Udondozi wa magazeti ya Ujerumani leo
13 Julai 2005Halmashauri ya umoja wa Ulaya imetoa onyo kali kwa Ujerumani juu ya nakisi ya bajeti, kwa sababau Ujerumani haijajitolea kikamilifu kulisuluhisha tatizo hilo.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine limeandika; kamishna wa umoja wa Ulaya anayeshughulikia maswala ya fedha, Joaquin Almunia, anafahamu wazi kwamba mkataba wa kuzidhibiti bajeti za mataifa wanachama wa umoja wa Ulaya hautakubalika katika mataifa yote wanachama wa umoja huo. Na sasa kwa makusudi na ujasiri anawageukia waongoza kampeni za uchaguzi wa vyama vyote vya kisiasa hapa nchini Ujerumani, ukiwemo pia muungano wa CDU-CSU, ambao muongozo wao katika uchaguzi haujalizingatia swala hilo.
Kwa mtazamo mwingine tangazo hilo lililotolewa na kamishna wa umoja wa Ulaya linadhihirisha tofauti za maoni ya wanasiasa wa Ujerumani kuhusiana na matumizi ya fedha.
Gazeti la Kölnische Rundschau kuhusu mada hii limeandika; tatizo hili sasa linataka kufanywa kuwa la kawaida na kujadiliwa kila mara. Mtu anajikuta katika matatizo makubwa, kwa kuwa hakuna anayezipokea kwa hofu habari hizo mpya zilizotangazwa mjini Brussels. Ujerumani kwa kweli itaendelea kulaumiwa mwaka huu na hata miaka ijayo ili mradi sheria za umoja wa Ulaya juu ya nakisi ya bajeti zitaendelea kubakia hivyo.
Gazeti limeendelea kunakili kwamba bajeti ya seriklai ya Berlin kwa wakati huu inakiuka mkataba wa kudhibiti bajeti za mataifa wanachama wa umoja wa Ulaya, jambo ambalo linahatarisha thamani ya sarafu ya euro. Na ikiwa Ujerumani haitachukua hatua yoykote kuirekebisha hali hii, halmashauri ya jumuiya ya Ulaya itaichukulia hatua za kisheria Ujerumani, liemeandika gazeti hilo.
Mada ya pili iliyochambuliwa na wahariri ni mabishano juu ya kufanyiwa mabadiliko baraza la usalama la umoja wa mataifa. Gazeti la Tageszeitung kutoka Berlin limesema; katika mkutano wa baraza kuu la umoja wa mataifa juu ya kufanyiwa magaeuzi baraza la usalama la umoja huo, matumaini ya serikali ya muungano wa chama cha SPD na chama cha Kijani wa kutaka Ujerumani ipate kiti cha kudumu katika baraza hilo la usalama, sasa yamefika mwisho. Sasa mataifa ya Afrika yatapata matatizo ya kulaumiwa kwa hatua ya serikali ya Ujerumani kukosa kutathmini barabara.
Ishara za mwanzo za kushindwa kwa juhudi hizi zilianza kujitokeza juma lililopita, wakati baadhi ya viongozi wa serikali ya Berlin walipotabiri kwamba juhudi za Ujerumani kutaka kiti cha kudumu hazingeweza kufua dafu. Hii ni kufuatia upinzani uliongozwa na Itali, Argentina na Pakistan dhidi ya mataifa ya G4, na hakuna mapendekezo yoyote yaliyoweza kutolewa wakati wa mkutano wa baraza kuu la umoja wa mataifa, yakuweza kuliongezea nguvu ombi la Ujerumani.
Gazeti la Westfälische Nachrichten limeandika; kwa vyovyote vile katibu mkuu wa umoja wa mataifa, bwana Kofi Annan, anakabiliwa na shinikizo. Mkutano wa baraza kuu umedhihirisha kwamba umoja wa mataifa sio umoja tena wa mataifa. Ni hali ya kuhuzinisha kwani linalotarajiwa hapa hatimaye ni kufanyiwa mabadiliko baraza la usalama la umoja huo, ambalo ni kitengo muhimu cha umoja huo.
Ni nafasi ya Annan kujaribu kuunganisha umoja huo ambao unaonekana ukikaribia kusambaratika. Umoja huo hauitumii nafasi hii vyema na hivyo swala la kulifanyia mabadiliko baraza la usalama linayumbayumba.
Mada ya mwisho ni juu ya hatua ya chama cha FDP kupinga kupandishwa kwa kodi ya mauzo hapa Ujerumani. Gazeti la Märkische Oderzeitung linasema chama cha FDP kinayo haki ya kupinga kupandishwa kwa kodi hiyo. Lakini ikizingatiwa hali mbaya ya kiuchumi na gharama kubwa ya matumizi ya kijamii, swala hili lazima lifikiriwe kwa umakini.
Kwa upande mwingine chama cha FDP kinapinga kupandishwa kwa kodi hiyo ili kufunika uchi wake wa kutokuwa na mpango wowote juu ya maswala ya kiuchumi katika programu yake ya uchaguzi.
Gazeti la Lübecker Nachrichten laandika hivyo ndivyo tunavyokifahamu chama cha FDP. Lengo lake kubwa ni kuwa katika siasa tu, lakini ukweli kwamba hakuna mtu anayemsikiliza mwenyekiti wa chama Guido Westerwelle hautajwi. Vyama vya mrengo wa kushoto vinazungumzia kuunda muungano mkubwa, na jambo hili litaifanya hali ya chama cha FDP kuwa ngumu.