Udondozi wa magazeti ya Ujerumani tarehe 01-12-2004
1 Desemba 2004Tangu mwaka 1988, tarehe mosi-Disemba ni siku ya Ukimwi duniani.
Kuhusu mada hii gazeti la BERLINER ZEITUNG limeandika:
"Kila mwaka kwenye siku ya Ukimwi duniani, takwimu nyingi za ugonjwa huu usio na tiba husambazwa duniani kote. Hivi sasa walimwengu wanajua kwamba hata Ulaya Mashariki na Asia zinakabiliwa na baa la Ukimwi. Watu wameanza pia kufahamu athari za kushuka kwa matarajio ya muda wa kuishi kwa binadamu hadi kufikia miaka 35 tu. Watu wanajiuliza sasa, wangefanya nini, kuzuia baa hili.
Mpaka sasa hakuna mkakati wa kimataifa wa kupambana na ugonjwa huu kama vile ilivyokuwa kwenye upande wa polio au ndui. Gazeti la BERLINER ZEITUNG limemalizia kwa kuandika: Mafanikio yatapatikana kwa kuongeza mikakati ya kutoa maelezo ya ugonjwa huu, njia za kujikinga na tiba.
Kwa kutokana na hali ya kutojali sana ugonjwa huu, hasa katika nchi za viwanda, gazeti la ESSLINGER ZEITUNG limetoa wito ufuatao:
Vijana wa leo katika nchi za viwanda hawakushuhudia kampeni kubwa za Ukimwi za miaka iliyopita. Hali hii inachangia kwenye hali inayoendelea katika nchi zilizoendelea. Hali kadhalika uamuzi wa baadhi ya mikoa wa kupunguza bajeti ya misaada ya Ukimwi, ni kutoona mbali.
Kama inavyokuwa kila mwaka, hata leo hii, waathirika na wafanyakazi wa vituo vya ushauri wa ukimwi, wanaandamana ili kuwakumbusha wahusika juu ya janga hili.
Gazeti linalochapishiwa Berlin, DIE WELT, limeongezea kwa kuandika:
Licha ya Afrika, hivi sasa Asia ya Mashariki, Uchina na Ulaya ya Mashariki zinazongwa pia na baa la Ukimwi. Nchi ambazo mpaka sasa zinaona aibu kuzungumzia wazi tatizo la Ukimwi na kudhani kuambukizwa kwa ukimwi ni alama ya fedheha, nchi hizi ziko hatarini kushindwa kwenye vita dhidi ya ugonjwa huu. Ili kuepukana na baa hili, nchi hizi lazima zifuate ujasiri wa nchi za magharibi: kujenga demokrasia, uwajibikaji wa kila mtu na maendeleo ya kiuchumi."
Mada nyingine iliyopewa uzito mkubwa kwenye magazeti ya Ujerumani hii leo ni kuongezeka kwa umuhimu wa Umoja wa Ulaya, hususani kwenye upande wa diplomasia.
Gazeti la HANDELSBLATT limeandika:
"Huko Ukraine kuna matumaini sasa ya kurudiwa kwa uchaguzi kwa amani. Iran nayo hatimaye imeafiki kusitisha kwa muda mpango wake wa kuandaa madini ya URANI kwa ajili ya matumizi nyeti. Haya yote yamewezekana kwa upatanishi wa nchi za Umoja wa Ulaya.
Kwa muda mrefu Marekani imekuwa ikizicheka nchi za Umoja wa Ulaya zinapopendekeza kutafuta suluhu ya masuala mbalimbali kwa njia za kidiplomasia na kiuchumi. Umoja wa Ulaya uliopanuka zaidi hivi karibuni, umeanza kutumia ushawishi wake mkubwa wa kiuchumi, hususani katika maeneo ya jirani. Nchi za Umoja wa Ulaya zimetambua uzito wake duniani na zimeanza kuutumia ipasavyo pale inapobidi. Kwa upande mwingine heba ya Marekani kidiplomasia ilitiwa doa na vita vya Iraq.