja na kuibuka kwa ugonjwa huu kwenye jumba la kufugia kuku kwenye mkoa wa Saxony, mpaka sasa wananchi hawako hatarini.
Pili jambo hili si la kushangaza. Baada ya ndege mwitu kuambukizwa ugonjwa huu, ilikuwa inajulikana kuwa siku moja hata ndege wa kufugwa wataambukizwa viini vya ugonjwa huu.
Gazeti hili limemalizia kwa kuandika:
“Muhimu sasa ni wahusika wote, kuwaua kuku na bata wote wanaohofiwa kuwa na ugonjwa huu. Mpaka sasa hii ndiyo njia pekee ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu.”
Gazeti la NORDKURIER kutoka Neu-Brandenburg limetoa wito kwa wafugaji wa kuku na bata:
“Wafugaji wa ndege kwenye mkoa wa Saxony lazima watekeleze kikamilifu uamuzi wa kuwaua ndege wote, hata kama ni maelfu.
Iwapo mfugaji mmoja tu, kwa kutowajibika au kwa uchu wa pesa au kwa kujifanya ana mapenzi ya kupita kiasi kwa na mifugo yake, anaweza kusababisha balaa kubwa.”
Kwa upande mwingine gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG limetathmini chanzo cha ugonjwa huu kwenye mkoa huo wa kaskazini kwa kuandika:
“Maelfu ya ndege mwitu waliokutwa wamekufa kwenye pwani ya kisiwa cha Rüge, hata karibu na majumba ya kufugia kuku na bata, walikutwa na viini vya homa ya mafua. Ndege mwitu hawa bila shaka wamewaambukiza hata kuku na bata wa wakulima, baada ya kuruhusiwa kutoka nje.”
Mada muhimu ya pili hii leo ni juu ya tatizo la upotovu wa nidhamu kwenye baadhi ya shule hapa Ujerumani. Hivi sasa watu wanajadili hatua zinazofaa kuchukuliwa na jinsi ya kuwajumuisha watototo wa kigeni na wazazi wao kwenye maisha ya kila siku.
Kuhusu shule zinazotumiwa zaidi na watoto wa kigeni, Hauptshule, gazeti la Berlin, TAGESSPIEGEL, limeandika:
“Walimu wa shule hizi hawakulalamika mapema kwani wamezoea au kwa vile wanajua wameachwa peke yao na tatizo hili. Wazazi wa watoto kwenye shule hizi nao hawakulalamika, kwa vile wengi wao wanatoka kwenye jamii zilizozoea kukaa kimnya.
Watu wengine wanafurahi kuona shule hizi bado zipo, kwani zinawaepusha na matatizo kwa vile zinawachukua ya watoto wote watukukutu. Aidha kwa kufanya hivi, asilimia 90 ya watoto wa shule hawakutanishwi na watoto walio na matatizo.”
Kwa kuhitimisha udondozi wa magazeti ya Ujerumani hii leo, gazeti la MITTELBAYERISCHE ZEITUNG limeandika:
“Pengine mkutano wa kilele juu ya mkakati wa kuwajumuisha watoto wa kigeni kwenye jamii ndiyo utaleta ufumbuzi wa mambo.
Kinachotakiwa hivi sasa ni mpango wa muda mrefu utakaowashirikisha washika dau wote, kutoka kwenye serikali kuu, mikoani mpaka kwenye serikali za miji.”