Udondozi wa magazeti ya Ujerumani, tarehe 02-11-2005
2 Novemba 2005Kuhusu mzozo wa ndani ya chama cha Social Democrats, gazeti la WESTDEUTSCHE ALLGEMEINE ZEITUNG limandika:
„Kama kweli chama cha SPD kinataka kuunda serikali ya mseto na vyama ndugu vya CDU na CSU, lazima kiwe na msimamo mmoja; kama kinataka kuwa chama cha upinzani cha mrengo wa kushoto au kama kinataka kushiriki kwenye serikali na kutetea maslahi ya mrengo wa kushoto.
Chama cha SPD kina hali ngumu kwa sasa -- kwanza hakina kiongozi aliye na uwezo wa kuleta mshikamano wa makundi yote ndani ya chama. Na pili chama hiki lazima kiwe na mwelekeo thabiti.“
Kuhusu mada hii gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG limeandika:
„Mstakabali wa serikali ya mseto kati ya vyama vikuu vya kisiasa unategemea zaidi hali ya chama cha SPD. Ili mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto yawe na mafanikio, chama hiki lazima kipate kiongozi mpya na kiwe na msimamo.
Ingawaje kwa upande mwingine haijulikani, kama kiongozi mpya atakuwa na uwezo wa kupítisha maamuzi ya uhakika kama ilivyokuwa kwa kiongozi aliyemtangulia bwana Müntefering.
Mgawanyiko wa ndani ya chama hiki, uliomwangusa hata mwenyekiti wake, unaweza kuendelea hata kufikia kwenye madai ya serikali ya mseto ya vyama vya mrengo wa kushoto.”
Gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN limeandika:
„Chama vya SPD na vyama ndugu conservative CDU na CSU vilianza mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto kwa lengo la kuikwamua Ujerumani. Lakini badala ya kutekeleza azma hii, hivi sasa vyama hivi vimekumbwa na migogoro.
Kwa chinichini viongozi wa vyama hivi wanatafutwa mwanzo mpya ili wakamilishe mazungumzo hayo. Ukweli wa mambo ni kuwa, mpango wa kuunda serikali ya mseto kati ya vyama hivi uko mashakani.“
Utata mwingine wa mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto, ni tamko la mwenyekiti wa chama cha CSU bwana Edmund Stoiber, la kutoshiriki kwenye baraza jipya la mawaziri.
Badala yake anataka kubakia Bavaria kama waziri mkuu. Stoiber anadai, baada ya kuondoka kwa bwana Müntefering, ni vigumu kukiamini chama cha SPD.
Nalo gazeti la BERLINER KURIER limeandika:
„Bwana Stoiber ametumia upenyo wa kwanza kabisa kujitoa kwenye kinyang’anyiro cha kushiriki kwenye serikali mpya ya mseto na kuamua kurudi kwenye mkoa wa Bavaria anaouongoza kwa mafanikio kwa muda mrefu.
Lakini uamuzi huu ungepitishwa na mwanasiasa wa chama cha SPD, Bwana Stoiber angekuwa mtu wa kwanza kulalamika na kumwita mwanasiasa huyo msaliti. Hoja anazotoa kutetea uamuzi wake ni finyu. Alichofanya bila shaka kimempunguzia heba yake kisiasa.“